Na. Edward Kondela
Wadau wa tasnia ya kuku nchini wametakiwa kutafakari namna ya kupunguza gharama za uzalishaji ili mnufaika wa mwisho ambaye ni mlaji aweze kununua kuku kwa bei nafuu na kufikia lengo la kila mtanzania kula nyama Kilogramu 50 kwa mwaka, kulingana na mwongozo wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amebainisha hayo (14.05.2022) katika viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam, wakati wa tamasha la Kuku Choma ambapo amefafanua kuwa wazalishaji wa chakula cha kuku wanatakiwa kutafakari namna ya kupunguza bei za vyakula vya kuku hali kadhalika wazalishaji wa vifaranga vya kuku kupunguza bei za vifaranga ili watu wengi wajitokeze kufuga kuku na kufanya bidhaa hiyo upatikanaji wake uwe wa wingi na bei nafuu.
Waziri Ndaki amesema endapo bei za vyakula vya kuku na vifaranga zitazidi kupanda, mnufaika wa mwisho hataweza kumudu kununua kuku ambapo amesema kwa sasa ulaji wa nyama hapa nchini kwa kila mtanzania ni takriban Kilogramu 15 kwa mwaka kulingana na utafiti uliofanywa na FAO.
“Wadau wote wa nyama kwa ujumla wake tujitahidi kwenda pamoja na walaji wanavyotaka, suala la bei, lakini suala la ubora na masuala mengine ambayo yanavutia wateja wetu ili kuweza kuinua tasnia hii ya nyama kwenye nchi yetu.” Amesema Mhe. Ndaki
Aidha Waziri Ndaki akizungumza katika tamasha hilo la Kuku Choma amewataka wadau wa tasnia ya kuku, kuangalia namna ya kuzidi kuwaongezea thamani kuku wa asili na kuzalishwa kwa wingi ili soko lake lizidi kuwa imara zaidi kama soko la kuku wa kisasa.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Nyama nchini (TMB) Dkt. Daniel Mushi akizungumzia juu ya tamasha hilo ambalo bodi yake imeliratibu, amesema lengo lake ni kuihamasisha jamii kuhusu ulaji wa nyama ambapo kwa kuanzia wameanza na kuhamasisha ulaji wa nyama ya kuku kwa sababu mfugo huo ni rahisi kufuga na kwamba hauhitaji eneo kubwa na pia ni njia mojawapo ya kumuondolea mwananchi katika umasikini.
Pia amesema lengo lingine la tamasha la Kuku Choma ni kuwakutanisha wadau wa tasnia ya kuku ili kubadilishana mawazo na kuulizana maswali ili kuboresha ufugaji wa kuku na kuiongezea thamani tasnia hiyo na hatimaye tasnia ya nyama iweze kukua.
Nao baadhi ya wadau wa tasnia ya kuku walioshiriki katika tamasha la Kuku Choma lililofanyika kwenye viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam wamesema wameridhishwa na tamasha hilo na kuomba matamasha ya namna hiyo yawe yanafanyika mara kwa mara kote nchini ili kuwakutanisha pamoja wazalishaji wa vyakula vya kuku na vifaranga vya kuku, pamoja na wafugaji na watumiaji wa mazao ya kuku ili kuiboresha zaidi tasnia ya kuku.
Wameongeza kuwa tasnia ya nyama nchini inatakiwa kuboreshwa zaidi hususan gharama za uzalishaji kupunguzwa ili wananchi wengi zaidi waweze kula nyama mara kwa mara pamoja na kuiomba serikali kusimamia sheria ili kuondokana na wazalishaji holela wa vifaranga vya kuku ambavyo vimekuwa vikiwasababishia wafugaji hasara kwa magonjwa na kufa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni