Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na Waziri wa Nchi-Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo wanakusudia kusitisha uwekezaji uliofanywa Ziwa Babati na kampuni ya watu wa China ya XIN SI LIU mara baada ya kuonekana kwa dosari kadhaa zilizoainishwa na mamlaka zilizo chini ya Wizara hizo.
Hayo yamesemwa na Mawaziri hao leo (10.08.2022) Mkoani Manyara wakati wa mkutano wa majumuisho mara baada ya kwenda kutembelea eneo unalokusudiwa kuwekwa mradi huo na kupokea taarifa kutoka kwenye mamlaka zilizokuwa zikifanya tathmini ya uwekezaji huo.
Akizungumza juu ya aina ya uwekezaji uliotarajiwa kufanyika katika eneo hilo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa kwa mujibu wa Taarifa waliyopokea na hali waliyoiona ufugaji wa samaki kwenye vizimba kwenye eneo hilo la Ziwa hauwezi kuwa na matokeo chanya kwa mwekezaji na utasababisha mgogoro baina ya wananchi na Serikali hivyo amemshauri mwekezaji huyo kuangalia eneo jingine ambalo anaweza kufanya uwekezaji wenye faida kwake na tija kwa Taifa kwa ujumla.
“Kwenye rasilimali yoyote ni lazima yaangaliwe maslahi ya pande zote mbili ambayo ni upande wa mwekezaji na upande wa wanufaika wa uwekezaji huo au wadau wanazunguka eneo la uwekezaji na kazi yetu kama Serikali ni kupima na kuangalia uzito uko wapi zaidi” Ameongeza Mhe. Ndaki.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi-Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa Taarifa iliyotolewa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeainisha athari za kimazingira zitakazotokea kwa upande wa Ziwa Babati kutokana na uwekezaji huo ambapo amewataka wataalam kuendelea kuwashauri wawekezaji juu ya usahihi na usalama wa maeneo wanayokusudia kuwekeza.
Awali akipendekeza kusitishwa kwa uwekezaji huo Mbunge wa jimbo la Babati mjini Mhe. Pauline Gekul amesema kuwa uwekezaji huo utaibua migogoro kwa wananchi wa Wilaya hiyo hasa kutokana na Ziwa hilo kutegemewa na zaidi ya wavuvi 1000 kuendesha maisha yao.
Kampuni ya China ya XIN SI LU ilikuwa inakusudia kufanya uwekezaji wa ufugaji wa samaki kwenye vizimba katikati ya ziwa Babati ambapo ilitarajia kuchukua eneo la ukubwa wa hekari tatu kwa ajili ya shughuli hiyo jambo ambalo limeonekana kuwa na athari ya mazingira na kiuchumi kwa wananchi wanaonufaika na ziwa hilo.
Waziri wa Mifugo na uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akifafanua sababu za kukusudia kusitishwa kwa uwekezaji unaofanywa na kampuni ya China ya XIN SI LIU kwenye Ziwa Babati wakati wa Mkutano wa Majumuisho kuhusu Uwekezaji huo uliofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara leo (10.08.2022), kulia ni Waziri wa Nchi-Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Selemani Jafo.
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madala (katikati) akiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo upande wa Maji baridi Dkt. Iman Kapinga (kushoto) na Afisa Uvuvi Mkuu bi. Pudensiana Panga (kulia) wakisikiliza maelekezo ya Maelekezo ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati wa Mkutano wa Majumuisho kuhusu hatma ya Uwekezaji wa Ufugaji wa vizimba katikati ya Ziwa Babati uliofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara leo (10.08.2022).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni