Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali imedhamiria kuboresha mifugo na kwamba katika mwaka wa fedha 2022/23 wizara kupitia Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) itahimilisha ng’ombe Laki Tatu lengo ni kuwafanya wafugaji kuwa na mifugo bora na yenye tija.
Waziri Ndaki amebainisha hayo (02.08.2022) kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, wakati akipokea msaada wa ng’ombe dume wa kisasa aina ya boran kutoka Ranchi ya Mbogo kwa ajili kuzalisha mbegu na kupandikiza kwa ng’ombe jike kwa njia ya uhimilishaji.
Akizungumza wakati akipokea nyaraka za makabidhiano kutoka kwa Mkurugenzi wa Mbogo Ranchi Bw. Pirmohamed Mulla, Waziri Ndaki amewaomba wadau wengine katika sekta ya mifugo kuunga mkono juhudi za serikali za kutaka kubadilisha mfumo wa ufugaji wa asili ambao umekuwa hauna tija kwa kuwa mifugo hiyo inatoa maziwa na nyama kwa kiwango kidogo sana.
Ameongeza kuwa wafugaji wamekuwa na mifugo mingi ambayo haina tija na kusababisha kuwepo na migogoro na upungufu wa maeneo ya kuchungia hivyo serikali imekuwa ikihimiza ufugaji wa kisasa ambao ni mifugo michache na bora yenye kutoa maziwa na nyama kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mbogo Ranchi Bw. Pirmohamed Mulla, wakati akikabidhi nyaraka za makabidhiano ya ng’ombe dume aina ya boran kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema wameamua kuipatia serikali ng’ombe huyo ili aweze kutumika kuzalisha mbegu nyingi na kuwafikia wafugaji na hatimaye waweze kuboresha mifugo yao.
Bw. Mulla amesema ng’ombe huyo mwenye umri wa miaka mitatu ambaye ana kilogramu 624 ana thamani ya Shilingi Milioni Sita (6) na ana uwezo kustahimili hali ya hewa ya maeneo mbalimbali.
Wakati huo huo, baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki kutembelea mabanda kwenye maonesho ya wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya ametoa tathmini ya maonesho hayo ambapo amesema amebaini wajasiramali wako kwenye hatua za kutaka kufikia malengo yao licha ya changamoto mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo amewataka wataalamu kuanzia ngazi ya taifa hadi kijiji kuwaunga mkono wazalishaji na wajasiriamali ili waweze kufikia malengo yao na watanzania waweze kununua bidhaa zinazotengezwa hapa nchini.
Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kwa mwaka 2022 yenye kauli mbiu Kilimo ni Biashara, Shiriki, Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yamefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango Tarehe 1 Mwezi Agosti Mwaka 2022.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akimfanyia tathmini ng’ombe dume aina ya boran mwenye umri wa miaka mitatu ambaye ana kilogramu 624 na ana thamani ya Shilingi Milioni Sita baada ya serikali kukabidhiwa ng’ombe huyo kutoka Ranchi ya Mbogo, ambapo Waziri Ndaki amesema dhamira ya serikali ni kuhimilisha ng’ombe jike Laki Tatu kwa mwaka wa fedha 2022/23, hivyo ng’ombe huyo atapelekwa katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji kilichopo jijini Arusha kwa ajili ya kuzalisha mbegu. Waziri Ndaki amebainisha hayo baada ya makabidhiano ya ng’ombe huyo yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale yanapofanyika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa jijini Mbeya. (02.08.2022)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akiangalia baadhi ya vyakula vya mifugo vinavyozalishwa hapa nchini na kuwataka wazalishaji wa vyakula hivyo kuhakikisha wanavitangaza kwa wafugaji waweze kuvitumia kwa ajili ya mifugo yao ili ipate virutubisho muhimu na kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama. Waziri Ndaki amebainisha hayo wakati alipokuwa akitembelea mbanda mbalimbali kwenye viwanja vya John Mwakangale yanapofanyika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa jijini Mbeya. (02.08.2022)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), (wa pili kutoka kushoto mstari wa mbele) akisikiliza maelezo ya mmoja wa wafugaji wa samaki waliofika kwenye viwanja vya John Mwakangale yanapofanyika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa jijini Mbeya, namna anavyonufaika na ufugaji huo huku akiiomba serikali kuwasaidia wafugaji kupata chakula cha samaki kwa bei nafuu. Pembeni ya Waziri Ndaki ni Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka katika wizara hiyo Bw. Emmanuel Bulayi. (02.08.2022)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na baadhi ya viongozi wa serikali wa Mkoa wa Mbeya, wazalishaji na wajasiriamali pamoja na wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari juu ya Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya baada ya kuhitimisha ziara ya kikazi ya siku moja katika maonesho hayo ambapo anasema amebaini kuwa wazalishaji na wajasiriamali wanaonesha nia ya kufikia malengo yao hivyo kuwataka wataalamu kuanzia ngazi ya taifa hadi kijiji kuwasaidia ili watanzania waweze kununua zaidi bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. (02.08.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni