Na Mbaraka Kambona,
Mratibu
wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya
Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila ameziomba Halmashauri kuvitambua
Vikundi vya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) na kuzipa uwezo wa
kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi ili ziweze kusaidia vikundi
hivyo kujiendesha na kuendeleza sekta ya uvuvi nchini.
Dkt.
Mlalila alitoa rai hiyo katika ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Pauline Gekul alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya BMU
inayojengwa na Mradi wa SWIOFish katika Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo
Januari 7, 2021.
Kwa
mujibu wa Dkt. Mlalila sehemu kubwa ya mapato yanayokusanywa kwa sasa na
Halmashauri hayarudishwi kwa Jamii ya wavuvi kwa ajili ya kuendeleza shughuli
za sekta na uchumi wa jamii husika.
Dkt.
Mlalila alisema anatambua kuwa kuna changamoto ya kisheria ambayo baadhi ya
Halmashauri zimetumia kuzizuia BMU kukusanya mapato yanayotokana na rasilimali
za uvuvi.
“Tunahamasisha
Halmashauri kuwapa uwezo BMU kukusanya mapato ili kuziwezesha kupata kipato cha
uhakika cha kuendesha shughuli zao za kulinda rasilimali za Uvuvi lakini pia
mapato hayo yatawezesha kuendeleza sekta ya uvuvi tofauti na ilivyo sasa,”
alisema Dkt. Mlalila
Katika
baadhi ya Halmashauri ambazo wamewapa kazi BMU ya kukusanya mapato kama vile
Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga, Mapato yanayotokana na uvuvi
yameongezeka kutoka shilingi milioni 9 kwa robo mwaka hadi milioni 51 na kutoka
shilingi milioni 36 hadi milioni 256 kwa mwaka.
“Nazishauri
Halmashauri nyingine zichukue mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kwa
sababu sisi tumezipa mafunzo ya kina hizi BMU katika kusimamia fedha na
ukusanyaji wa mapato, hivyo tunaamini hilo ni suala la mchakato na
tumewasilisha andiko TAMISEMI ili kuangalia namna ya kuzifanya BMU kuendelea na
shughuli zake hata pale ambapo mradi wa SWIOFish utakapokwisha muda wake,”
aliongeza Dkt. Mlalila
Akizungumzia
suala hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alisema kuwa BMU ya
kata ya Dunda na zingine zikajifunze Pangani kuona wao wanafanyaje na sisi kama
Wizara tutaangalia kama kuna chanzo ambacho wataalam wa Halmashauri wanakusanya
na hakifanyi vizuri na kuna BMU mahali inakusanya vizuri basi tutaibua hiyo
hoja tuone tutafanyaje.
“Ukweli
ni kwamba kwenye vyanzo hivi vya leseni na ushuru wa rasilimali za uvuvi katika
halmashauri zetu nyingi hazifanyi vizuri na hivyo kuna haja ya kuviangalia
vizuri hasa wataalam wetu wanaotumika kukusanya hayo mapato kwa sababu kuna
baadhi yao wamefanya hapo ndio maeneo yao ya kupatia pesa zao,” alisema Gekul
Alisema
Wakurugenzi wanaweza kuwa na nia njema kabisa lakini wale wanaotumwa kukusanya
hayo mapato wanarudisha maduhuli hayo kama walivyotumwa? Kama kuna watu
wanauwezo wa kukusanya zaidi ya wataalam wa Halmashauri sidhani kama kuna haja
ya kuwa na kigugumizi cha kuwatoa hao watu ili kazi hiyo apewe anayeweza
kukusanya vizuri.
“Kwa
sababu mwisho wa siku sisi wananchi tunachotaka ni maendeleo hivyo nisingependa
niseme moja kwa moja hapa kuwa BMU wapewe kazi hiyo isipokuwa Halmashauri
ziangalie kama sheria inawaruhusu kuwatumia BMU kukusanya mapato,” aliongeza
Gekul
Gekul
alisema kuwa wao kama Wizara watawasiliana na TAMISEMI kuona maelekezo yakoje
kwa sababu anasema kuna vyanzo Halmashauri zenyewe zinakusanya na vingine
vinaruhusiwa kukusanywa na wakala na pale ambapo BMU itaonekana inafaa ipewe
uwezo wa kukusanya.
Mradi
wa SWIOFish unafadhiliwa na Benki ya Dunia kuhamasisha ulinzi na usimamizi wa
rasilimali za bahari na ndio umeimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi wa
rasilimali za bahari (BMU) kwa ajili ya kulinda na kuhamasisha uvunaji endelevu
wa rasilimali za bahari katika Wilaya za Mkinga, Pangani, Bagamoyo, Lindi
Vijijini na Tanga Jiji.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila (kulia) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Kikundi Cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo Januari 7, 2021.
Mwenyekiti
wa Kikundi cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU), Kata ya Dunda,
Wilayani Bagamoyo, Isihaka Hudi (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa
Ofisi ya BMU hiyo Januari 7, 2021.
Mratibu
wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya
Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa
ofisi ya Kikundi cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) inayojengwa
katika Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo Januari 7, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni