TUTAHAKIKISHA WAFUGAJI WOTE WANAFUGA KISASA NA KWA TIJA- DKT. MRUTTU
Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo, Dkt. Hassan Ally Mruttu amewataka wafugaji mkoani Pwani kufuga kisasa na kwa tija huku wakichukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya korona. Akiongea wakati wa Mafunzo elekezi na uhamasishaji kwa ajili ya kupandisha ng'ombe kwa njia ya chupa (uhimilishaji) kwenye kijiji cha Mkwalia kitumbo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga jana ( 22/04/2020) Dkt. Mruttu amesema lengo la Mafunzo hayo ni kutaka wafugaji kufuga kisasa na kupata Mifugo iliyo bora na mizuri ili kuwezesha wafugaji kufaidika na Mifugo yao. "Ni jukumu la Wizara kuhakikisha wafugaji wote nchini wanapata mbegu bora kwa njia ya uhimilishaji ili kupata Mifugo iliyo bora." Alisema Dr. Mrutu. Aidha ametoa wito kwa wataalam wa Mifugo kuwa tayari wakati wowote kuwasaidia wafugaji pindi wanapotaka kupandikiziwa mbegu bora kwenye Mifugo yao. Naye Mtafiti wa Mifugo, Bi. Neema Urassa kutoka taasisi ya utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI...