Na. Edward Kondela
Wafanyabiashara katika Mnada wa
Kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam, wameiomba Wizara ya Mifugo na
Uvuvi kuendelea kutatua changamoto zilizopo katika mnada huo ili uwe na tija
kwao na taifa kwa ujumla.
Wakizungumza mara jana (12.04.2021)
baada ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof.
Elisante Ole Gabirel kufika mnadani hapo, kwa ajili ya kufuatilia maelekezo ya
uboreshaji aliyoyatoa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki baada ya
kufika mnadani hapo hivi karibuni, wamesema wana imani kuwa mnada huo
ukiboreshwa zaidi utaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.
Baadhi ya wafanyabiashara
waliowasilisha kero zao kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo
Prof. Elisante Ole Gabriel wamesema bado wanakabiliwa na changamoto ya
upatikanaji wa maji ya uhakika kwa ajili ya kunyweshea mifugo yao, uzio wa
mnada kutokuwepo katika baadhi ya maeneo na kuchangia mifugo kutoka nje ya
mnada hali ambayo inaweza kusababisha baadhi ya mifugo kupotea.
“Tatizo kubwa hapa kwenye mnada huu ni
maji kwa ajili ya mifugo viongozi mbalimbali wamewahi kuja hapa pamoja na
kuchimba kisima na kuwekwa birika la kunywea maji mifugo, lakini hakujawahi
kuwepo maji hata siku moja ninashauri lirekebishwe lambo ambalo limekuwa
likitumiwa siku nyingi tutakuwa na uhakika wa maji.” Amesema Bw. Said Waziri
mmoja wa wadau katika mnada huo.
Aidha, baadhi ya wafanyabiashara hao
wamemuomba katibu mkuu huyo kuangalia uwezekano wa ukarabati wa barabara kutoka
Gongo la Mboto ambayo inaelekea kwenye mnada huo ili magari yanayobeba mifugo
yaweze kupita kwa urahisi kwa kuwa mifugo imekuwa ikipata majeraha na mingine
kufa kutokana na kukanyagana wakati magari hayo yanapopita kwenye barabara hiyo
ambayo ina mashimo makubwa.
Akizungumza mara baada ya kuwasikiliza
wafanyabiashara hao Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia
Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wizara itafanya kila liwezekanalo
ianze kufanya ukarabati wa uzio wa mnada kuanzia mwaka huu wa fedha 2020/21 na
kuendelea na ukarabati katika bajeti ijayo ya mwaka fedha 2021/22.
Prof. Gabriel amesema suala la uzio
wizara inalipa kipaumbele likisimamiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki ili mnada huo wa kimataifa wa Pugu uweze kukidhi mahitaji ya
wafanyabiashara wa mnada huo.
“Nikiri kwamba pamoja na mambo mengine
alichonituma waziri kuja kuangalia kwa umakini sana ni suala la uzio na tutaona
jinsi gani ya kuanza kwa mwaka huu wa fedha na tutalianza mara moja na
nimeshawaelekeza wataalamu waje kuangalia nini cha kufanya.” Amesema Prof.
Gabriel
Kuhusu changamoto ya ubovu wa barabara
kutoka Gongo la Mboto hadi katika mnada huo, katibu mkuu huyo ameongea kwa njia
ya simu akiwa mnadani hapo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini
na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff, ambaye amesema atalisimamia suala hilo
kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Prof. Gabriel amesema kuhusu changamoto
ya ukosefu wa maji, suala hilo analichukua kwa ajili ya kulifanyia kazi zaidi
na kutafuta njia ambayo itaweza kusaidia uwepo wa maji ya uhakika kwa ajili ya
kunyweshea mifugo.
Pia, katibu mkuu huyo ameelekeza kuanza
kutumika mara moja kipakilio cha mifugo kwenye malori ambacho kimekamilika
licha ya uwepo wa baadhi ya marekebisho ambayo ameelekeza yafanyiwe huku
kikiendelea kutumika kutokana na wafanyabiashara kulalamika kupata wakati mgumu
wakati wa kupakia na kushusha mifugo kwenye malori.
Kufuatia maelekezo hayo baadhi ya wafanyabiashara wamesema wamefurahishwa na kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel na kubainisha kuwa wamepata imani kubwa kwa wizara hiyo kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira rafiki zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni