Nav bar

Alhamisi, 9 Julai 2020

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YADHAMIRIA KUFIKIA MALENGO YA KISEKTA KATIKA UCHUMI WA KATI.


Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendeleza jitihada za kuhakikisha inafikia malengo ya kisekta baada ya Tanzania kuorodheshwa na Benki ya Dunia hivi karibuni kuwa moja ya nchi zilizoingia katika uchumi wa kati ulioainishwa katika dira ya taifa ya mwaka 2020-2025.

Akizungumza wakati wa mafunzo rejea yanayotolewa na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kwa wafugaji katika wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mhandisi Mshamu Munde ameipongeza LITA kwa kutoa mafunzo hayo yenye lengo la kuifanya wilaya hiyo kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi ukiwemo ufugaji wa kuku kibiashara.

“Sisi sio wafugaji, sasa mafunzo haya yatasaidia kupanua wigo wa shughuli za kiuchumi ambapo licha ya wananchi kufanya shuguli za kilimo na uvuvi walizozizoea sasa watajishughulisha na ufugaji wa kibiashara  wa wanayama na ndege wafugwao kwa maana ya kuku”, alisema Mhandisi Munde.

“Wafugaji wengi wanafuga kuku wa kienyeji ambao siyo wa kibiashara na tunapoongelea kunyanyuka kiuchumi tunataka chakula lakini pia kupata kipato kwa ajili ya matumizi mengine”, aliongeza Mhandisi Munde

Pia Mhandisi Munde alisema kuwa, kupitia mafunzo hayo wanafunzi watajifunza kwa vitendo ufugaji wa kuku na hata watakapo toka watakwenda kufundisha jamii inayowazunguka.

Pia ameipongeza wizara ya mifugo na uvuvi kupitia kwa Naibu Waziri Abdallah Ulega kwa kuhamasisha ufugaji wa kuku kibiashara katika maeneo mbalimbali nchini. Vilevile kwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa Oktoba 4, 2019 ya kutoa vifaranga vya kuku aina ya kroiler kwa vikundi 25 vya wilaya hiyo vilivyohudhuria mafunzo katika kipindi hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya mapinduzi makubwa katika sekta za mifugo na uvuvi kwa kuhamaisha ufugaji endelevu na ufugaji bora kote nchini.

Dkt. Mwilawa amesema wizara imekuwa ikifanya mkakati wa kuboresha uzalishaji na biashara ya ndege wafugwao wakiwemo kuku, kwa kuwa kaya nyingi nchini zimekuwa zikitegemea ufugaji wa kuku ambao umekuwa na faida kwa kaya kwa kuboresha lishe na kipato na pato la taifa. Hivyo wizara inaendelea kuhimiza ufugaji wa kuku kwa kuwa mtaji wake ni mdogo na mfugaji anaweza kuongeza mtaji kuwa mkubwa endapo atafuata masharti ya ufugaji bora.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utafiti kutoka Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA), Bw. Silaju Kapembe akitoa mafunzo kwa wafugaji hao amewataka kabla ya kuanza kufuga kuku ni muhimu kuandaa mazingira bora ili kuhakikisha vifaranga vinamudu mazingira ya awali.

Bw. Nyanza Mwinshehe ambaye ni mfugaji ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuandaa mafunzo ya ufugaji bora wa kuku na kuiomba wizara hiyo kuweka mkazo zaidi wa shughuli za ufugaji katika Wilaya ya Mkuranga ili kuongeza wigo wa shughuli za kiuchumi zitakazosaidia kuongeza kipato.

LITA imekuwa na malengo makuu ya kutoa mafunzo kwa wafugaji wakiwemo wa kuku katika wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani ili kuondokana na ufugaji wa mazoea na kwenda kwenye ufugaji wenye tija na endelevu. Mafunzo hayo yamejumuisha walimu kutoka shule tano za msingi zilizopo wilayani Mkuranga ambazo pia zitapatiwa vifaranga vya kuku aina ya kroiler vikiwa na umri wa wiki tatu.

Picha ya pamoja, Mkurugenzi Mtandaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani Dkt. Angello Mwilawa wakiwa na wafugaji baada ya mafunzo rejea ya ufugaji wa kuku. (08.07.2020)

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa akizungumza na wafugaji (hawapo pichani) na kuwahamasisha kufuga kwa tija. (08.07.2020)

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, Mhandisi Mshuma Munde akizungumza wakati akifungua rasmi mafunzo rejea ya siku mbili kwa wafugaji katika wilaya hiyo yanayoendeshwa na wakufunzi kutoka Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA). (08.07.2020)

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki Ubora kutoka LITA Bw. Zuberi Mbwana (aliyesimama) akitoa elimu juu ya ufugaji bora wa kuku kwa wafugaji. (08.07.2020)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni