Na. Edward Kondela
Serikali imesema ipo katika hatua mbalimbali za utafiti wa mifugo ambao utawezesha wafugaji kufuga mifugo yao kwa kutumia virutubisho asilia.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Komba amebainisha hayo kwenye viwanja vya Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya wakati akiwa katika banda la Wizara ya Mifugo na kuelezea faida za mifugo ambayo inazaliwa na kukuzwa hadi bidhaa zake kutumika kwa mtumiaji wa mwisho.
Prof. Komba amesema TALIRI kwa sasa inashirikiana na Kampuni ya Afrint Bio Solution ya nchini Indonesia ambayo inatengeneza bidhaa ambazo hazitumii kemikali yoyote bali virutubisho asilia ambavyo havimhitaji mnyama kutumia dawa wala chanjo yoyote tangu kuzaliwa hadi kukua kwake.
Aidha, amesema kwa sasa serikali inaelekea kupata ufumbuzi wa magonjwa mbalimbali ya mifugo kwa kutumia virutubisho asilia ambavyo havina kemikali yoyote na kwamba vinasaidia ukuzaji wa mnyama kwa haraka na kukuza uchumi kwa mfugaji.
Kwa upande wake Rais wa Kanda ya Afrika wa Kampuni ya Afrint Bio Solution Bw. Paluku Emmanuel amesema wamekuwa wakifanya majaribio ya kufuga kuku bila kutumia chanjo yoyote na kwamba kuku hao wamefikia uzito wa Kilogramu Mbili (2) katika kipindi cha mwezi mmoja na nyama haina mafuta mengi.
Bw. Emmanuel amesema virutubisho hivyo asilia pia vimekuwa vikitoa matokeo mazuri kwa ng’ombe na kuku wa mayai kwa kuongeza uzalishaji wa maziwa na mayai hivyo kuiomba serikali kushirikiana na kampuni hiyo ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo kwa wafugaji kufuga kwa tija pamoja na gharama nafuu.
Baadhi ya wananchi waliofika katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya wamesema wamefurahia kujionea teknolojia mbalimbali za ufugaji ikiwemo ya kuku na mifugo mingine bila kutumia dawa wala chanjo.
Kampuni ya Afrint Bio Siolution ya nchini Indonesia ipo hapa nchini ikishirikiana na serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kufanya utafiti wa virutubisho asilia vinavyotengenezwa na kampuni hiyo kwa ajili ya mifugo ambavyo humsaidia mnyama kuimarisha kinga za mwili na kumzuia kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali.
Rais wa Kanda ya Afrika wa Kampuni ya Afrint Bio Solution ya nchini Indonesia Bw. Paluku Emmanuel (kulia) akizungumza na baadhi ya wananchi waliofika kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, ambapo kampuni ya Afrint Bio Solution kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) inafanya utafiti wa namna ya kufuga mifugo kwa kutumia virutubisho asilia ambavyo vinatengenezwa na kampuni hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni