Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa Serikali imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya kilimo inayojumuisha pia mifugo na Uvuvi inabadilika kutoka kwenye hatua ya kujikimu mpaka kuwa kilimo biashara.
Mhe. Ndaki ameyasema hayo leo (05.08.2022) wakati wa hotuba yake ya Ufunguzi wa maonesho ya Nanenane kanda ya kati yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma ambapo amebainisha kuwa baada ya Serikali kubaini changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi kama miongoni mwa sababu zilizoshusha ukuaji wa uchumi wa sekta hiyo ilichukua hatua ya kuanza kuboresha miundombinu itakayotumiwa na wakulima, wafugaji na wavuvi hata kwa wakati wote bila kuathiriwa na mabadiliko hayo.
“Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi ya nchi yetu ya mwaka 2021, ukuaji wa uchumi wa kilimo kwa maana ya kilimo mazao, mifugo na uvuvi ulishuka kutoka asilimia 4.9 mwaka 2020 hadi asilimia 3.9 mwaka 2021 na zipo sababu nyingi zillizopelekea hali hiyo ikiwa ni pamoja na janga la ugonjwa wa uviko 19 lakini kubwa kabisa ni upungufu mkubwa wa mvua ulitokea mwaka 2021 na wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kufanya kilimo cha kujikimu ambacho hakitoi mchango wa kutosha kwenye uchumi wao na Taifa kwa ujumla” Amesema Mhe. Ndaki.
Mhe. Ndaki ameongeza kuwa dhamira ya Serikali katika kutekeleza azma hiyo imeanza kuonekana kupitia bajeti za Wizara za Kilimo na ile ya Mifugo na Uvuvi hivyo amewataka wakulima, wafugaji na wavuvi kuunga mkono jitihada hizo za Serikali ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao yote yatokanayo na kilimo, mifugo na uvuvi na mchango wake kwenye pato la Taifa.
“Na kwa kuwa moja ya maeneo ambayo Serikali imeongeza fedha ya kutosha ni eneo la umwagiliaji, tumeamua kufanya shughuli zetu ziende kwa pamoja ili kuwafanya wakulima, wafugaji na wavuvi waweze kuongeza tija zaidi ambapo sasa popote patakapojengwa miundombinu ya umwagiliaji, itawekwa na miundombinu ya kunyweshea mifugo na pale tutakapoweka miundombinu ya kunyweshea mifugo itawekwa na miundombinu ya umwagiliaji” Amesisitiza Mhe. Ndaki.
Akielezea namna sekta yake ilivyojipanga kupokea mabadiliko hayo, Kaimu katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo Dkt. Charles Mhina amesema kuwa miongoni wa njia ambazo sekta yake huzitumia ili kubadili fikra za wafugaji wakati wa maonesho ya Nanenane ni kuandaa maonesho ya paredi ya Mifugo ambayo hujumuisha mifugo kutoka kwenye Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo pamoja na wafugaji binafsi.
“Niwashukuru sana wote mliofika kwenye paredi ya mwaka huu na lengo letu huwa ni kuwafanya wafugaji waachane na ufugaji wa asili na kuingia kwenye ufugaji wa kisasa, nadhani hata nyie mmeona jinsi ng’ombe waliopita mbele yenu walivyo na siha nzuri na mmesikia kiwango chao cha uzito na uzalishaji wa maziwa” Amesema Dkt. Mhina.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa sekta yake imejipanga kuunga mkono juhudi hizo za Serikali za kuhakikisha wanaondokana na uvuaji samaki wa kujikimu kwa kuelekeza nguvu kwenye ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba ambao amebainisha kuwa ndio unaongoza kwa uzalishaji wa samaki wanaofugwa hapa nchini.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (Maji baridi) Dkt. Iman Kapinga (kulia) akimweleza Mgeni Rasmi wa maonesho ya Nanenane kanda ya kati ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto) kuhusu njia wanazotumia kufikisha elimu ya utengenezaji mabwawa ya kufugia samaki kwa wadau wao muda mfupi baada ya Mhe. Ndaki kufika katika eneo inapotolewa elimu hiyo leo (05.08.2022) kwenye maonesho hayo yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Wengine Pichani ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (wa pili kutoka kulia) na nyuma yao ni baadhi ya watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Dkt. Jonas Kizima (kushoto) akielezea namna ya kuhifadhi malisho ya mifugo kwa Mgeni rasmi wa Maonesho ya Nanenane kanda ya Kati ambaye pia ni Mgeni Rasmi wa maonesho ya Nanenane kanda ya kati ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) muda mfupi baada ya Mhe. Ndaki kufika katika eneo inapotolewa elimu ya ukataji na uhifadhi wa malisho ya mifugo kwenye maonesho hayo yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma leo (05.08.2022). Wengine Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (wa pili kutoka kulia), Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa (wa pili kutoka kushoto) na nyuma yao ni baadhi ya watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Mmoja wa wafugaji kutoka Wilaya ya Mpwapwa Bi. Glory Minja (kushoto) akimuonesha Mgeni rasmi wa maonesho ya Nanenane kanda ya kati ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki njia ya uoteshaji wa mbegu za mtama na ngano ili kupata majani yanayoweza kumuongezea ng’ombe kiwango cha Maziwa muda mfupi baada ya Mhe. Ndaki kufika katika banda lake kwenye maonesho hayo yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma leo (05.08.2022). Anayeshuhudia nyuma ya Bi. Minja ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule na wengine nyuma ya Mhe. Ndaki ni baadhi ya watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Meneja wa Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kanda ya kati Dkt. Japhet Nkangaga (kushoto) akimueleza Mgeni rasmi wa maonesho ya Nanenane kanda ya kati ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) kuhusu teknolojia mpya ambazo Taasisi hiyo imewapelekea wadau wake kwenye maonesho hayo muda mfupi baada ya Mhe. Ndaki kufika kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo (05.08.2022). Wengine pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (wa pili kutoka kulia) na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliopo kwenye banda hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni