Nav bar

Jumamosi, 4 Juni 2022

MWONGOZO KUSAIDIA WAFUGAJI KUPATA MIKOPO WAANDALIWA

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) na tume ya ushirika inatengeneza muongozo utakaoweza kuwasaidia wafugaji kupata mikopo kwenye vikundi vya wafugaji na badae kwenye vyama vya ushirika vya wafugaji Ili wafuge kwa tija bila kuamaama.


Hayo yamesemwa Juni 01, 2022 na Mwenyekiti wa chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Bw. Jeremiah Wambura wakati wa ziara yake mkoani Songwe yenye lengo la kuhakikisha wafugaji wanashiriki vyema katika zoezi la utambuzi wa Mifugo na kujiandaa kuesabiwa ifikapo agosti 2022


Alisema kuwa kuwepo kwa  vikundi vya wafugaji hupelekea kupata elimu, kukopesheka, kushauriwa na  kuweza kushirikiana katika kuchimba visima, kujenga majosho na  kulima malisho na hivyo Mifugo kupata huduma bora kwa kufikiwa na maafisa Mifugo na kupata chanjo na hii hupelekea kufuga kwa tija.


"Hivyo basi chama cha Wafugaji kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi tuna wajibu sasa wa kuhakikisha kuna soko la Mazao yatokanayo na Mifugo, kupeleka vituo vya kukusanyia maziwa kwa kuwa yatakuwa yanazalishwa kwa wingi na kuwa chanzo cha mapato cha eneo husika" alisema Bw. Wambura


Bw. Wambura aliongeza kuwa wafugaji waamasishwe na kujua kwamba tarehe 23/8/2022 kuna zoezi la sensa ya watu na makazi  na hivyo wajiandae kuesabiwa na kutoa taarifa sahihi na kujua ni nani atakayetoa taarifa hizo Ili kuepuka kutoa taarifa mara mbili mbili.


Aidha amesisitiza juu ya utunzaji wa mazingira Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuepuka kupoteza Mifugo kipindi hichi,


Bw. Wambura alisema wafugaji wanapaswa kushiriki kwenye vikao na shughuli za maendeleo kwani  na huko ndio wanakoweza kutatuliwa changamoto zao.


"Tunataka sasa wafugaji waache kufuga kwa kuhamahama jambo ambalo limekuwa likiathiri watoto waliofikia kwenda shule kushindwa na wale waliofauli kushindwa kuendelea na masomo" alisema Bw. Wambura.


Naye Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na haki za wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Annete Kitambi alisema ni wakati wa wafugaji kubadilika na kuanza kuekeza kwenye kulima malisho, kutengeneza majosho, kuchimba mabwawa na kuacha kufuga kwa mazoeya ya kuamaama.


"Chama cha Wafugaji tembeeni kuwaelimisha wafugaji kulima malisho na kuchimba mabwawa Ili kuondokana na adha ya ukame, tuende na kasi ya mabadiliko, na sisi viongozi tuwe chachu ya mabadiliko" alisema Dkt. Annete.


Aidha Afisa Mifugo Mkoa wa Songwe Bw. Omary Kapeyu ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na chama cha Wafugaji kwa kuweza kushirikiana nao kila mara na kuahidi kuendelea kuhamasisha wafugaji kuweza kutambua mifugo yao kwa kuivalisha hereni za kielektroniki na kuwaelimisha juu ya zoezi la sensa ya watu na makazi.

Mwenyekiti wa chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Bw. Jeremiah Wambura (katikati) akiongea wa majumbe walioshiriki kikao kifupi kilichofanyika kwenye wilaya ya mbozi Mkoani Songwe wakati wa ziara yake mkoani humo lengo likiwa ni pamoja na kusisitiza utoaji elimu na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi na kuhakikisha wafugaji wanashiriki vyema katika zoezi la utambuzi wa Mifugo yao Juni 01, 2022.


Afisa Mifugo Mkoa wa Songwe, Bw. Omary Kapeyu akichangia hoja kwenye kikao kifupi wakati wa ziara ya mwenyekiti wa chama cha  wafugaji Tanzania (CCWT) iliyolenga kuhamasisha wafugaji kushiriki vyema katika zoezi la utambuzi wa Mifugo na kusisitiza utoaji wa elimu na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kilichofanyika kwenye Ofisi ya wilaya Mbozi Mkoani Songwe. Juni 01, 2022.


Kaimu Katibu wa chama cha Wafugaji Mkoa wa Songwe Bw. Teobati Kapachi akieleza namna wafugaji  wamejiandaa kuvalisha heremi Mifugo yao kwenye kikao kifupi cha Mwenyekiti wa chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Bw. Jeremiah Wambura wakati wa ziara yake mkoani humo. Juni 01, 2022.


Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Bw. Jeremiah Wambura (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na haki za wanyama Dkt. Annete Kitambi (wa tatu kutoka kulia), Afisa kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Maafisa Mifugo Mkoa wa Songwe, na wajumbe wa chama cha Wafugaji Mkoa na Taifa mara baada ya kikao kifupi kilichofanyika kwenye Ofisi za mkoa huo wakati wa ziara yake Wilaya ya Mbozi  Mkoani Songwe. Lengo likiwa ni pamoja na kuhakikisha wafugaji wanashiriki vyema katika zoezi la utambuzi wa Mifugo yao.Juni 01, 2022


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni