Wadau wa Mfuko wa maendeleo
ya Mifugo (LDF) wakutana kujadili hatma ya tasnia ya ngozi hasa baada ya kuisha
kwa ugonjwa wa Corona.
Kikao hicho kimefanyika jana katika
ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo jengo la NBC jijini Dodoma ambapo
wadau hao kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara,
Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Taasisi ya Teknolojia Dar-es-salaama tawi la Mwanza na
wengine walishiriki.
Akifungua kikao kazi hicho,
Mkurugenzi wa Masoko na Uzalishaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Felix
Nandonde alibainisha kuwa tasnia ya ngozi iliathiriwa na janga la Corona lililosababisha
hivi sasa ngozi inayozalishwa hapa nchini kutouzwa tena nje ya nchi hata ikiwa
katika nusu hatua ya usindikaji.
“Lakini katika kikao hiki
mbali na kujadili matumizi ya fedha pia kitumike kujadili mbinu za kuikwamua
tasnia hii ya ngozi kutoka kwenye hali iliyopo kwa sababu mpaka hivi sasa nchi
yetu inaagiza zaidi ya pea milioni 52 huku uwezo wetu wa kuzalisha viatu ukiwa
ni milioni 1.2 tu kwa mwaka” Alisisitiza Dkt. Nandonde.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya
Teknolojia Dar-es-salaam (DIT) Tawi la Mwanza Dkt. Albert Mmari alisema kuwa
taasisi yake ilishaanza kuchukua hatua kadhaa za kuongeza thamani kwenye tasnia
ya ngozi ikiwemo kuongeza mashine za mafunzo ya kutengenezea viatu ambapo mpaka
sasa zipo 50 ukilinganisha na 25 zilizokuwepo hapo awali.
Dkt. Mmari amesema kuwa DIT kupitia
benki ya dunia imepata zaidi ya shilingi bilioni 37 ambazo zitatumika kwenye
mradi wa miaka mitano ya kuboresha miundombinu ya chuo ikiwemo kununua mashine
za kisasa za kufundishia, studio za kubuni mitindo mipya ya viatu na bidhaa
nyingine zitokanazo na ngozi, kujenga madarasa ambapo mara baada ya kukamilika
kwa madarasa hayo yatakuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi zaidi ya 1000.
Akielezea hatua
zilizochukuliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha inaongeza
thamani ya ngozi, Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa chakula na
lishe Bw. Gabriel Bura alisema kuwa mpaka sasa Wizara imeshatoa mafunzo kwa
zaidi ya wachunaji 735 katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Mwanza,
Simiyu, Shinyanga, Morogoro na Kagera na tayari mchakato wa kutoa leseni kwenye
mikoa hiyo umeshaanza.
Vilevile wizara imeanza
kugawa visu vinavyotakiwa kitaalam kwa ajili ya kazi ya uchunaji katika mikoa
ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara na mchakato wa kuhakikisha vinafika katika
kanda zote tulizotoa mafunzo unaendelea.
Bw. Bura alisema kuwa hatua
iliyopo hivi sasa ni kusubiri tu nyaraka za uteuzi wa wakaguzi wa Ngozi waliopatikana
kutoka kwenye Halmashauri 113 ambao tayari wameshapitishwa na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kusainiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Baada ya taratibu
kukamilika wataalam hao watakuwa na jukumu la kuhakikisha wanasimamia ubora wa
ngozi kama ulivyoainishwa kwenye sheria namba 18 ya masuala ya Ngozi.
Katika kikao hicho pia wadau
walifanya tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka wa fedha 2019/2020 na
kujadili changamoto zilizosababisha kutotekelezwa baadhi ya vipengele vya
mpango kazi huo.
Mkurugenzi wa Masoko na
Uzalishaji Dkt. Felix Nandonde akifungua kikao cha wadau wa Mfuko wa Maendeleo
ya Mifugo (LDF) kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi
zilizopo katika jengo la NBC, Dodoma. Lengo la kikao hicho ni kujadili hatma ya
tasnia ya ngozi nchini. (14.07.2020)
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura akizungumzia
namna Wizara ilivyotekeleza shughuli mbalimbali kwa lengo la kuinua tasnia ya
ngozi nchini katika kikao kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo
na Uvuvi zilizopo katika jengo la NBC, Dodoma. (14.07.2020)
Mkurugenzi wa taasisi ya
Teknolojia Dar-es-salaam (DIT) tawi la Mwanza, Dkt. Albert Mmari akielezea
namna taasisi yake ilivyotekeleza mpango wa kuinua tasnia ya ngozi nchini
wakati wa kikao cha wadau wa Mfuko wa Maendeleo ya Mifugo (LDF) kilichofanyika
katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo katika jengo la NBC,
Dodoma. (14.07.2020)
Sehemu wa wadau wa Mfuko wa
Maendeleo ya Mifugo (LDF) wakifuatilia mjadala wa hatma ya tasnia ya ngozi
nchini wakati wa kikao kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na
Uvuvi zilizopo katika jengo la NBC, Dodoma. (14.07.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni