Na. Edward Kondela
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Ngusa Samike amewataka maafisa wa serikali na wadau wa sekta ya mifugo watakaosimamia zoezi la uwekaji hereni za kieletroniki kwenye mifugo mkoani humo, kuhakikisha Mkoa wa Mwanza unakuwa wa mfano nchini katika kufikia malengo ya zoezi hilo.
Bw. Samike amesema hayo (17.12.2021) wakati akifungua mkutano wa mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki Mkoani Mwanza, mkutano ambao umehudhuriwa na maafisa kutoka Idara ya Mifugo na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mkoa wa Mwanza na wilaya zake, na kubainisha kuwa atakuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha zoezi la uwekaji hereni ili liweze kufanikiwa kwa Mkoa wa Mwanza kwa kuwa ni miongoni mwa mikoa yenye mifugo mingi hapa nchini.
Aidha, aliwataka maafisa wa serikali na wadau wa sekta ya mifugo
watakaokuwa wakitekeleza uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo kumpatia
taarifa kila mara na pindi wanapopata vikwazo vyovyote katika maeneo yao
wampatie taarifa ili pia atoe elimu kwa viongozi wenzake na mkoa uweze
kufanikiwa kusajili mifugo mingi.
“Sisi kwenye mkoa inabidi tujipange, nataka tuwe mkoa wa mfano kwenye hili zoezi na wote mnaohusika, wadau wote tutawapima kweli kweli, nitakapokuwa nakuja kwenye maeneo yenu hii itakuwa sehemu ya ajenda.” Amesema Bw. Samike
Pia, katibu tawala huyo ametaka elimu izidi kutolewa zaidi katika zoezi la uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo na kuipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kukishirikisha Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) ili kuongeza uelewa zaidi kwa wafugaji.
Akifafanua juu ya mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki Dkt. Audifas Sarimbo wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema kutokana na uwepo wa viwanda vya kuchakata nyama nchini, moja ya matakwa ya wawekezaji na wateja wao kutoka nchi mbalimbali ni uwepo wa mifugo ambayo inaweza kutambulika tangu kuzaliwa kwao kabla ya kununuliwa viwandani kwa ajili ya kuchakatwa na hatimaye mazao yake kupelekwa katika masoko ya nje.
Amebainisha hatua hiyo inasadia kupata taarifa sahihi ya mazao ya mnyama huyo yanayopelekwa nje ya nchi pamoja na kufuatilia historia ya magonjwa na maeneo mifugo ilipotoka pamoja na malisho iliyokuwa ikitumia.
Ameongeza kuwa nchi itaweza kupata idadi kamili ya mifugo iliyopo katika ngazi ya taifa, mkoa, wilaya, tarafa, kata hadi kijiji na kufahamu mahitaji mbalimbali ya wafugaji yakiwemo ya idadi ya dawa za mifugo zinazohitajika kwa ajili ya mifugo yao.
Katika hatua nyingine maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa katika utambulisho wa mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki Mkoani Mwanza, wamefika katika Kijiji cha Ng’ombe kilichopo Kata ya Igokelo Wilaya ya Misungwi mkoani humo na kukutana na wataalamu wa mifugo na viongozi wa wafugaji katika ngazi za wilaya, kata na vijiji ili kuhamasisha wafugaji kuweka hereni kwa mifugo yao, kwa maana ya ng’ombe, punda, mbuzi na kondoo.
Wakiwa kijijini hapo Katibu wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Kanda ya Ziwa Victoria Bw. Masala Elias, amewaaarufu wafugaji kuwa wanatakiwa kuwekea mifugo yao hereni hadi Mwezi Agosti Mwaka 2022 kabla serikali haijatoa maamuzi mengine na kuipongeza serikali kwa kuhakikisha hereni hizo zinapatikana kwa bei nafuu, huku mmoja wa wafugaji wa Kijiji cha Ng’ombe Bw. Cloud Lugiko akihamasisha wafugaji wenzake kuanza kutekeleza zoezi hilo kwa kadri idadi ya mifugo aliyonayo kila mfugaji ili kutekeleza zoezi hilo kwa wakati.
Zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa hereni za kieletroniki ambalo linafanyika kote nchini kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2011 linatekelezwa kwa mfugaji kulipia gharama ya Shilingi 1,750/= kwa ng’ombe na punda na Shilingi 1,000/= kwa mbuzi na kondoo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni