Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa utoaji vibali vya ufanyaji wa biashara za Mifugo, kukata na kuhuisha leseni za wataalam wa Mifugo na vibali vinavyohusu uingizaji, uzalishaji na uuzaji wa vyakula vya mifugo.
Hayo yamesemwa na Afisa Mfawidhi, Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo Kanda ya Mashariki (ZVC) Temeke, Dkt. Mwajuma Chaurembo wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo huo unaojulikana kama “ Mifugo Integrated Management Information System (MIMIS)” yaliyofanyika Jijini Dar es salaam Mei 25, 2022.
Alisema uwepo wa mfumo huo wa kielektroniki utawezesha wadau wote wa Sekta ya Mifugo kupata vibali, kulipa tozo na ushuru wa Serikali pamoja na usajili na Usimamizi wa biashara ya Mifugo na Mazao yake kwa urahisi bila kusafiri kwenda kwenye Ofisi za Wizara.
"Mfumo utawezesha wadau kuwasilisha nyaraka muhimu za kisheria kama vile leseni ya biashara, "Tin number", kitambulisho, anuani ya mdau pamoja na kuomba kibali husika na namna kinavyofanyiwa kazi na Wizara hadi kufikia sehemu ya kufanya malipo," alisema Dkt. Chaurembo
Dkt. Chaurembo aliongeza kuwa watumishi wa Wizara watakuwa na jukumu la kuipitia na kuidhinisha miamala inayowasilishwa na wadau kwa njia ya mtandao.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa upande wa Sekta ya Mifugo, Baltazari Kibola aliainisha maeneo ambayo mfumo huo utayaangazia kuwa ni pamoja na eneo la usafirishaji wa mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi, utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara wa vyakula vya mifugo na usajili wa wadau waliopo chini ya bodi za nyama na maziwa.
“Lakini pia mfumo huu sasa utaanza kuwasajili kwa njia ya mtandao wataalam wa vitu vinavyohusika na utoaji wa huduma za mifugo kama vile maabara au kliniki za mifugo ambazo zinaratibiwa na Baraza la Veterinari nchini na ikumbukwe hapo awali wataalam hawa walikuwa wanalazimika kupeleka maombi yao Wizarani ndipo mchakato wa kuyashughulikia uanze”, aliongeza Kibola
Kwa upande wake Mtaalam wa Mifumo kutoka kampuni iliyoratibu utengenezwaji wa mfumo huo ya Trade Mark East Africa (TMEA), James Temu alisema kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutawafanya wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo kupata huduma zote stahiki popote walipo ndani ya muda mfupi.
Mshauri elekezi kutoka kampuni ya ICTPARK , Bw. Vitus Ng'homi akitoa mafunzo ya namna ya kutumia mfumo wa kielektroniki wa usimamizi na utoaji wa vibali mbalimbali wa Sekta ya Mifugo (MIMIS) kwa washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa four points hotel Jijini Dar es salaam Mei 25, 2022.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali Sekta ya Mifugo unaojulikana kama “ Mifugo Integrated Management Information System (MIMIS)” wakimsikiliza Afisa Mfawidhi kutoka Kituo cha Uchunguzi wa magonjwa ya Mifugo (ZVC) Kanda ya Mashariki - Temeke, Dkt. Mwajuma Chaurembo (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya mfumo huo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa four points hotel Jijini Dar es salaam Mei 25, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni