Nav bar

Jumatatu, 9 Mei 2022

TUTAJENGA MAZINGIRA WEZESHI KWA WATAFITI WA MIFUGO - NZUNDA

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Bw. Tixon Nzunda amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa Wataalam wa utafiti wa magonjwa ya mifugo ikiwemo kuwapatia vibali vinavyohitajika ili kurahisisha utendaji wa kazi zao.


Aliyasema hayo jijini Dodoma Aprili 5, 2022 alipokutana na timu ya Wataalam wa utafiti kutoka SUA na Shirika la Kimataifa la Denmark la ICARS, linaloshughulika na afya za wanyama na binadamu.

Akiongea na Wataalam hao Nzunda alisema serikali itawezesha mazingira yote ya ufanyaji tafiti nchini huku akihimiza kuwa wizara itashirikiana kwa karibu na watafiti ili kuhakikisha maadili ya kisayansi katika ufanyaji utafiti yanazingatiwa ipasavyo.


Kwa upande wake, Mtafiti Kiongozi wa Miradi hiyo kutoka SUA, Prof. Robinson Mdegela wakati akiwasilisha taarifa yao ya miradi  kwa Katibu Mkuu huyo alisema kuwa kumekuwa na matumizi makubwa ya dawa hususan antibiotiki kwenye ufugaji wa kuku wa kisasa kama njia ya kukabiliana na magonjwa ya kuku kwa sababu ya uchanjaji hafifu na kutokuzingatia njia za ufugaji bora hali ambayo imepelekea uwepo wa mabaki mengi ya dawa kwenye nyama na mayai ya kuku.


Aliongeza kwa kusema kuwa kufuatia uwepo wa changamoto hiyo wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameandika maandiko mawili (2) ya miradi ya kutafiti juu ya uwezekanao wa kutumia njia za usafi kwenye mabanda ya kuku na kuchanja kuku ili kudhibiti magonjwa ya kuku na kupunguza matumizi ya madawa hizo. 


Katibu Mkuu, Nzunda  wameipokea miradi hiyo kwa furaha kwa sababu ni miradi ya kwanza kutekelezwa Barani Afrika na matokeo ya utafiti huo yatasaidia watu wengi kufanya ufugaji salama na kupunguza matumizi mengi ya dawa.


“Tutahakikisha matokeo ya utafiti yatakayopatikana  yanakwenda kutolewa kwa umma ili waweze kuyatumia, na upande wa serikali yatatumika kuandaa mifumo ya kiutawala ndani ya sekta ya mifugo kwa maana ya kuanzisha sera, sharia na miongozoz ya utumiaji wa matokeo ya utafiti huo”, alisema Nzunda


Aidha, alilishukuru shirika la Kimataifa la ICARS la Denmark kwa kukubali kutenga kiasi cha Dola za Kimarekani 564,699 kwa ajili ya kufadhali miradi hiyo miwili kwa miaka mitatu (3) kuanzia Mwezi Mei 2022 mpaka Mei 2025 huku akisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za matumizi hayo ya dawa kwa walaji lakini pia itawapunguzia mzigo wa gharama wafugaji wengi wa kuku hapa nchini.


Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka Shirika la ICARS, Helle Engslund Krarup aliishukuru serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi kwa kuruhusu miradi hiyo kutekelezwa hapa nchini huku akisema kuwa watahakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa mafanikio.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni