Na Mbaraka Kambona,
Serikali ya Marekani imesema itaendelea
kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuinua
Sekta za Mifugo na Uvuvi ili ziweze kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la
Taifa.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki wakati akizungumza na Waandishi wa Habari muda
mfupi baada ya mazungumzo na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Dkt. Donald
Wright yaliyofanyika jijini Dodoma Aprili 14, 2021.
Ndaki alisema kuwa katika mazungumzo
yao, Balozi Wright alimuhakikishia kuwa
Serikali ya Marekani ipo tayari kuleta wawekezaji kutoka Marekani ili kusisimua
na kukuza sekta hizo mbili ili ziweze kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa
viwanda.
“Balozi Wright ameahidi kuleta
wataalamu kutoka marekani ili kubadilishana uzoefu wa kiufundi katika sekta ya
mifugo ili wafugaji wetu waweze kubadilika na kuanza kufuga kibiashara ili kukuza kipato chao na kuongeza ajira
nchini,”alisema Ndaki
Kuhusu uchumi wa Bluu ambao Serikali ya
Tanzania imeanza kuwekeza, Ndaki alisema kuwa Serikali ya Marekani italeta
wawekezaji kuja kuwekeza katika eneo hilo na kuisaidia Tanzania kuona tija ya
uwekezaji uchumi huo.
“Wenzetu wa Marekani wameendelea na
wamewekeza sana katika uchumi wa bluu hivyo kupitia wao wanaweza kutusaidia
kuimarisha eneo hilo ili sekta ya uvuvi iweze kuwa na tija zaidi kwa taifa
letu,”aliongeza Ndaki
Aliendelea kusema kuwa Serikali ya
Marekani ipo tayari kusaidia mapambano ya uvuvi haramu nchini ili kuhakikisha
unakwisha na watu wanafanya uvuvi endelevu.
Aidha, Ndaki alimuomba Balozi huyo
kuona uwezekano wa kuwapatia Watanzania nafasi ya kwenda kujifunza na kupata
ujuzi kuhusu masuala ya mifugo na uvuvi katika nchi ya Marekani ili waweze kusaidia
kuimarisha sekta hizo nchini.
Waziri Ndaki alisema kuwa ziara ya
Balozi Wright ni kwa ajili kuimarisha ushirikiano katika sekta za mifugo na
uvuvi, pia ililenga kutoa salamu za pole kutoka nchini Marekani kwa Rais wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt.
John Pombe Magufuli kufariki.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Dkt. Donald Wright muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dodoma Aprili 14, 2021. Lengo la mazungumzo yao ni kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili katika sekta za Mifugo na Uvuvi nchini.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (mstari wa mbele kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Dkt. Donald Wright (kulia) muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika jijiji Dodoma Aprili 14, 2021.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati) akionesha kuvutiwa na zawadi aliyopewa na Balozi wa Marekani Nchini Tanzania, Dkt. Donald Wright (kulia) alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma Aprili 14, 2021. Lengo la ziara hiyo ya Balozi Dkt. Wright ni kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili hususani katika sekta za Mifugo na Uvuvi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni