Nav bar

Jumanne, 11 Januari 2022

WAFUGAJI WATAKIWA KUTOA TAKWIMU SAHIHI ZA MIFUGO YAO

Na Saja Kigumbe

Afisa Mifugo na Uvuvi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, Bi.  Asha Churu amewataka wafugaji katika kata ya Duga  kutoa takwimu sahihi za mifugo wanayomiliki pindi zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa mfumo wa hereni za kielekroniki litakapoanza.

Asha alitoa rai hiyo Disemba 19, 2021 wakati wa ufunguzi wa zoezi la kuhamasisha  wafugaji juu ya mfumo wa utambuzi wa mifugo kwa njia ya kielekroniki ambao unatarajia  kuanza Januari 2022.

Alisema kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wafugaji ya kutotoa takwimu sahihi za mifugo yao kwa kuhofia kupunguziwa kutokana na wingi wao, jambo ambalo limekuwa likikwamisha jitihada za Serikali hasa katika ugawaji wa maeneo ya malisho.

"Serikali inapoleta sensa ya mifugo moja kwa moja hata kwenye uwekezaji wa miundombinu ya majosho na malisho inakua ni rahisi, lakini sisi wawekezaji sasa tumekuwa na dhana ya kwamba ukitoa takwimu sahihi ya mifugo na kubainika ni mingi labda itakufa au itachukuliwa niwaambie sio kweli tujitokeze na takwimu sahihi ili kusaidia uwekezaji wa miundombinu" alisema

Mkurugenzi Msaidizi huduma za ukaguzi na Ustawi wa Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Annette Kitambi aliwataka wafugaji hao kutambua umuhimu wa zoezi hilo kwani kutoshiriki kikamilifu kutawakosesha fursa ya kuuza mifugo yao ndani na nje ya nchi kwa sababu itakuwa haitambuliki kisheria.

Alisema miongoni mwa majukumu ya chama na wafugaji ni kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa namna ambavyo halitaleta kero kwa wafugaji na kuhamasisha wanachama wao kujitokeza kuvalisha hereni mifugo yao yote.

"Mfugaji atakayeshindwa kusajili mifugo yake atashindwa kuuza mifugo hiyo mahali popote nchini na kimataifa,  Alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafugaji kata ya Duga, Juma Athumani aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuanzisha mfumo huo kwa sababu utaenda kumaliza changamoto ya wizi wa mifugo baada ya kuvalishwa hereni za kielektroniki hasa kwa wafugaji walio katika mipaka ya nchi.


Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Annette Kitambi akiwaeleza wafugaji wa kata ya Duga Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga umuhimu  wa utambuzi usajili na ufuatiliaji wa mifugo. Disemba 19,2021. 

Mwenyekiti wa wafugaji kata ya Duga, Bw. Juma Athuman, akihamasisha wafugaji wa kata hiyo juu ya utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya kielektroniki kwani ni njia bora na ina faida kwao na kwa Mifugo yao. Disemba 19,2021. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni