Nav bar

Jumapili, 14 Agosti 2022

MIFUGO NA UVUVI, TAASISI ZAKE WAIBUKA KIDEDEA NANENANE KANDA YA KATI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi zake wameibuka kidedea katika vipengele mbalimbali vilivyoshindanishwa wakati wa Maonesho ya Nanenane  kanda ya kati yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma kuanzia Agosti 1-8, 2022.


Katika hafla hiyo ya utoaji wa zawadi kwa washindi mbalimbali wa maonesho hayo iliyofanyika jana (08.08.2022) muda mfupi baada ya hotuba ya kufunga maonesho hayo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetangazwa kuwa mshindi wa pili kwenye kipengele cha Wizara za Sekta ya Uchumi na Uzalishaji.


Aidha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) imekuwa kinara kwa upande wa kundi la Taasisi za Utafiti na Mafunzo huku pia ikishika nafasi ya pili katika kipengele cha wafugaji wakubwa wa ng’ombe wa nyama ambapo nafasi ya kwanza katika kipegele hicho imenyakuliwa na Kampuni ya ranchi za Taifa (NARCO) kituo cha Kongwa.


Kwa upande wa Bodi zilizopo chini ya Wizara za kisekta, Bodi ya nyama nchini (TMB) imeshika nafasi ya kwanza mara baada ya kuonekana kufanya vizuri zaidi hasa kwenye utoaji wa huduma kwa wateja ambapo walikabidhiwa zawadi ya kikombe na cheti.


Akitoa salamu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Mifugo Dkt. Charles Mhina mbali na kutoa shukrani zake kwa niaba ya Wizara kwa Wadau wote walioshiriki kuandaa maonesho hayo kwa mwaka huu, amewaasa wananchi wote waliofika na kupata elimu ya ufugaji na uvuvi kwenda kuitumia katika shughuli zao ili waweze kupata tija.


“Tumetoa elimu kubwa kuhusu Uhimilishaji wa Ng’ombe wa nyama na maziwa na mwaka huu kwa mara ya kwanza tumefundisha namna ya kuhimilisha kuku ili kuongeza idadi ya kuku wa kienyeji hasa wale wa jamii ya kuchi ambao hawapatikani kwa urahisi siku hizi” Ameongeza Dkt. Mhina.


Aidha Dkt. Mhina ametumia fursa hiyo kuwaasa wafugaji kote nchini kuhakikisha wanahifadhi malisho ya mifugo na vyanzo vya maji ili kuepuka madhara kwa mifugo yanayoweza kutokea tena kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.


Akizungumzia kuhusu hitaji la mabadiliko katika sekta ya kilimo inayojumuisha ufugaji na Uvuvi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewataka wadau wote wanaojihusisha na sekta hiyo kuhakikisha wanabadilika na kuanza kutekeleza dira ya Serikali ambayo imedhamiria kufanya mapinduzi makubwa kwa upande wa kilimo, Mifugo na Uvuvi.


“Serikali haitaki utumie nguvu nyingi kufuga au kulima afu mwishoni usipate tija na ndio maana inasisitiza ni lazima wakulima, wafugaji na wavuvi waanze kubadilika kutoka kwenye kilimo cha kujikimu na kuingia kwenye kilimo biashara, mfugaji awe na ng'ombe wachache wanaompa tija na sisi tuliopo kwenye mikoa isiyo na vyanzo vya asili vya maji tuangalie tunawezaje kufuga samaki kwa kutumia teknolojia mbalimbali zilizopo” Amesisitiza Mhe. Senyamule.


Aidha Mhe. Senyamule ametoa rai kwa wafugaji wote waliopo mkoani Dodoma kuhakikisha wanashiriki zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kuwavalisha hereni za kielektroniki ambapo amesema kuwa jambo hilo litaisaidia Serikali kupata takwimu sahihi za Idadi ya Mifugo iliyopo nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (kushoto) akikabidhi kombe na cheti kwa Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima baada ya Taasisi hiyo kuibuka vinara kwa upande wa kipengele cha Taasisi za Utafiti na Mafunzo kwenye Maadhimisho ya Maonesho ya Nanenane kanda ya Kati yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Nzuguni jijiji Dodoma kuanzia Agosti 1-8, 2022.

Katibu Muhtasi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Pedaya Lukamya (kulia) akipokea zawadi ya cheti kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule mara baada ya Wizara hiyo kushika nafasi ya pili kwa upande wa Wizara za sekta ya Uchumi na Uzalishaji kwenye Maadhimisho ya Maonesho ya Nanenane kanda ya Kati yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Nzuguni jijiji Dodoma kuanzia Agosti 1-8, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni