Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Kattanga amesema lengo la serikali ni kuhakikisha sekta binafsi inawekeza zaidi katika sekta za mifugo na uvuvi ili wananchi waweze kunufaika zaidi kupitia fursa zilizopo katika sekta hizo.
Mhe. Balozi Kattanga amebainisha hayo leo (07.08.2022) alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale, ambapo amesema wizara inatakiwa kuhamasisha zaidi wananchi na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta za mifugo na uvuvi kwa kuwa zina tija zaidi kiuchumi.
Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inatoa elimu zaidi juu ya ufugaji wa mifugo na viumbe maji ili wananchi waweze kujikita katika sekta hizo ambazo ni rahisi katika kukuza kipato chao na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda amemwambia Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Kattanga kuwa wizara imekua kwenye kampeni ya nchi nzima kuhamasisha wafugaji kuiwekea mifugo yao hereni za kieletroniki ili iweze kutambulika na serikali kujua idadi ya mifugo na huduma mbalimbali ambazo zinatakiwa kwa wafugaji.
Pia, amesema licha ya changamoto mbalimbali ambazo wizara imekuwa ikikutana nazo za baadhi ya wafugaji kutoelewa vyema zoezi hilo na kutoonesha utayari wa kuwekea mifugo yao hereni, bado elimu imekuwa ikitolewa kwa kushirikiana na Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT).
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amemwambia Mhe. Balozi Kattanga kuwa wizara tayari ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi wa bandari ya uvuvi katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ikiwa ni mojawapo ya matayarisho kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu.
Dkt. Tamatamah amebainisha kuwa uvuvi wa bahari kuu utaenda sambamba na uwepo wa meli zenye uwezo wa kuvua katika kina kirefu cha bahari pamoja na kuvutia sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kufanikisha uvuvi huo.
Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Kattanga amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Kattanga (kulia) akipatiwa maelezo ya kina juu ya shughuli mbalimbali za Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia mifugo Bw. Tixon Nzunda (katikati) na Katibu Mkuu wa wizara anayeshughulikia uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto), baada ya katibu mkuu kiongozi kufika katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. (07.08.2022)
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi (kushoto) akifafanua kwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Kattanga aina mbalimbali za nyavu zinazoruhusiwa na zisizoruhusiwa kisheria katika uvuaji wa samaki, baada ya katibu mkuu kiongozi kufika katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. (07.08.2022)
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Komba (kushoto) akimuelezea Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Kattanga shughuli mbalimbali za kitafiti ambazo taasisi hiyo imekuwa ikifanya baada ya katibu mkuu kiongozi kufika katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kutaka tafiti za mifugo zilete matokeo chanya. (07.08.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni