Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameagiza upatikanaji wa chanjo ya mifugo ya ugonjwa wa miguu na midomo (FMD) ifikapo mwakani ili bidhaa zitokanazo na mifugo ziweze kuuzwa katika masoko ya kimataifa.
Prof. Gabriel ameyasema hayo jana
(16.04.2021) jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha baraza la
wafanyakazi la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), ambapo
amemuelekeza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Prof. Hezron Nonga kusimamia
utekelezaji wa uanzishwaji wa chanjo hiyo ili kuwezesha viwanda vinavyozalisha
nyama zitokanazo na mifugo hapa nchini kupata masoko ya bidhaa zao katika nchi
mbalimbali.
Aidha ameitaka TVLA kuhakikisha
changamoto ya homa ya nguruwe inatatuliwa kwa kupatikana kwa chanjo yake na
kutokomeza kabisa ugonjwa huo hapa nchini na kuondoa dhana iliyojengeka kwa
baadhi ya wananchi kuwa baadhi ya mifugo imekuwa ikibaguliwa katika upatikanaji
wa huduma mbalimbali zikiwemo za chanjo.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo
kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amesema mkakati uliopo ni
kuhakikisha mwaka ujao zinazalishwa chanjo tatu za mifugo ikiwemo ya kichaa cha
mbwa ili kufikia ukomo wa ugonjwa huo kwa kuwa lengo la dunia ni kuhakikisha
ifikapo mwaka 2030 ugonjwa huo unatokomezwa duniani.
Pia amesema chanjo zingine za ugonjwa
wa sotoka ya mbuzi na kondoo tayari hatua zaidi zinaendelea kufanywa na TVLA
ili kuhakikisha mwaka ujao chanjo hizo zinazalishwa hapa nchini pamoja na
kuzalisha chanjo ya mapele ngozi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala
ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi amesema wakala
hiyo tayari imezalisha chanjo ya saba ya homa ya mapafu ya mbuzi kati ya chanjo
13 za kimkakati na tayari imethibtishwa na maabara ya chanjo za mifugo Afrika
na imepata cheti cha ubora na uzalishaji wake umeshaanza.
Dkt. Bitanyi amesema TVLA inatategemea
kuzindua chanjo hiyo kati ya Mwezi Mei na Juni mwaka huu ili itangazwe na
wafugaji waanze kuitumia pamoja na kuweka mikakati ya uwezo wa kuzalisha zaidi
chanjo dhidi ya homa ya mapafu ya ng’ombe kwa kuagiza mashine yenye uwezo
mkubwa zaidi wa kuzalisha chanjo hiyo.
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo ipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inazalisha chanjo 13 za mifugo ambazo ni za kimkakati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni