Nav bar

Jumanne, 24 Mei 2022

RASILIMALI ZA UVUVI BAHARI KUU KULINDWA KISAYANSI

 Na Mbaraka Kambona, Dodoma


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amekutana na Mshauri Mwandamizi wa Kampuni ya CS-Group kutoka Paris, Ufaransa, Bw. Hakim Kachetel kuona namna serikali inaweza kushirikiana na kampuni hiyo katika kulinda rasilimali za uvuvi katika ukanda wa bahari kuu hapa nchini.

Dkt. Tamatamah alikutana na Mshauri huyo mapema leo ofisini kwake jijini Dodoma ambapo Bw. Kachetel alipata fursa ya kueleza shughuli za kampuni hiyo ikiwemo kutengeneza mifumo ya mawasiliano ya kiusalama inayoweza kutumika kulinda rasilimali za uvuvi dhidi ya uvuvi haramu.

Aidha, Dkt. Tamatamah alisema kuwa ujio wa kampuni hiyo ni matokeo ya ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini ufaransa ambapo moja ya maeneo waliyokubaliana kushirikiana baina ya nchi ya Tanzania na Ufaransa ni eneo la uchumi wa buluu hasa ulinzi wa rasilimali za uvuvi.

Alifafanua kuwa eneo la ukanda wa bahari kuu nchini Tanzania ni mkubwa sana wenye takriban kilometa za mraba 223,000 hivyo sio rahisi kulilinda lote, lakini kupitia teknolojia hiyo uwezekano wa kulisimamia eneo hilo utakuwa mkubwa.

“Teknolojia hii ya kutumia mawasiliano ya kisasa ikifungwa katika maeneo yetu itatuwezesha kuona maeneo yote ya bahari kuu na hivyo itatusaidia sana katika usalama na tuko tayari kushirikiana nao, tumekubaliana kuwa teknolojia hii ni muhimu na itafaa kutumika hapa nchini kusaidia kulinda rasilimali zetu”, alisema Dkt. Tamatamah.

Dkt. Tamatamah alibainisha kuwa wavuvi haramu wakiona ulinzi umeimarishwa hapa nchini wataacha kufanya hivyo na watakuja kukata leseni za uvuvi na serikali itapata mapato yake.

Kampuni hiyo ya CS-Group inajishughulisha na utengenezaji wa mifumo ya mawasaliano ya ulinzi na usalama na wamekuja nchini kwa ajili ya kuitangaza teknolojia hiyo ili iweze kutumika hapa nchini.



Mshauri Mwandamizi wa Kampuni ya CS-Group kutoka Paris, Ufaransa, Bw. Hakim Kachetel akiwasilisha kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (kulia aliyekaa) na timu yake taarifa za namna teknolojia waliyonayo inavyoweza kusaidia ulinzi wa rasilimali za bahari kuu mapema leo.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akiongea na Mshauri Mwandamizi wa Kampuni ya CS-Group kutoka Paris, Ufaransa, Bw. Hakim Kachetel walipokutana mapema leo jijini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni