Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wafugaji pamoja na wataalam wa sekta ya mifugo kuusimamia na kuutekeleza mwongozo wa chanjo za mifugo.
Waziri
Ndaki ameyasema hayo jana (07.02.2021) baada ya kumalizika kwa semina kuhusu
masuala ya chanjo za mifugo iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa
wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji iliyofanyika katika
ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma.
“Wizara
ilishaandaa na kuzindua mwongozo utakao simamia masuala ya uchanjaji mifugo
hivyo ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunausimami na kuutekeleza badala ya
kusubiri mpaka sheria zitumike,” alisema Mhe. Ndaki.
Akizungumza
na wajumbe hao wa kamati, Waziri Ndaki amewaomba pindi watakapo rejea majimbo
kwao kila mmoja akasaidie kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa mwongozo huo
kwani kwa kufanya hivyo nchi itakuwa na uhakika wa kuwa na mifugo iliyo na afya
bora na ambayo ipo salama hivyo kuongeza thamani ya mazao yanayotokana na
mifugo hiyo.
Pia
alieleza kuwa wizara inaendelea kuboresha huduma za chanjo kwa kuendelea na
mkakati wa kuhakikisha inakamilisha uzalishaji wa chanjo zote 13 za magonjwa ya
kimkakati ili wafugaji wasiendelee kuteseka dhidi ya magonjwa hayo pindi chanjo
zitakapokamilika. Hivyo amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kwenda kusaidia kutoa
elimu kwa wafugaji na wananchi kwa ujumla katika maeneo wanayotoka ili wote kwa
pamoja waweze kufahamu umuhimu wa chanjo kwa mifugo.
Aidha,
Waziri Ndaki amesema kuwa katika semina hiyo wamepokea michango mizuri sana kutoka
kwa wajumbe wa kamati, kuhusu masuala ya chanjo, mwongozo wa chanjo na mambo
mengine ya sekta ya mifugo. Pia amesema amewaomba wajumbe hao wa kamati kwenda
kusimamia utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na serikali kwenye Mamlaka za
Serikali za Mitaa katika maeneo wanayotoka ili malengo yaliyowekwa yaweze
kufikiwa.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe.
Christine Ishengoma alisema upo umuhimu wa maafisa ugani kuhakikisha wanafanya
ufuatiliaji kuhakikisha wafugaji wanachanja mifugo yao kwani kwa kutofanya
hivyo magonjwa ya mifugo yataendelea kusambaa hasa pale mifugo iliyochanjwa
ikichanganyika na isiyochanjwa.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul, amewataka
wakurugenzi wa halmashauri kuusoma vizuri mwongozo wa chanjo na kuangalia
uwezekano wa kuwatumia wataalam wa mifugo waliomaliza vyuo wakishirikiana na
madaktari wa mifugo wa halmashauri kutoa chanjo za mifugo.
Gekul
amesema kuwa kwa kufanya hivyo halmashauri zitakuwa zinapata mapato ambayo
yatasaidia pia katika kukarabati na kujenga miundombinu ya mifugo kama majosho,
malambo na minada na hivyo kuleta manufaa kwa wafugaji pia.
Vilevile
alisema kuwa wizara ilishatoa bei elekezi za chanjo hizo ambapo kila mmoja
anatakiwa kuzifuata na endapo katika utekelezaji kutakuwa na changamoto yoyote
ni vema wahusika wakafanya mawasiliano na wataalam wa wizara. Pia amesema
wizara imejipanga kuhakikisha inaendelea kutoa elimu kuhusu chanjo kwa
kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Chama cha Wafugaji ambapo pia
amewataka wataalam wa mifugo katika mikoa na halmashauri kuhakikisha wanatumia
mikutano ya kisheria iliyopo katika ngazi mbalimbali kutoa elimu kuhusu masuala
ya chanjo.
Naye,
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof.Elisante Ole Gabriel alisema kuwa vipaumbele vikubwa
vilivyopo katika sekta ya mifugo kwasasa ni kushughulikia afya ya mifugo kwa
ujumla, kuboresha kosaafu za mifugo ili kupata mifugo iliyo bora na kujenga na
kukarabati miundombinu ya mifugo kama vile majosho, malambo, masoko (minada) na
uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda kwa ajili ya kuchakata mazao yatokanayo na
mifugo.
Kwa
upande wa chanjo za mifugo, Prof. Gabriel alisema upo umuhimu kwa nchi
kuzalisha chanjo zake yenyewe kwani kwa kutegemea chanjo kutoka nje ni rahisi kwa
mtu mwenye nia mbaya kuweka kemikali ambazo zinaweza kuidhuru mifugo. Lakini pia
alisema kwa nchi kuzalisha chanjo yenyewe kutasaidia kutoa ajira kwa wahitimu
kutoka katika vyuo vya hapa nchini, kuongeza kipato katika nchi na
kujihakikishia usalama wa chanjo zinazokwenda kutumika katika kuchanja mifugo
ya hapa nchini na hata nje ya nchi.
Prof.
Gabriel alisema kuwa asilimia 60 ya magonjwa wanayougua binadamu yanatokana na magonjwa
yanayohama kutoka kwenye mifugo, hivyo mkazo, hivyo mkazo mkubwa ukiwekwa
kwenye kudhibiti afya ya wanyama serikali itaokoa fedha takribani Sh. Bilioni
160 zinazotumika na Wizara ya Afya kutibu magonjwa hayo.
Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella
Bitanyi amesema wakala hiyo ina majukumu mbalimbali ikiwemo utafiti na utambuzi
wa magonjwa ya mifugo na kuhakiki ubora wa mifugo na kuzalisha chanjo za
magonjwa ya mifugo.
Dkt.
Bitanyi amesema TVLA imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kufikisha
huduma zake katika mikoa, lakini pia wameweza kuzalisha chanjo 6 za magonjwa ya
kimkakati kati ya magonjwa 13 na mwezi Machi mwaka huu wanatarajia kuzalisha
chanjo ya saba.
Wakala
hiyo ya Maabara ya Veterinari kwa sasa inahitaji kupata sh. Bilioni 2.6 ili
kujiimarisha katika miundombinu, vifaa vya maabara na wataalam ambapo watakuwa
na uwezo wa kuzalisha sh. Bilioni 10.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt.
Christine Ishengoma (wa pili kutoka kulia), Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kushoto), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Pauline Gekul (wa kwanza kushoto) na Katibu Mkuu anayesimamia sekta ya
Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kulia) wote kwa pamoja wakiandika
hoja zilizokuwa zikiulizwa na wajumbe wa kamati hiyo (hawapo pichani) wakati wa
semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala ya chanjo za
mifugo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma.
(07.02.2021)
Kaimu Mtendaji Mkuu –
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi
akiwasilisha mada kuhusu majukumu na mipango ya Wakala ya Maabara ya Veterinari
kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Uvuvi wakati wa
semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala ya chanjo za
mifugo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma.
(07.02.2021)
Kaimu Mkurugenzi wa Idara
ya Huduma za Mifugo, Dkt. Gibonce Kayuni (kulia aliyesimama) akiwasilisha mada
kuhusu masuala ya chanjo za mifugo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na
Uvuvi kuhusu masuala ya chanjo za mifugo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi
wa Pius Msekwa Jijini Dodoma. (07.02.2021)
Baadhi ya wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji wakiwa pamoja na wataalam kutoka
WMUV, wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa semina
iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala ya chanjo za mifugo.
Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma. (07.02.2021)
Baadhi ya Viongozi na
Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiandika hoja na maelekezo
yaliyokuwa yanatolewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na
Maji wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu masuala
ya chanjo za mifugo. Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa Jijini
Dodoma. (07.02.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni