Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa serikali inatumia zaidi ya shilingi Milioni 900 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa Mabwawa mawili ya kunyweshea mifugo ya Narakauo lililopo Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara na Bwawa la Kimokuwa lililopo Wilayani Longido, Mkoani Arusha.
Prof. Gabriel alieleza hayo
alipokuwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa mabwawa hayo
katika Mikoa ya Arusha na Manyara Novemba 7, 2020.
Akiongea na Wafugaji wa
maeneo hayo baada ya kufanya ziara hiyo, Prof. Gabriel alisema kuwa bwawa la
Narakauo limetengewa milioni 413 wakati bwawa la Kimokuwa limetengewa milioni
511.9.
Prof. Gabriel alieleza kuwa
ukarabati huo ni utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Rais, Dkt. John
Magufuli alipokuwa Mkoani Manyara hivi karibuni ya kuhakikisha Wizara ya Mifugo
na Uvuvi inafanya jitihada za dhati kutatua changamoto ya maji kwa mifugo.
Aliongeza kuwa, mbali na
ukarabati wa mabwawa hayo mawili, miradi kama hii ya ukarabati wa mabwawa ya
kunyweshea mifugo unaendelea pia katika Kata ya Chamakweza, Chalinze, Mkoani
Pwani na mwingine wa Kata ya Mbangala, Mkoani Songwe upo katika hatua za
kukamilika, huku akisisitiza kuwa Wizara itaendelea kuboresha upatikanaji wa
maji kwa mifugo ili wafugaji waondokane na kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Aidha, Prof. Gabriel alitumia
nafasi hiyo pia kuitaka kampuni ya Ujenzi ya Zeco ambayo ndio imepewa jukumu la
kukarabati mabwawa hayo mawili ya Narakauo na Kimokuwa kuhakikisha kuwa miradi
hiyo inakamilika kabla ya Novemba 25, 2020 ili kukwepa changamoto ya mvua.
“Ongezeni nguvu na spidi ya
ujenzi huu ili muukamilishe kabla ya mvua hazijaanza, mvua zikiwakuta kabla
hamjamaliza, kazi yote mliyoifanya itakuwa haina maana”, alisisitiza Prof.
Gabriel
“Tunategemea ujenzi wa
mabwawa haya uishe kwa wakati ili yaweze kusaidia wafugaji wetu ,mabwawa haya
yatawapunguzia wafugaji kutembea umbali mrefu kutafuta maji”, aliongeza Prof. Gabriel
Akizungumzia bwawa hilo,
Mfugaji, kijiji cha Narakauo, Petro Narotoka aliishukuru serikali kwa kutoa
pesa hizo kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo huku akiongeza kuwa mradi huo
ukikamilika utakuwa ni msaada mkubwa kwa mifugo na jamii kwa ujumla.
“Ujenzi huu ukikamilika
tutajitahidi sisi kama wafugaji kulinda miundo mbinu ya bwawa hili ili idumu
kwa muda mrefu kwa faida ya jamii yetu”, alisema Narokota
Naye, Mfugaji wa kijiji cha
Kimokuwa, Wilayani Longido, Mkoani Arusha, Kasaine Lamaiba alisema kuwa uamuzi
huo wa serikali wa kujenga bwawa katika kijiji hicho umeonesha ni kwa kiasi
gani serikali inathamini wafugaji nchini.
“Ujenzi wa bwawa hili
utasaidia pia visima vya asili vilivyopo hapa kijijini kutumika kwa muda mrefu
bila kukauka kwa sababu uwepo wa bwawa hili utaongeza chanzo cha uhakika cha
maji”, alisema Lamaiba
Aidha, prof. Gabriel aliuomba uongozi wa
Halmashauri za Wilaya hizo za Longido na Simanjiro kuendelea kutoa ushirikiano
ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati huku akiwaomba kuendelea kuwaandaa
jamii kutunza miradi hiyo pindi itakapokamilika.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa Kampuni ya Ujenzi ya Zeco, Bw. Gerald Oswald (kulia) alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa bwawa la kunyweshea maji mifugo la Narakauo lililopo wilayani Simanjiro, mkoani Manyara. (07.11.2020)
Diwani Mteule wa Kata ya Laibor siret, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, Ezekiel Lesenga (wa pili kulia)
akimueleza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante
Ole Gabriel (kushoto) alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa
la kunyweshea maji mifugo lililopo katika Kijiji cha Narakauo. (07.11.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiendesha moja ya Mtambo unaotumika
katika ujenzi wa bwawa la kunyweshea maji mifugo lililopo katika Kijiji cha
Kimokuwa, wilayani Longido, mkoani Arusha alipofanya ziara ya kukagua maendeleo
ya ujenzi. (07.11.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiongea na wafugaji wa
kijiji cha Narakauo, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara alipokuwa njiani
kuelekea mkoani Arusha muda mfupi baada ya kukagua ujenzi wa bwawa la
kunyweshea maji mifugo katika kijiji hicho. (07.11.2020)
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliosimama) akiwa katika picha ya pamoja na Wafugaji na Viongozi wa Kampuni ya ujenzi ya Zeco alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa bwawa la kunyweshea maji mifugo lililopo katika kijiji cha Kimokuwa, wilayani Longido, mkoani Arusha. (07.11.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni