Nav bar

Jumatatu, 9 Mei 2022

TUTENGENEZE UHITAJI WA MAZIWA KWANZA-NDAKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameiagiza Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kushirikiana na chama cha Wasindikaji wa Maziwa (TAMPA) kutengeneza uhitaji wa maziwa kwa wananchi badala ya kuendelea kutumia nguvu kubwa sana kwenye kusisitiza uzalishaji na Usindikaji wa bidhaa hiyo.


Mhe. Ndaki ameyasema hayo leo (05.04.2022) kwenye mkutano wa Chama cha Wasindikaji wa Maziwa nchini (TAMPA) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) jijini Dar-es-salaam ambapo amezitaka pande hizo kuhakikisha zinapata suluhu ya changamoto ya kiwango kidogo cha matumizi ya bidhaa hiyo nchini.


"Hebu jiulizeni tu kwa mfano maziwa yakakosekana siku nzima hapa Tanzania kuna watu wataandamana kama ilivyo kwa bidhaa nyingine? Kwa sababu inawezekana tunatumia nguvu kubwa kusisitiza uzalishaji na usindikaji wakati hakuna uhitaji wa bidhaa hiyo hapa kwetu" Amesisitiza Mhe. Ndaki.


Mhe. Ndaki amesema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha bidhaa hiyo inawasaidia wafugaji na wasindikaji waliopo hapa nchini kwa kuanza na soko la ndani hivyo ni lazima Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi wahakikishe linakuwa la uhakika.


"Katika kuhakikisha tunawalinda Wasindikaji na Wazalishaji wa maziwa wa ndani, Sisi kama Serikali tutaendelea kutoza kiasi cha shilingi 2000 kwa kila pakiti ya Maziwa yanayoingia kutoka nje na hatuwezi kuiondoa kabisa labda tuipunguze kidogo kama tutalazimika kufanya hivyo" Ameongeza Ndaki.


Kuhusu wingi wa Tozo zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa Maziwa yanayozalishwa na kusindikwa hapa nchini, Waziri Ndaki amesema kuwa Serikali itaendelea kuondoa tozo kwenye bidhaa mbalimbali zinazotumika kwenye shughuli za uzalishaji na usindikaji wa Maziwa hapa nchini.


"Nimesikia malalamiko  hapa kuwa yale malori yanayotumika kusafirishia maziwa yanatozwa utitiri wa kodi mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinawakwamisha kufanya shughuli zenu hivyo na hili tutaenda kuangalia namna ya kuliweka sawa ili lisiwe kikwazo kwenu" Amesisitiza Ndaki.


Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Dkt. George Msalya amekiri kuwa mchango wa tasnia ya Maziwa kwenye pato la Taifa bado upo chini ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.


"Mpaka sasa Tasnia yetu inakuwa kwa asilimia 2.3 na mchango wake kwenye pato la Taifa ni asilimia 2 kwa mujibu wa takwimu zilizopo wakati wenzetu Kenya wanachangia asilimia 5 na Uganda na Rwanda nao wanakuja kwa kasi kubwa hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya" Amesema Dkt. Msalya.


Naye mmoja wa wasindikaji wa Maziwa nchini kutoka Kiwanda cha Nronga kilichopo Siha Mkoani Kilimanjaro Bi Hellen Usiri amebainisha kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni uwepo wa wauzaji maziwa wasio rasmi ambao hununua maziwa kwa mfugaji kwa bei kubwa ikilinganishwa na ile inayotolewa na viwanda vya kusindika bidhaa hiyo.


"Hawa wenzetu hawalipi kodi na hawana gharama yoyote ya uchakataji ndio maana wanauza kwa bei wanayotaka wao hivyo nashauri wafanyabiashara hao wa mitaani wajiunge kwenye vyama vya ushirika ili maziwa wanayouza yatoke kwenye vyama hivyo yakiwa salama kabisa tofauti na sasa ambapo maziwa mengi yanayouzwa mtaani si salama" Amesisitiza Bi. Usiri.


Kikao cha leo ni mwanzo wa vikao vitakavyofanyika mara kwa mara kati ya Wizara, Taasisi zake na wadau wake ili kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau hao.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni