Edward Kondela
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inatumia vyema wataalamu waliopo katika wizara hiyo ili kuboresha sekta za mifugo na uvuvi pamoja na kushirikiana na wadau wa sekta binafsi.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo (03.08.2022) katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya wakati alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja hivyo na kufafanua kuwa serikali ina wataalamu wa kutosha hivyo ni lazima kuwatumia ili sekta za mifugo na uvuvi ziwe za kisasa zaidi.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu ijayo atataka kuona Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga ambapo baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi katika Hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha wamehamishiwa huko, wawe na mifugo bora ya kisasa zaidi ili kuepusha wafugaji hao kuhamahama na kuwa na mifugo mingi isiyo na tija.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Dkt. Asimwe Rweguza amemwambia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wizara kupitia Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) inauza madume bora ya ng’ombe kwa Shilingi Milioni Tatu badala ya Shilingi Milioni Tatu na Laki Tano ili wananchi waweze kununua ng’ombe hao na kwenda kuboresha mifugo yao.
Dkt. Asimwe ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, amemwamabia Waziri Mkuu Majaliwa wizara inahakikisha wafugaji wanapatiwa elimu ya ufugaji bora pamoja na kupata malisho bora kwa ajili ya mifugo yao ili mifugo hiyo iwe na tija kwa kutoa nyama na maziwa mengi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla amemwambia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuwa wizara inazidi kuboresha vituo vyake vya ukuzaji viumbe maji ili kuzalisha vifaranga vingi zaidi vya samaki na kuwafikia wafugaji.
Amesema lengo la wizara ni kuzalisha vifaranga vingi vya samaki na kuhakikisha chakula cha samaki kinapatikana kwa wingi na bei nafuu ili wananchi wengi wajikite katika ufugaji samaki kufikia lengo la wizara la kuongeza uzalishaji wa samaki watokanao na kufugwa sambamba na samaki kutoka kwenye maji ya asili.
Katika zira hiyo Waziri Mkuu Majaliwa ameongozana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera
Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa kwa mwaka 2022 yenye kauli mbiu, Kilimo ni Biashara, Shiriki, Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yanaendelea katika maeneo mbalimbali nchini na kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni