Na Mbaraka Kambona,
Serikali imezindua mpango wa unywaji
maziwa kwa Watumishi wa Umma kwa lengo la kuhamasisha unywaji wa maziwa
yanayozalishwa ndani ya nchi lakini pia kuongeza kipato cha wafugaji.
Akizindua mpango huo jijini Dodoma
Aprili 13, 2021, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema kuwa
utekelezwaji wa mpango huo utasaidia kutatua changamoto ya soko la maziwa na
kuleta tija kwa wafugaji.
Waziri Ndaki alisema kuwa lita za
maziwa zinazozalishwa na wafugaji nchini ni bilioni 3 lakini maziwa
yanayochakatwa kwa mwaka ni milioni 74.3 na hivyo kufanya maziwa mengi kupotea
kwa kukosa soko la uhakika jambo ambalo sio zuri kwa mustakabali wa tasnia ya
maziwa.
" Leo tunazindua awamu ya kwanza
ya unywaji wa maziwa kwenye Ofisi za Serikali na kwa awamu hii ya kwanza tumeanza
na wizara kumi (10), lakini kutakuwa na
awamu nyingine ya uzinduzi zitakazohusisha
wizara, taasisi na mashirika ya umma,” alisema Ndaki
Alisema kuwa uzinduzi huo unakwenda
sambamba na ugawaji wa majokofu ya kutunzia maziwa kwa wizara hizo huku akitumia
nafasi hiyo kuwaomba Viongozi katika Wizara, Watumishi na Wananchi kwa ujumla
kuunga mkono mpango huo.
Aliongeza kuwa unywaji wa maziwa katika
ofisi za umma utainua kwa kiwango kikubwa soko la maziwa yanayozalishwa nchini
na kuepuka unywaji wa maziwa kutoka nje ya nchi, na hivyo kukuza pato la
wafugaji pia itachochea upatikanaji wa ajira.
Ndaki alisema itakua ni jambo la ajabu
kuona Ofisi ya Serikali inaagiza maziwa yanayotengenezwa kutoka nje wakati
Serikali imezindua mpango mahususi unaohamasisha unywaji wa maziwa
yanayozalishwa nchini.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya
Maziwa nchini, Dkt. George Msalya alisema ana imani kuwa kama ofisi zote za
Serikali ambapo watumishi wa umma wanafika takribani Laki Tano zitaunga mkono
unywaji huo wa maziwa itakua ni fursa nzuri na pana ya kukuza soko la maziwa ya
ndani.
Wizara
ambazo zimehusishwa katika awamu hiyo ya kwanza ya uzinduzi wa unywaji wa maziwa unaoratibiwa na Bodi ya
Maziwa ni pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara
ya Viwanda na Biashara, TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Elimu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa Wawakilishi wa Kampuni ya kuchakata maziwa ya ASAS kuhusu bidhaa mbalimbali wanazozalisha muda mfupi kabla ya uzinduzi wa mpango wa unywaji maziwa kwa Watumishi wa Umma uliofanyika jijini Dodoma Aprili 13, 2021.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba
Ndaki (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
Wawakilishi wa Makampuni ya kuchakata Maziwa yaliyoungana na Wizara ya Mifugo
na Uvuvi kupitia Bodi ya Maziwa kuzindua mpango wa unywaji maziwa kwa Watumishi
wa Umma jijini Dodoma Aprili 13, 2021. Baadhi ya Makampuni hayo
yaliyoshirikiana na Wizara ni pamoja na ASAS, Milkcom, na Kilimanjaro Fresh.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dkt. George Msalya (wa kwanza kushoto) na Watumishi wengine wa Bodi hiyo muda mfupi baada ya uzinduzi wa mpango wa unywaji wa maziwa kwa Watumishi wa Umma uliofanyika jijini Dodoma Aprili 13, 2021.Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akimkabidhi Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Bedan Masuruli (kushoto) Jokofu lenye maziwa ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa mpango wa unywaji wa maziwa kwa Watumishi wa Umma uliofanyika jijini Dodoma Aprili 13, 2021.
Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dkt. George Msalya (kulia) akitoa maelezo mafupi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba ndaki (wa kwanza kushoto) kuhusu Mpango wa Unywaji wa Maziwa kwa Watumishi wa Umma muda mfupi kabla kuuzindua jijini Dodoma Aprili 13, 2021.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati) akinywa maziwa kuashiria uzinduzi wa mpango wa unywaji maziwa kwa Watumishi wa Umma uliofanyika jijini Dodoma Aprili 13, 2021. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Bedan Masuruli na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uzalishaji na Masoko, Abdallah Temba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni