Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Mahmoud Kimbokota amewataka Wavuvi mkoani Lindi kuzingatia sheria na taratibu zinasimamia uvunaji wa rasilimali za Bahari.
Kimbokota aliyasema hayo
alipokutana na timu ya Wataalamu wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali
za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOfish) walipokwenda kufanya
ufuatiliaji na kutathimini maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, mkoani Lindi Septemba, 28, 2020.
Akiongea na timu hiyo wakati
akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa SWIOfish, Kimbokota alisema kuwa Wavuvi
wanatakiwa kutambua kuwa uvuvi ni shughuli rasmi ya kujipatia kipato kama
zilivyo shughuli nyingine, hivyo ni lazima waiheshimu na kuithamini.
“Wavuvi ni lazima wazingatie sheria
na taratibu, na wabadilike,ule uvuvi wa kutumia Mabomu, Kokoro na matumizi ya
nyavu haramu waache, kila mvuvi awe mlinzi na mwalimu wa mwenzake, uvuvi haramu
tuukomeshe sisi wenyewe,” alisema Kimbokota
“Uvuvi wa kutumia mabomu
haufai, kwanza ni hatari kwa maisha yao, pia unaharibu mazalia ya samaki na
mazingira ikiwemo uoto wa miti ya mikoko, miti ya mikoko ni lazima iachwe ili
kulinda mazalia ya samaki baharini,” aliongeza Kimbokota
Kimbokota aliishukuru
Serikali kwa kupeleka mradi wa SWIOfish Wilayani humo na kusema kuwa jamii imeanza kubadirika, huku akiiomba
Serikali kuendelea kuwawezesha wavuvi ili waweze kukuza mitaji yao na kupata
zana za kisasa na kuachana na matumizi ya zana za kienyeji.
“Mradi uendelee kutoa elimu kwa wavuvi ili maeneo
yote ya Uvuvi yaendelee kuwa Salama na wavuvi wafanye shughuli zao kwa kufuata
sheria na taratibu,”alisisitiza Kimbokota
Kimbokota aliongeza kwa
kusema kuwa kutokana na uboreshwaji wa usimamizi wa rasilimali uliofanywa na
mradi hususani katika eneo la doria, wavuvi wameanza kufuata sheria na taratibu
na umesababisha kudhibitiwa vizuri kwa mapato ya Halmashauri.
“Kutokana na kuimarishwa kwa
doria Halmashauri imeweza kudhibiti mapato yatokanayo na shughuli za uvunaji wa
rasilimali za baharini, na mapato yamepanda kutoka shilingi Milioni 13. 5 mwaka
2015 hadi kufikia shilingi Milioni 29.9 mwaka 2020, hili ni ongezeko la zaidi
ya asilimia 50,” alifafanua Kimbokota
Aliendelea kueleza kuwa
kufuatia doria hiyo kumeisaidia Halmashauri kuwa na Takwimu sahihi ya vyombo
vya uvuvi vinavyotumika katika shughuli za uvuvi Wilayani humo, huku akisema
kuwa doria imepelekea pia uvuvi wa kutumia mabomu, makokoro na nyavu haramu
kupungua kwa kiasi kikubwa.
Aidha, aliushukuru mradi wa
SWIOfish kwa kuamua kujenga Ofisi ya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Bahari
(BMU) katika kijiji cha Sudi huku akisema kuwa ofisi hiyo itasaidia kuimarisha
ulinzi wa rasilimali za bahari na katika maeneo hayo na hivyo uvuvi haramu
hauna muda mrefu utakoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni