Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amevitaka Vyama vya Ushirika vya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi nchini kuwa msaada katika kuleta maendeleo na sio kushiriki kushusha maendeleo ya wadau wa sekta hizo.
Naibu
Waziri Ulega ameyasema hayo leo (07.08.2022) wakati wa siku ya Mifugo na Uvuvi
ya Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja
vya Ngongo mkoani Lindi, ambapo amesema lengo la kuanzishwa kwa ushirika ni
kuwasaidia wanyonge kuwa na nguvu moja itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Vyama
vya Ushirika ni muhimu kwa wafugaji na wavuvi kwani vinasaidia kuwakutanisha
pamoja ambapo wataweza kupata fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo na bima.
Wizara inaendelea kuwahamasisha wafugaji na wavuvi kujiunga kwenye vyama vya
ushirika kwa kuwa ni njia ambayo itawafanya wawe na nguvu moja kwenye maamuzi ya
biashara ya mazao yao.
Naibu
Waziri Ulega pia amewataka viongozi wa Vyama vya Ushirika kufanya kazi kwa kuzingatia
sheria, kanuni na taratibu kwani kumekuwepo na malalamiko mengi kwenye baadhi
ya vyama kutokana na ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji kitu kinachosababisha wakulima,
wafugaji na wavuvi kuilalamikia serikali.
Vilevile
ameendelea kuwasihi wananchi kutumia mazao yatokanayo na mifugo na uvuvi kwa
kuwa ni muhimu katika kujenga na kuimarisha afya. Pia amewashauri watanzania
kuendele kutumia bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao la ngozi kama viatu,
mikanda na mikoba kwa kuwa bidhaa hizo ni bora na zinazalishwa hapa nchini.
Naibu
Waziri Ulega amewasihi wafugaji kuhakikisha wanavisha hereni za kielektroniki
kwenye mifugo yao kama taratibu zinavyotaka kwa kuwa mfumo huo una faida kubwa.
Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira ya wafugaji kwa ujenzi wa
majosho, malambo na uhamasishaji wa utunzaji wa nyanda za malisho na kilimo cha
malisho ya mifugo ili wakati wa kiangazi wafugaji wasiweze kupata tabu. Pamoja
na mambo mengine kwa mkoa wa Lindi, Wizara inajenga Malambo kwenye Kijiji cha
Kimambi (Wilayani Liwale) na Matekwe (Wilayani Nachingwea) ili wafugaji waweze
kupata maji ya kunyweshea mifugo yao.
Aidha, amesema
Wizara hiyo inakusudia kuanza kutoa mikopo kwa vifaa kwa wavuvi ili waendeleze
shughuli zao na hatimaye kuinuka kiuchumi, ambapo pia amesema zipo boti 250 za
kisasa ambazo zitakopeshwa kwa wavuvi. Huku akibainisha kwamba kipindi kirefu
wavuvi wamekuwa wakitumia zana duni za uvuvi na hivyo kuvua kwa kubahatisha
lakini sasa serikali imedhamiria kumsaidia mvuvi kuhakikisha anakwenda kuvua
eneo ambalo samaki wanapatikana.
Pia
Naibu Waziri Ulega amewataka viongozi wa vijiji kuhakikisha wanasimamia Mpango
wa Matumizi Bora ya Ardhi ili maeneo yanayotengwa kwa ajili ya shughuli za
mifugo zisiweze kuingiliwa na watumiaji wengine wa ardhi. Lakini pia amewasihi
wafugaji kuto lisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima kwa kuwa hiyo ni
moja ya chanzo cha migogoro na ikitokea tukio kama hilo serikali itachukua
hatua.
”Wakulima
na Wafugaji ni ndugu kwa kuwa wote wanategemeana, hivyo ni vyema kila mmoja
akaiheshimu kazi anayoifanya mwenzake ili wote kwa pamoja waweze kuendelea na
kujiingizia kipato kutokana na shughuli wanazofanya,” alisema Naibu Waziri
Ulega
Mkuu wa
Wilaya ya Liwale, Mhe. Judith Nguli amesema kuwa kupitia elimu inayotolewa kwenye
maonesho ya nanenane anaamini wakulima, wafugaji na wavuvi watakwenda kutumia
mbinu za kisasa kwenye shughuli wanazofanya, kitu ambacho kitawasaidia kuongeza
tija katika uzalishaji na biashara ya mazao hayo.
Kwa
upande wake Dkt Hasan Mruttu Mkurugenzi Msaidizi Utafiti na Mafunzo amezishauri
Halmashauri kuendelea kuwahamasisha wafugaji na wavuvi kujiunga kwenye vyama
vya vyama vya ushirika ili viwasaidie katika kutetea maslai yao.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo, Dkt. Erastus Mosha amewashukuru viongozi wa Kanda ya kusini kwa maandalizi mazuri waliyoyafanya kwa kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata fursa kubwa kupitia maonesho hayo kukutana na wadau mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni