Na. Edward Kondela
Wafanyabiashara wa mifugo nchini
wametakiwa kuepuka kusafirisha mifugo yao kwenda nje ya nchi bila kufuata
utaratibu kwa kuwa serikali itakosa mapato kupitia rasilimali za nchi na pia ni
kosa kisheria.
Akizungumza jana (14.04.2021) wakati
alipotembelea eneo ambalo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepewa na Kijiji cha
Horohoro Kijijini, kilichopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, kwa ajili ya
kuanzisha mnada wa mifugo wa mpakani, Katibu Mkuu wa wizara hiyo
anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara haitakuwa
tayari kumtetea mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutenda kosa hilo.
Prof. Gabriel amesema Wizara ya Mifugo
na Uvuvi imedhamiria kuanzisha mnada wa mpakani kati ya Tanzania na Kenya
katika Kijiji cha Horohoro Kijijini kabla ya mwaka ujao wa fedha 2021/22 ili
kudhibiti baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitorosha mifugo kwenda
nchi ya jirani kwa ajili ya kuuza.
“Mfanyabiashara akibainika kufanya
hivyo atashughulikiwa kwa kutumia mkono wa sheria, kwani kwa kufanya hivyo
inakosesha serikali mapato kupitia rasilimali za nchi.” Amefafanua Prof.
Gabriel
Ameongeza kuwa eneo hilo ambalo wizara
imepatiwa na Kijiji cha Horohoro Kijijini lina ukubwa wa ekari 23 na lipo kando
mwa barabara kuu ya kuelekea mpakani mwa Tanzania na Kenya, hivyo uwepo wa
mnada huo utawezesha wafugaji wa Tanzania kuuza mifugo yao kwa wafanyabishara
wa nchi hizo mbili.
Ametoa wito kwa wafugaji Mkoa wa Tanga
na mikoa ya jirani kuwa malighafi ya biashara ya minada ni mifugo, hivyo
watambue jitihada za serikali na kumnukuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameitaka Sekta ya Mifugo kusogeza
huduma zinazotakiwa kwa wafugaji ili mifugo yao isikonde na wafugaji wasikonde
kiuchumi.
Aidha, amebainisha kuwa nia ya Wizara
ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha Sekta ya Mifugo inachangia zaidi katika pato
la taifa hivyo ni lazima kudhibiti utoroshaji wa mifugo kwenda nchi za jirani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali
ya Kijiji cha Horohoro Kijijini Bw. Jumapili Yohana amesema wameamua kuipatia
Wizara ya Mifugo na Uvuvi eneo hilo bila malipo yoyote wakiamini uwepo wa mnada
mpakani katika kijiji hicho kutachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ajira na
kukuza biashara zingine ikiwemo ya vyakula.
Bw. Yohana amesema kijiji kimefuata
taratibu zote za ardhi na kukubaliana kuwa mara baada ya mnada huo utakapoanza
kufanya kazi utachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijiji chao na
kuishukuru wizara kwa ushirikiano.
Pia, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika ziara ya
siku moja Mkoani Tanga amefika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na
kujionea shughuli mbalimbali ikiwemo ya tafiti ya malisho bora ya mifugo na
kuwaasa wafugaji kuipatia mifugo yao malisho bora ili iweze kuwa na afya njema
na kuwa na nyama bora, maziwa bora na ngozi bora.
Amewataka wafugaji kufuga kisasa kwa
kutumia sayansi na kuitaka TALIRI kusambaza tafiti zao mikoa mbalimbali ili
wafugaji waweze kupata elimu ya kufuga kisasa na kuwa na mifugo bora na yenye
afya ambayo itakuwa na tija kiuchumi.
Amewaasa pia wawekezaji na watu
wanaofikiria kuwekeza, wafikirie kuwekeza katika malisho ya mifugo ili malisho
bora yapatikane kwa wingi kwa kuwa wafugaji wengi wameanza kubadili fikra za
ufugaji na kuhitaji malisho ya kisasa na kisayansi ambayo yanafaa kwa matokeo
chanya ya mifugo yao.
Prof. Gabriel katika ziara yake ya siku
moja Mkoani Tanga ametembelea pia Ranchi ya Mzeri iliyopo Wilaya ya Handeni na
kuzungumza na wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo na Kampuni ya
Ranchi za Taifa (NARCO) na kukemea tabia ya baadhi ya watu wanaoiba mifugo
kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kwenye ranchi.
Katibu mkuu huyo pia amefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kuwa na mazungumzo na mkuu wa mkoa huo Mhe. Martine Shigella pamoja na Katibu Tawala wa mkoa Bi. Judica Omari juu ya maendeleo ya sekta ya mifugo katika Mkoa wa Tanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni