Nav bar

Jumatatu, 10 Januari 2022

WAKUU WA WILAYA, WAKURUGENZI WAAGIZWA KUSIMAMIA ZOEZI LA UTAMBUZI WA MIFUGO.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha amewaagiza wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki Ili kujua idadi ya Mifugo iliyopo katika Wilaya zao.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Longido  Bw. Nurdin Babu ametoa agizo  hilo leo Disemba 14, 2021 wakati akizindua zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa Mkoa wa Arusha ambapo ameeleza kuwa zoezi hilo linalotekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Serikali za mitaa ni muhimu kwa sababu litasaidia kuondoa changamoto mbalimbali hasa katika mifugo na mazao yake.

Amesema zoezi hilo linaloenda na utoaji elimu kwa watendaji wa Serikali ngazi ya halmashauri ni vyema kwa wataalam kila mmoja akaelewa vizuri muongozo wa sheria na kanuni ili aweze kwenda kutoa elimu kwa wafugaji na wataalam waliopo ngazi za chini.

"Niwaagize wakuu wa Wilaya na wakurugenzi kuhakikisha elimu hii inayotolewa leo inawafikia wafugaji na kuhakikisha mifugo yote iliyoainishwa kwenye muongozo ambayo ni Ng'ombe, Punda, Mbuzi na kondoo inavalishwa hereni katika maeneo yenu" amesema

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga, amesema kuwa hereni hizo zimetengenezwa na plastiki maalum ambazo haziharibiwi na joto la jua au kipindi cha mvua kwa kipindi cha miaka takribani 10 zikiwekwa kwenye sikio la mifugo.

Amesema hereni hizo zitakuwa na namba ambazo kila mfugo utasajiliwa kielektroniki ikianzia na namba ya nchi, mkoa hadi ngazi ya chini ambapo pamoja na mambo mengine itabainisha mifugo inayohamishwa mkoa.

"Baada ya kuweka hereni na tukakuta mifugo iliyosajiliwa arusha ipo mtwara tutaangalia kwenye mfumo kama wamehamishwa kihalali na si vinginevyo, kwa hiyo ni mfumo utakaotusaidia kweli kweli kwenye kudhibiti mifugo kuhama kiholela" amesema Prof Nonga.


Mkuu wa Wilaya ya Longido Bw. Nurdin Babu akisoma hotuba wakati wa uzinduzi wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo Mkoani Arusha Disemba 14, 2021. 

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akieleza lengo na faida za utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Jijini Arusha, Disemba 14, 2021 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni