Na. Edward Kondela
Jeshi
la Polisi Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na
vyombo vingine vya ulinzi na usalama limewakamata watuhumiwa wawili wa
utoroshaji wa mifugo maeneo ya mipakani.
Kwa
mujibu wa taarifa aliyotoa jana (02.02.2021), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Blasius Chatanda alisema kufuatia
operesheni kubwa ya kitaifa iliyoanzishwa hivi karibuni, ambayo ililenga
kudhibiti matukio ya wizi wa mifugo pamoja na usafirishaji wa mifugo nje ya
nchi bila kufuata utaratibu, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa hao na
linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine.
“Kama
mnavyofahamu mpaka wetu wa Horohoro ni miongoni mwa mipaka ambayo inaweza
kutumika kupeleka mifugo nje ya nchi hususan nchi jirani ya Kenya lakini pia
bahari yetu (Bahari ya Hindi) inaweza kutumiwa pia kuvusha mifugo kupeleka
Tanzania visiwani, Comoro, Ushelisheli lakini pia Madagascar, kufuatia
operesheni hiyo kali na kabambe huku kwetu kulikuwa na watuhumiwa Wilaya ya
Mkinga, walikuwa watuhumiwa watatu kati ya hao watuhumiwa wawili tayari
wamekamatwa na wameshaunganishwa na wenzao kule Arusha ili kuendelea na
taratibu za kichunguzi na hatimaye wafikishwe mahakamani.” Alisema Kamishna
Msaidizi Chatanda.
Aliongeza
kuwa Mkoa wa Tanga ni kati ya mikoa yenye wafugaji wengi na kuwasihi wale wote
wanaojihusisha na vitendo vya utoroshaji wa mifugo waache mara moja, kwa sababu
mkono wa sheria hautawaacha salama na kwamba serikali iko makini kupitia Wizara
ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha vitendo hivyo vinakoma na kubainisha kuwa katika
mpaka wa Horohoro kwa miaka mingi mifugo ilikuwa haivuki kwa kufuata utaratibu,
kwa kuwa ilikuwa inapitishwa njia zisizo rasmi na kwenda kwenye soko la jirani
la nchi ya Kenya hali ambayo ilifanya wafugaji kuuza mifugo kwa hasara na
wengine kupoteza mifugo wakati wa kuvusha kwenda nchi ya jirani.
Aliongeza
kuwa kufuatia uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi ilibainika wapokeaji
wengi wa mifugo walikuwa mpakani na wengine wakiwa na madaraka kwenye maeneo
wanayoishi na kufafanua kuwa endapo suala hilo likiendekezwa wanaohusika
hawawezi kubaki salama, lazima wakumbane na mkono wa sheria na waliokuwa
wanafikiria kuanza kutorosha mifugo kwenda nchi ya jirani waache mara moja.
Mwishoni
mwa wiki Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki alifanya ziara ya kikazi
ya siku mbili Mkoani Tanga, ambapo wakati akiwa na mazungumzo na mkuu wa mkoa
huo Mhe. Martine Shigella pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo,
Mhe. Ndaki aliagiza kukamatwa kwa watuhumiwa wa utororshaji wa mifugo na mazao
ya mifugo katika Mkoa wa Tanga na kuupongeza Mkoa wa Tanga kwa jitihada
mbalimbali wanazozichukua katika kudhibiti wizi wa mifugo na utoroshaji wa
mifugo kwenda nchi za nje.
Waziri
Ndaki alisema watuhumiwa 67 wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake tayari
wanafahamika kwa majina na mahali wanapoishi kufuatia ripoti aliyopatiwa na
Jeshi la Polisi nchini kupitia Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo.
Mwanzoni
mwa wiki iliyopita, Jeshi la polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Wizara
ya Mifugo na Uvuvi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama lilitoa
taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa watatu wa wizi na utoroshaji wa mifugo
maeneo ya mipakani.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la
Polisi Salum Hamduni, alisema jeshi hilo liliwakamata watuhumiwa hao katika
tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani humo kufuatia agizo alilolitoa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki la kukamatwa kwa watuhumiwa 67 wa
utoroshaji wa mifugo na mazao yake.
Kamanda
Hamduni alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao watatu kunatokana na baada ya
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutangaza operesheni ya kudhibiti wizi na utororshaji
wa mifugo maeneo ya mipakani ambapo zilipatikana taarifa za uwepo wa watu
wanaojihusisha na wizi na utoroshaji wa mifugo katika Wilaya ya Ngorongoro.
Aliongeza
kuwa upelelezi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo, mara utakapokamilika
jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya hatua zaidi za
kisheria.
Alitoa
wito kwa wananchi kuepuka usumbufu kwa kuhakikisha wanafuata sheria za biashara
ya usafirishaji wa mifugo kwani wasipofanya hivyo watakamatwa na kuchukuliwa
hatua kali za kisheria.
Hivi
karibuni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa katika ofisi za
wizara hiyo zilizopo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma wakati
akiwasilishiwa ripoti ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani
aliliagiza Jeshi la Polisi nchini Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo kuwakamata
mara moja watuhumiwa 67 wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake kwenda nchi za
jirani.
Katika
ripoti ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani, iliyowasilishwa na
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Julius Mjengi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki, imeeleza kuwa kabla ya tarehe 7 Novemba, 2020, mifugo
iliyokuwa inatoka kwenye minada ya awali ya Handeni na Kilindi kuelekea nchini
Kenya kupitia mpaka wa Horohoro haikuwa inafuata taratibu za forodha kama
shehena nyingine.
Aidha,
ripoti hiyo ilibainisha kuwa takwimu za daftari la mifugo katika mpaka wa
Horohoro zinaonyesha idadi ya mifugo iliyopitishwa kuelekea nchini Kenya kwa
kipindi cha miaka 17 kutoka mwaka 2003 hadi Novemba, 2020 ilikuwa ni ng’ombe
24,980 na Mbuzi na Kondoo 9,368 (sawa na wastani wa Ng’ombe 122 na Mbuzi/Kondoo
46 kwa mwezi).
Pia,
imefafanua kuwa baada ya uchunguzi, ilionekana kuwa kati ya tarehe 7 Novemba,
2020 hadi tarehe 9 Desemba, 2020 (kipindi cha mwezi mmoja tu) jumla ya Ng’ombe
1,096 na Mbuzi na Kondoo 1,044 walipitishwa katika kituo cha Forodha kuelekea
nchini Kenya, ambapo huo ni wastani wa idadi ya mifugo iliyopita mpakani ndani
ya mwezi mmoja ukilinganisha na siku za nyuma.
Katika ripoti hiyo ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani, imebaini pia viashiria vya udanganyifu wa kurekodi idadi sahihi ya mifugo inayokaguliwa kwenda Kenya hususan katika mpaka wa Hororohoro – Tanga.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (watatu kutoka kushoto) akipata maelezo
ya Shamba la Mifugo Mruazi Heifer Breeding Unit, kutoka kwa meneja wa shamba
hilo Bw. William Mgunya (aliyevaa kofia). Waziri Ndaki alikuwa akihitimisha
ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Tanga alipotembelea shamba hilo
mwishoni mwa wiki lililopo Wilaya ya Korogwe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni