Serikali imesema ipo tayari kuendelea kupitia Sera na Sheria ya Uvuvi nchini ili iweze kukidhi mahitaji ya wavuvi wadogo kama ambavyo imekuwa ikifanya hivyo mara kwa mara pale inapohitajika.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge
wa viti maalum kutoka mkoani Kagera Mhe. Neema Lugangira ambaye alitaka
kufahamu mikakati ya Serikali katika kuhakikisha Sera na Sheria ya uvuvi nchini
inakidhi mahitaji ya wavuvi wadogo.
Mhe. Ulega amesema kuwa katika
kuhakikisha wavuvi wadogo nao wananufaika na Sera na sheria iliyopo, Wizara
ilifanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 2015 ambayo imezingatia
mahitaji ya wadau wote wa sekta ya uvuvi na uendelezaji wa rasilimali za uvuvi
nchini.
“Aidha Wizara ilifanya mapitio ya
sheria namba 6 ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania ya mwaka 1980 na kutunga
sheria namba 11 ya mwaka 2016 ili kuimarisha shughuli za utafiti nchini” Aliongeza
Mhe. Ulega.
Mhe. Ulega ameongezea kuwa mwaka 2020
Wizara ilifanya marekebisho madogo kwenye sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka
2003 kwa lengo la kuimarisha shughuli za ulinzi na usimamizi shirikishi wa
rasilimali za Uvuvi nchini.
“Mhe. Spika Wizara inaendelea kufanya
maboresho makubwa kwenye sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 ili iweze
kuendana na mahitaji halisi ya sasa ya kisekta ikiwemo kutatua kero mbalimbali
za wadau wa sekta ya uvuvi hususani wavuvi wadogo na wakuzaji viumbe maji”
Alisema Mhe. Ulega.
Akijibu swali la nyongeza la Mhe.
Lugangira ambaye alitaka kufahamu mpango wa Serikali katika kuhakikisha
wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi wananufaika ipasavyo baada ya kuuza samaki na
mabondo kwa pamoja, Mhe. Ulega mbali na kukiri kuwa mabondo yana thamani kubwa
hivi sasa hasa kwenye masoko ya bara la Asia, amesema kuwa Sheria ya Uvuvi na kanuni zilizopo hivi
sasa zinayatambua mabondo kama moja ya bidhaa zinazotokana na samaki hivyo
aliahidi kupokea rai na ushauri uliotolewa na Mhe. Lugangira na kwenda
kuufanyia kazi.
Mhe. Ulega alihitimisha majibu yake kwa
kujibu swali la nyongeza la Mhe. Lugangira aliyetaka kufahamu mikakati ya
Serikali katika kuwalinda wanawake wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi
dhidi ya ukatili wanaofanyiwa wakati wa utekelezaji wa shughuli zao ambapo
amesema kuwa Serikali ilifanya maboresho ya Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015 na
kuweka jukwaa maalum la kuwasaidia wanawake ikiwa ni pamoja na kuwatambua moja
kwa moja wanawake wafanyabiashara wa samaki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni