Katibu Mkuu Wizara ya Mifugp na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wafugaji wanaposhirikishwa katika uchangiaji wa miradi mbalimbali kwa ajili ya mifugo yao wamekuwa wakionyesha utayari na kufanya miradi hiyo kudumu kwa kuwa wanajisikia kuwa sehemu miundombinu hiyo.
Akizungumza (30.11.2020)
katika bwawa la kunyweshea mifugo maji la Elwaniolera lililopo kijiji cha
Eluwai, Kata ya Monduli Juu, Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha, Prof. Gabriel
amesema wakazi katika eneo hilo wameonesha utayari wa kulifanyia ukarabati
bwawa hilo linalohudumia zaidi ya wafugaji 2,000 katika vijiji vya Eluwai,
Emairete na Enguiki kutokana na kina cha bwawa hilo kupungua kutokana na
shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo ya kilimo.
“Uongozi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Monduli umenieleza kuwa wakazi wa Kata ya Monduli Juu wako tayari
kushiriki kwa kiwango kikubwa katika kulifanyia maboresho bwawa hili, wafugaji
wanaposhirikishwa nao wako tayari kushiriki na faida yake kubwa hakutakuwa na
haja ya serikali kugharamia kila kitu lakini pia wanaposhirikishwa mara zote
miundombinu hiyo huwa inadumu kwa kuwa nao watajisikia sehemu ya miundombinu
hiyo.” Amesema Prof. Gabriel.
Ameongeza kuwa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi ipo tayari kulikarabati Bwawa la Elwaniolera kwa kujenga
mabirika kwa ajili ya mifugo kunywea maji kwa kuwa hali ilivyo sasa ni hatari
kwa mifugo, wachungaji pamoja na usalama wa bwawa lenyewe.
Aidha, Prof. Gabriel amesema
wizara itaangalia namna ya kuboresha masuala ya majosho katika vijiji vya Eluwai,
Emairete na Enguiki ili kuhakikisha kwamba dhana nzima ya kuboresha afya ya
mifugo inafanikiwa.
Pia, amesema wakati Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizindua Bunge
la 12 alifafanua kuwa angependa kuona Sekta ya Mifugo inachangia zaidi katika
uchumi.
Amebainisha kuwa kwa sasa
Sekta ya Mifugo inachangia kwa asilimia 7.64 na inakuwa kwa asilimia tano
ambapo lengo la wizara ni kuhakikisha sekta hiyo ifikie kuchangia kwa zaidi ya
asilimia 15.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Kata ya
Monduli Juu ina mifugo mingi hivyo masuala ya malisho na afya ya mnyama ni
muhimu kwa kuwa na mifugo mingi na bora ni muhimu kushirikiana na Halmashauri
ya Wilaya ya Monduli ili wafugaji waweze kunufaika kupitia Bwawa la Elwaniolera
ili maji yake yaweze pia kutumika katika shughuli nyingine za kilimo cha
umwagiliaji.
Kwa upande wake Afisa Mifugo
wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Dkt. Yandru Marmo amemueleza Prof. Gabriel
kuwa Bwawa la Elwaniolera limeanza kupungua kina chake kutokana na shughuli za
kibinadamu zinazoendelea katika chanzo cha maji ya bwawa hilo, hali
inayosababisha udongo kusafirishwa hadi kwenye bwawa na kusababisha kina chake
kuzidi kupungua na kuhofia madhara makubwa kwa wafugaji wanaolitegemea
kunyweshea mifugo maji.
Dkt. Marmo ameongeza kuwa ni
muhimu kwa bwawa hilo kufanyiwa ukarabati kwa kuwepo kwa mabirika ya kunyweshea
mifugo maji ili mifugo isiingie ndani ya bwawa kwa kuwa inachangia pia udongo
kuingia ndani ya bwawa pamoja na shughuli za kibinadamu ikiwemo ya kilimo
zisifanywe karibu na chanzo cha maji ya bwawa hilo ili kuzuia pia udongo
kusafirishwa hadi kwenye bwawa na kusababisha kina chake kupungua.
Bwawa la Elwaniolera lililopo
Kata ya Monduli Juu, Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha, lilijengwa mwishoni mwa
miaka ya 1970 kwa jitihada za serikali wakati Hayati Edward Moringe Sokoine
akiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Muonekano wa Bwawa la
Elwaniolera lililopo Kata ya Monduli Juu, Wilaya ya Monduli, Mkoani Arusha
ambalo linakabiliwa na changamoto ya kupungua kwa kina chake kutokana na kujaa
udongo unaosababishwa na mifugo kunywea maji ndani ya bwawa pamoja na chanzo
cha maji ya bwawa hilo kusafirisha udongo hadi kwenye bwawa kutokana na
shughuli za kibinadamu ikiwemo ya kilimo zinazofanywa katika chanzo hicho.
(30.11.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni