Nav bar

Jumanne, 22 Aprili 2025

SERIKALI KUENDELEA KUWEZESHA UFUGAJI WA KISASA

Na Hamisi Hussein - WMUV, Mwanza.

⬛️ Mhe. Mnyeti akikabidhi Mitamba 10 ya Maziwa kwa UWAMATA

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuwezesha ufugaji wa kisasa ili kuongeza tija katika uzalishaji na kukuza uchumi wa wafugaji nchini.

Hayo yameelezwa leo Aprili 19, 2025 na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alaxender Mnyeti wakati wa kukabidhi ng'ombe 10 wa Maziwa kwa kikundi cha Umoja wa Mapadri Tanzania (UWAMATA) hafla iliyofanyika katika Shamba la Uzalishaji Mifugo lililopo Misungwi mkoani Mwanza.

Mhe. Mnyeti amesema lengo la serikali nikuona inawezesha ufugaji wa kisasa kwa kuhimiza wafugaji kuwa na mifugo michache yenye tija itakayotoa mazao bora yanayokidhi  ushindani wa masoko.

" Mhe. Rais wetu anataka kuona ufugaji wa Kisasa unakuwa na tija kwa wafugaji na sisi Wizara tunaendelea kuhimiza ufugaji wa kisasa ambapo tumekuwa tukihamasisha ulimaji wa malisho ambayo yametajwa na wataalam wetu kuwa yanaprotini nyingi" alisema Mhe. Mnyeti.

Kuhusu ng'ombe wa maziwa (Mitamba) waliotolewa na serikali kwa Kikundi cha Umoja wa Mapadri Tanzania  (UWAMATA) Mhe. Naibu Waziri Mnyeti amesema zoezi la upandikizaji wa ng'ombe hao limefanywa na Wataalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwa na uhakika wa uzalishaji wa ng'ombe hao.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Mapadri Tanzania (UWAMATA) Padri George Nzungu ameishukuru serikali kwa kuwapatia ng'ombe hao kwani wataleta tija ya uzalishaji wa maziwa na kuahidi kuwa balozi wa ufugaji wa kisasa kwa wananchi wanaozunguka eneo lao.

Aidha Mkurugenzi Msaidi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko Dkt . Yeremia Sanka amesema ng'ombe hao waliopatikana kutokana na upandikizaji wa mbegu za madume halisi ya maziwa (Friesian) na majike ya kienyeji aina ya Boran na  watazalisha kati ya lita 8  hadi 12 kwa siku tofauti na ng'ombe wa asili ambaye anatoa maziwa lita 1.5 hadi 3 tu kwa siku.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (Mwenye Fimbo) akiwa Kwenye Picha ya Pamoja  na Mapadri wakati wa Makabidhiano ya Majike 10 ya maziwa kwenye Shamba la uzalishaji Mifugo Mabuki, Mwanza Aprili 19, 2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti  akizungumza na Mapadri waliopo kwenye Umoja wa Mapadri Tanzania (UWAMATA) wakati wa makabidhiano ya Majike 10  ya maziwa yenye mimba kwenye Shamba la uzalishaji Mifugo Mabuki, Mwanza Aprili 19, 2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (Kulia) akimkabidhi Mwongozo wa ufugaji wa ng'ombe wa Maziwa Padri Samweli Massawe(Katikati) wakati wa Makabidhiano ya Majike 10 ya maziwa kwenye Shamba la uzalishaji Mifugo Mabuki, Mwanza Aprili 19, 2025.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (Kulia) akimkabidhi Boski la Dawa ya kuongeshea ng'ombe wa Maziwa Padri Samweli Massawe wakati wa Makabidhiano ya Majike 10 ya maziwa kwenye Shamba la uzalishaji Mifugo Mabuki, Mwanza Aprili 19, 2025.

Mitamba ya Maziwa ilitokana na madume halisi ya maziwa (Friesian) na Majike ya asili aina ya Boran ikichunga katika Shamba la Mifugo Mabuki kabla la hafla ya makabidhiano baina ya Naibu Waziri  wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti  na Umoja wa Mapadri Tanzania UWAMATA hafla iliyofanyika Shamba la uzalishaji Mifugo Mabuki lililopo Misungwi, Mwanza Aprili 19, 2025.



 




Jumatano, 16 Aprili 2025

TDB YAHIMIZWA KUENDELEA KUSAJILI WADAU WA TASNIA YA MAZIWA

Na. Stanley Brayton, WMUV 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul Mhinte ameihimiza Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kuendelea kuwatambua na kuwasajili wadau wa Tasnia ya Maziwa ili kuongeza Uzalishaji wa maziwa nchini.

Ndg. Mhinte amesema hayo wakati akizungumza na Watumishi wa TDB katika Kikao kazi kinachofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Aprili 16, 2025.

"kama wadau wa Tasnia ya Maziwa hawafahamiki na hawajasajiliwa, ni ngumu sana kufikia Malengo na kuzalisha Maziwa kwa wingi, kwani wanahitaji kutatuliwa changamoto zao, ikiwemo za Masoko ya Maziwa hayo" amesema Ndg. Mhinte 

Vilevile, Ndg. Mhinte amesema kuwa wadau wa Tasnia ya Maziwa wapo sehemu mbalimbali nchini, na ni vyema Vituo vya ukusanyaji Maziwa vikarekebishwa na kuongezwa, ikiwa pamoja na Usimamizi  mzuri ili Maziwa yakusanywe kwa wingi.

Ndg. Mhinte, pia amehimiza Bodi kubuni Miradi mbalimbali kama ya Bar za Maziwa ili kuhakikisha Watumishi wanayapata kiurahisi na kuongeza Pato la Taifa.

Naye, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Prof. George Msalya amesema kuwa leo wamekuwa na Kikao na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kujadili Maendeleo ya Taasisi yao hususani Maendeleo ya Tasnia ya Maziwa hapa nchini pamoja na utendaji kiujumla.

"tumepokea maagizo yote tuliopewa na Naibu Katibu Mkuu ambayo yatatujenga na kuongeza hali ya utendaji kazi katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku katika Tasnia ya Maziwa" amesema Prof. Msalya 

Halikadhalika, Prof. Msalya amesema kwa sasa Maziwa yanakusanywa katika vituo 258 maalum vya kukusanyia, na wataendelea kuongeza vituo vingine pamoja na Miradi mingine kama Bar za Maziwa ili kuhakikisha Maziwa yanapatikana kwa wingi nchini.

Prof. Msalya amebainisha kuwa kwa sasa Takwimu zinaonyesha kila Mtanzania mmoja anatumia takribani Lita 67.5 kwa mwaka, ila viwango vilivyowekwa Kimataifa kwa mtu mmoja kunywa Maziwa kwa mwaka ni Lita 200.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul Mhinte, akihutubia Watumishi wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), katika Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Prof. George Msalya, akizungumza na watumishi  wa Bodi hiyo, katika Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utumishi  na Utawala - Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bi. Victoria Masanja, akielezea kuhusu umuhimu wa utoaji Taarifa kwa Utumishi, katika  Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Afisa Matekelezo Mkuu - Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Juma Milinga, akielezea jinsi PSSSF inavyofanya kazi na Taratibu za kuomba Mafao kwa Mtumishi, ni katika Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Meneja Fedha Utawala na Rasilimali Watu - Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bw. Walter Vasolela, akichangia  hoja katika Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Mchumi - Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bw. Davis Wambura, akifanya mapitio ya Mpango Mkakati wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) ya mwaka 2025/26 na kuelezea Utekelezaji wa Bajeti ya Bodi hiyo kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/25, katika Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Afisa Mteknolojia  wa Chakula - Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bi. Neema Moshi, akielezea umuhimu wa Ushirikishwaji wa Idara ya Sheria katika kuwawajibisha wadau wa Maziwa wanaoshindwa kufuata Taratibu za Kisheria katika Tasnia hiyo na umuhimu wa ushirikiano katika utendaji kazi, ni katika Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Afisa Mteknolojia wa Chakula - Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bw. Francisco Juma, akielezea kuhusu umuhimu wa kubuni vyanzo vya Mapato na kuweka Mikakati mizuri ya Ukusanyaji Mapato katika Bodi na swala la ushirikishwaji wa Watumishi katika kupanga Bajeti kwa kukaa pamoja na kujadili kipi Cha kufanya kwa Mwaka wa Fedha ujao, ni katika Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Mhasibu - Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bw. Christian Makawa, akielezea umuhimu wa kufungua Kituo cha Taarifa  za Maziwa (Information Center) ili wadau wa Tasnia ya  Maziwa wapate Habari zinazohusu Maziwa, ni katika Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Picha ni Watumishi wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), wakiwa katika Kikao kazi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul Mhinte (aliyesimama katikati mstari wa mbele), akiwa kwenye picha ya pamoja na Watumishi wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), baada ya Kikao kazi cha Watumishi wa Bodi hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House), Aprili 16, 2025, Dodoma


​KONGAMANO LA KITAIFA LA NGURUWE KUFANYIKA TANZANIA

Na. Chiku Makwai (MUV). Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikishirikiana na chama cha wafugaji wa Nguruwe Tanzania (TAPIFA) imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa la ufugaji wa nguruwe litakalo fanyika Septemba 11-13, 2025 jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Aprili 16, 2025 na Naibu Waziri, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti Wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari Uliofanyika katika Ukumbi uliopo jengo la NBC jijini Dodoma.

Mhe. Mnyeti amesema kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki takribani 2000 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika wakiwemo Viongozi wa Serikali na Wizara za kisekta, Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, Vijana na Wanawake, Wanataaluma, Wadau wa Maendeleo, Wafugaji na Wafanyabiashara katika mnyororo wa thamani wa Nguruwe.

Aidha, ameongeza kuwa kongamano hilo litaambatana na Mafunzo kutoka kwa wataalam na Wadau wa Maendeleo katika tasnia ya Nguruwe, pia washiriki kufanya majadiliano ya kibiashara na kuzitambua fursa zilizopo Kitaifa, Kikanda na Kimataifa pamoja na kutembelea uwandani kwa wadau kujionea namna ufugaji wa kisasa wa Nguruwe unavyofanyika.

Mhe. Mnyeti amebainisha kuwa ufugaji wa Nguruwe unaendana na malengo ya nchi katika kuhimiza maendeleo ya sekta ya mifugo ili kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa zinazotokana na Nguruwe.



Jumanne, 15 Aprili 2025

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUPANDA MALISHO YA MIFUGO

Na. Stanley Brayton, WMUV - Dodoma

◼️Waelezewa athari za kulisha Mifugo katika maeneo ya Hifadhi za Misitu.

Naibu Katibu Mkuu Wizara  ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul Mhinte, amewataka wafugaji Wilayani Bahi na Chamwino kupanda Malisho kwa ajili ya Mifugo ili kuepukana na changamoto za kukosa Malisho ya Mifugo.

Akizungumza katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika leo Aprili 15, 2025, Mkoani Dodoma, katika Kitongoji cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji cha Mayamaya, Wilaya ni Bahi, Ndg. Mhinte, amesema yapo maeneo muhimu ya Malisho ambayo yametengwa na Serikali ili kutatua changamoto za Malisho.

"yapo maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya Malisho japo yanapungua kadri Mifugo inavyozidi kuongezeka, na ni muhimu kuhakikisha kila mfugaji anapanda Malisho kwa ajili ya Mifugo yake" amesema Ndg. Mhite 

Vilevile, Ndg. Mhite amebainisha kuwa maeneo ya Malisho yanapungua kadri Mifugo na watu wanavyoongezeka, kiasi cha kwamba kunapelekea Misitu na Malisho kupungua au kutoweka kabisa.

Pia, Ndg. Mhinte ametolea ufafanuzi kuhusu athari za kulisha Mifugo katika maeneo ya Hifadhi ya Misitu, ikiwa ni pamoja na kuharibu Hifadhi hiyo na hatimaye kuamia katika Hifadhi zingine na kuziharibu na mwishowe kukosa Malisho kabisa pamoja na kuharibu Hifadhi hizo.

Ndg. Mhinte amesema kuwa Biashara ya kupanda Malisho imekuwa kama Dhahabu na hii ndio itakayosaidia wafugaji wengi katika kulisha Mifugo yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za vyakula za Mifugo. Dkt. Asimwe Rwiguza, amesema kwa sasa Serikali haitegemei Malisho ya asili kwa sababu haitoshelezi idadi ya Mifugo ambayo tunayo hapa nchini.

Dkt. Rwiguza amefafanua kuwa kwa sasa kuna namna ya kukabiliana na changamoto za Malisho, ikiwa ni pamoja na kulima Malisho, na ndio maana Serikali imetoa maeneo maalum kwa ajili ya kupanda Malisho na inaendelea kutoa mbegu hizo za Malisho na kutoa elimu namna ya kupanda hizo mbegu ili kuhakikisha kila mfugaji anakuwa nazo na anapandikiza katika eneo lake.

Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wote, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Bw. Kusundwa Wamalwa amesema zipo changamoto nyingi zinazowakumba wafugaji wengi hususan wa hapa Wilaya ya Bahi na Chamwino, ikiwemo Maji, Malisho na Masoko, kwa hiyo ni vyema Serikali  ikaangalia ni jinsi gani itaweza kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji hao 

Naye, Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kati ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Bw. Mathew Kiondo amesema miaka ya nyuma TFS ilitoa Hekta 2000 kwa wafugaji, ila kutokana na ongezeko la watu limepelekea Mahitaji ya Malisho kuwa makubwa kutokana na idadi kubwa ya watu na Mifugo, kwa hiyo wao kama TFS wataangalia ni jinsi gani wataweza kufanya ili kunasua wafugaji na changamoto ya uhaba wa maji kupitia Mfuko wa Kusaidia Jamii (CSR), ili kuwatengenezea Miundombinu ya maji kutoka kwenye Hifadhi ya Msitu wa Chenene kwenda kwenye maeneo yao ya Ufugaji.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul  Mhinte, akizungumza na Wafugaji wa Wilaya ya Chamwino na Bahi katika kikao chake na Wafugaji hao cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji cha Mayamaya, Wilayani Bahi, Dodoma, Aprili 15, 2025.

Katibu Tawala Msaidizi - Sekta za Uchumi Mkoa wa Dodoma, Bi. Aziza Mumba, akizungumza na Wafugaji na kuelezea umuhimu wa Sekta ya Mifugo katika kuchangia Pato la Taifa, katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji Cha Mayamaya, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.

MKurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za vyakula za Mifugo. Dkt. Asimwe Rwiguza, akitoa ufafanuzi kwa wafugaji juu ya umuhimu wa kupanda na Malisho kwa ajili ya Mifugo ili kutatua changamoto zao, katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji Cha Mayamaya, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Bw. Kusundwa Wamalwa, akimuelezea Naibu Katibu  Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), changamoto wanazokumbana nazo wafugaji nchi ikiwemo Maji, Malisho na Masoko, katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji Cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji cha Mayamaya, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.

Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kati ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Bw. Mathew Kiondo, akiwaelezea wafugaji umuhimu wa Hifadhi ya Msitu wa Chenene Mashariki na Magharibi ambao umeingia kwenye Halmashauri zote mbili za Bahi na Chamwino na kubainisha jinsi watakavyozitatua changamoto  za wafugaji katika Malisho na maji, katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji Cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji cha Mayamaya, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.

Mfugaji, Bw. Anthony Makaka, akiiomba Serikali kuweka utaratibu wa kupata Malisho ili kutatua changamoto zao ikiwa pamoja na kuwapatia mabwawa kwa ajili ya Mifugo na matumizi yao binafsi, katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji Cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji Cha Mayamaya, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.

Mfugaji, Bw. Manimba oloya, akielekeza  jinsi Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanavyokamata Mifugo yao wakati wanapoipeleka kwenye Malisho katika Hifadhi ya Msitu wa Chenene kutokana na kutoandaliwa sehemu za Malisho na kuwapatia elimu ya kutosha, katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji Cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji Cha Mayamaya, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.

Mfugaji, Bi. Kafutuku Kipara, akielezea changamoto alizokutana nazo za kuchukuliwa maeneo yake ya kufugia, katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji Cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji Cha Mayamaya, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.

Mfugaji, Bi. Katarina Garabuu, akielezea changamoto anazokumbana nazo akienda katika Hifadhi ya Msitu wa Chenene katika kutafuta Maji kwa ajili ya Mifugo, katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji Cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji Cha Mayamaya, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.
Mfugaji, Bw. Tadayo Sembuche, akilalamikia faini kubwa wanazotozwa na kunyang'anywa Mifugo baada ya kuingia Mifugo hiyo katika Hifadhi ya Msitu wa Chenene, katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika katika Kitongoji Cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji Cha Mayamaya, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.

Picha ni baadhi ya wafugaji, wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul  Mhinte (hayupo pichani), akielezea kuhusu, katika Kikao chake na Wafugaji hao cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika Mtungutu Kijiji cha Mayamaya kata ya Zanka, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul  Mhinte (waliokaa katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na Wafugaji wa Wilaya ya Chamwino na Bahi, baada ya Kikao chake na Wafugaji hao cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika Mtungutu Kijiji cha Mayamaya kata ya Zanka, Aprili 15, 2025, Bahi - Dodoma.






























DKT. MHINA AWATAKA WATUMISHI KUZINGATIA WELEDI, UAMINIFU NA WAJIBU

Na. Chiku Makwai (WMUV). Dodoma

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina amewataka watumishi wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kuzingatia weledi, uaminifu na wajibu katika kutekeleza majukumu yao.

Ameyasema hayo Aprili 15, 2025 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha  menejimenti pamoja na watumishi wa bodi hiyo kilichofanyika katika moja ya ukumbi ziliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Dodoma. 

Aidha,  Dkt Mhina ameipongeza TDB kwa kuendelea kupiga hatua katika utoaji huduma zilizo bora na amewasisitiza kuwa ili kupata maendeleo ni wajibu wa kila mtumishi kufanya kazi kwa bidii. 

Kwa upande wake Msajili Mkuu wa TDB Prof. George Msalya amesema kuwa Tasnia ya Maziwa inazidi kukua nchini na mpaka sasa kuna zaidi ya viwanda 152 vya uchakataji maziwa.

Vile vile ameongeza kuwa ipo mipango mbalimbali inayoandaliwa na kuratibiwa na bodi hiyo itakayolenga kuhamasisha unywaji maziwa nchini pamoja na manufaa yake.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina akizungumza jambo wakati wa kikao kazi cha Menejimenti pamoja na watumishi wote wa Taasisi ya Bodi ya Maziwa Tanzania kilichofanyika Aprili 15, 2025 jijini Dodoma.

Msajili wa Taasisi ya Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya akichangia jambo wakati wa kikao kazi hicho kilichofanyika Aprili 15, 2025 jijini Dodoma.

Sehemu ya Watumishi wa Taasisi ya Bodi ya Maziwa nchini walioshiriki katika kikaokazi cha Menejimenti pamoja na watumishi wake kilichofanyika Aprili 15, 2025 jijini Dodoma.






SHEMDOE ABAINISHA FURSA ZA MALISHO YA MIFUGO

Na. Omary Mtamike

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amewataka wafugaji nchini kuendelea kutenga maeneo ya kuzalisha malisho ya mifugo yao ili waendelee kuboresha afya za wanyama na kujipatia kipato baada ya kuyauza.

Prof. Shemdoe amesema hayo Aprili 14,2025 wakati akifungua kikao cha wataalam wa malisho ya Mifugo kilichofanyika mkoani Morogoro ambapo ametoa rai kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo kama wanavyofanya kwenye shughuli nyingine za kiuchumi.

“Tuwawezeshe vijana waanzishe mashamba ya kulima malisho kwa sababu nina uhakika masoko yapo na nina mfano wa mtu mmoja hapa Pwani yeye kila mwaka anauza tani nyingi za malisho na hana biashara nyingine zaidi ya hiyo” Ameongeza Prof. Shemdoe.

Aidha katika hatua ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita cha wataalam hao, Prof. Shemdoe amesema Wizara yake imeendelea kuajiri vijana wengi wanaotokana na shahada ya nyanda za malisho huku pia wakiendelea kutoa elimu kuhusu chakula stahiki kwa mifugo.

Akizungumza awali kabla ya kumkaribisha Prof. Shemdoe, Mwenyekiti wa chama hicho Prof. Ismail Selemani ameishukuru Wizara kwa kufanyia kazi baadhi ya maazimio ya wataalam hao ikiwa ni pamoja na kuboresha sheria ya Maeneo ya Malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo namba 180 ya mwaka 2010 na kuendelea kutenga maeneo ya malisho na uanzishwaji wa mashamba darasa ya malisho hayo.

Akigusia fursa inayotokana na malisho Visiwani Zanzibar, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo visiwani humo Dkt. Abdultwalib Suleiman amesema kuwa wafugaji waliopo huko wamekuwa na changamoto ya uzalishaji wa malisho kutokana na sehemu kubwa ya visiwa hivyo kuzungukwa na majengo na miundombinu mbalimbali hivyo amewataka wazalishaji wa malisho ya Mifugo kuzalisha malisho ya kutosha na kuyapeleka Zanzibar.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akitoa hotuba ya ufunguzi wa kikao cha Wataalam wa Malisho nchini kilichofanyika Aprili 14, 2025 mkoani Morogoro.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akimkabidhi zawadi ya cheti cha Andiko bora la biashara ya Mifugo Mwanafunzi Laurian Jackline Josephat kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wakati wa kikao cha Wataalam wa Malisho ya Mifugo kilichofanyika mkoani Morogoro  Aprili 14, 2025.

Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya (kulia) akiratibu kikao cha Wataalam wa malisho ya Mifugo nchini kilichofanyika Aprili 14, 2025 mkoani Morogoro.


Jumapili, 13 Aprili 2025

NDEGE NYUKI YAANZA RASMI KUWASAKA WAVUVI HARAMU ZIWA VICTORIA

Na Edward Kondela - WMUV, Mwanza

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mara ya kwanza imenunua na kuzindua matumizi ya ndege nyuki (drone) itakayofanya kazi ya kuimarisha usimamizi wa shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ndege nyuki hiyo jijini Mwanza Aprili 13, 2025 kwa niaba ya Mgeni Rasmi Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Alexander Mnyeti amesema serikali imeamua kuchukua hatua madhubuti za kisasa kuhakikisha inadhibiti uvuvi haramu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Mhe. Mnyeti ameongeza kuwa katika awamu hii wizara imetumia kiasi cha Shilingi Milioni 259, kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyuki, kutoa mafunzo kwa waendeshaji, kufunga vituo vya kudhibiti, kufanya usajili na kuanzisha mfumo wa kuhifadhi na kuchambua taarifa zinazopatikana kutoka kwenye ndege hiyo.

“Ndege nyuki hii ni kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria. Ndege nyuki hii ina uwezo wa kukimbia kwa mwendo kasi wa Kilometa 108 kwa saa na uwezo wa kuchukua picha za matukio kutoka umbali mita 350 na kuruka mita 120 kutoka usawa wa bahari na kusafiri umbali wa Kilometa 400 na kuweza kukaa angani kwa muda wa saa mbili.” amesema Mhe. Mnyeti

Aidha, amesema mpango wa matumizi ya ndege nyuki hautaishia Ziwa Victoria pekee, bali kupeleka matumizi hayo katika Ziwa Tanganyika na Nyasa, pamoja na maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi ili kuhakikisha kila pembe ya nchi inaonja matunda ya teknolojia ya kisasa katika usimamizi wa rasilimali.

Pia, amesema ndege nyuki hiyo ina uwezo wa kutoa taarifa kulingana na muda halisia na kwamba itasaidia kupunguza vitendo vya uvuvi haramu na gharama za uendeshaji wa doria ziwani pamoja na kutumika katika masuala ya utafutaji na uokoaji.

Amefafanua kuwa ndege nyuki hiyo ni kifaa cha kisasa kinachoruka angani bila rubani kwa lengo la kusaidia kuimarisha doria na usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kuwa kifaa hicho ni mali ya serikali, wizara itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi zingine za serikali kuimarisha ulinzi na usalama kwenye Ziwa Victoria.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede akizungumza katika hafla hiyo amesema uwepo wa ndege nyuki unaenda sambamba na takwa la kidunia la matumizi ya teknolojia rafiki za kimazingira.

Ameongeza kuwa katika mapambano ya uvuvi haramu serikali ililazimika kutumia boti na magari yanayotumia mafuta ya diesel ambayo yanaleta hewa ya ukaa kwa kiasi kikubwa ila kwa matumizi ya ndege nyuki, itakuwa ikienda eneo mahsusi ambalo kuna viashiria vya uvuvi haramu hivyo kupunguza matumizi ya boti na magari kwa ajili ya kuwasaka wavuvi haramu.

Kufuatia maelekezo ya Naibu Waziri Mhe. Mnyeti, katika kudhibiti uvuvi haramu Dkt. Mhede amebainisha kuwa atahakikisha anasimamia maelekezo hayo yakiwemo ya baadhi ya maafisa uvuvi kutuhumiwa kushiriki katika matukio ya uvuvi haramu.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema mkoa huo unategemea sana Sekta ya Uvuvi katika kukuza uchumi, hivyo kuzinduliwa kwa ndege nyuki kwa matumizi ya kudhibiti upotevu wa rasilimali za uvuvi kutasaidia kuwabaini wahalifu na kukomesha uvuvi haramu.

Amesema kama mkoa wamekuwa wakihakikisha doria zinafanyaika  mara kwa mara ili kuhakikisha maeneo yote ya Ziwa Victoria katika Mkoa wa Mwanza yanakuwa salama dhidi ya uvuvi haramu.

Baadhi wakazi wa jiji la Mwanza waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa ndege nyuki kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu, wamepongeza jitihada za serikali na kusema ni jambo la kipekee kuwa na kifaa hicho ambacho wameshuhudia namna kinavyofanya kazi kwa mara ya kwanza baada ya uzinduzi.

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka wazi kuwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 itatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyuki zaidi ili kuongeza wigo wa kudhibiti uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali nchini.



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi matumizi ya ndege nyuki (drone) kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria. (April 13, 2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa matumizi ya ndege nyuki (drone) kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, ambapo ametaka ndege hiyo itumike ipasavyo kukabiliana na vitendo hivyo. Hafla hiyo fupi imefanyika jijini Mwanza April 13,2025.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede akifafanua baadhi ya taarifa kuhusu Sekta ya Uvuvi wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa matumizi ya ndege nyuki (drone) kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria. (April 13, 2025)

Baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza wakiiangalia ndege nyuki (drone) maalum kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu, baada ya kuzinduliwa rasmi matumizi yake, ikiwa inaanza kuruka kuelekea angani kwa ajili ya kupiga picha katika Ziwa Victoria. (April 13, 2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti (katikati) akipata maelezo kutoka kwa marubani wanaorusha ndege nyuki (drone) kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, namna ndege hiyo inavyofanya kazi ikiwa angani na kuifuatilia nyendo zake kupitia televisheni. Kushoto kwa Naibu Waziri Mhe. Mnyeti ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede na anayemfuatia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi. (April 13, 2025)

Ndege nyuki (drone) yenye namba za usajili 5H-25038 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ambayo ni maalum kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu ikiwa angani kwa mara ya kwanza baada ya kuzinduliwa rasmi matumizi yake na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti, katika hafla fupi iliyofanyika jijini Mwanza, ambapo ndege nyuki hiyo imegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 259. Ndege hiyo imenunuliwa na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (April 13, 2025)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti akibonyeza kifaa maalum cha kuongozea ndege nyuki (drone) na kuiruhusu ndege hiyo kuruka baada ya kuizindua rasmi kwa ajili ya matumizi ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria. (April 13, 2025)

Muonekano wa ndege nyuki (drone) yenye namba za usajili 5H-25038 kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ikiwa ardhini kabla ya kuruka. Ndege hiyo imenunuliwa na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. (April 13, 2025)

Jumatano, 9 Aprili 2025

MIFUGO ZAIDI YA MILIONI 370 IMEPATIWA CHANJO DHIDI YA MAGONJWA

Na. Chiku Makwai - MUV, Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa chanjo kwa mifugo zaidi ya milioni 370 kwa lengo la kutibu na kuzuia magonjwa aina ya kiimeta na homa ya mapafu, pamoja na  mifugo kukidhi matakwa ya soko la kimataifa. 

Hayo yameelezwa leo (Aprili 9, 2025) na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati akitoa hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio na Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 bungeni jijini Dodoma. 

“Kwa kuimarisha huduma za ugani na kudhibiti magonjwa ya mifugo yanayovuka mipaka, katika kipindi cha Mwezi Julai, 2024 hadi Mwezi Januari 2025, serikali imenunua chanjo zenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.1 kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo nchin.i” amesema Mhe. Waziri Mkuu

Aidha Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa ufugaji wa kisasa unaozingatia malisho bora na idadi ya mifugo inayoweza kuleta tija kwa mfugaji serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo ambapo ujenzi wa mabwawa manne ya Bukabwa (Butiama), Kihumbu (Bunda), Isulamilomo (Nsimbo) na Kwenkikwembe (Kilindi).

Ameongeza kuwa kutokana na Kampeni ya Tutunzane Mvomero iliyozinduliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, uzalishaji wa mbegu za malisho umeongezeka kutoka tani 127.8 Mwaka 2023/2024 hadi tani 152.67 Mwaka 2024/2025 na uzalishaji wa malisho yaliyosindikwa umeongezeka kutoka tani 728.6 hadi tani 2,669.84.

Aidha, amesema kuwa kutokana na jitahada zilizofanyika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2024/2025 uzalishaji wa mifugo umeongezeka na kufikia milioni 189.8 kutoka mifugo milioni 181.8 Mwaka 2023/2024, Ongezeko hilo limechangia uzalishaji wa nyama kutoka tani 963,856.55 kwa Mwaka 2023/2024 hadi kufikia tani 1,054,114.03 Mwezi Februari, 2025.

Pia, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na huduma za chanjo ya mifugo, kujenga na kukarabati minada ya mifugo, kujenga machinjio ya kisasa na kuimarisha mashamba darasa ya malisho.

Kwa Upande wa Sekta Ya Uvuvi Mhe Waziri Mkuu amesema kuwa serikali imeendelea kutekeleza mradi wa mikopo nafuu kwa wananchi ili kuwekeza katika ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ambapo mikopo ya Shilingi Bilioni 36.64 imetolewa kwa wanufaika 7,130. Kupitia mikopo hiyo, ajira 3,000 za moja kwa moja, na zaidi ya 1,000 katika mnyororo wa thamani zimezalishwa.

Ameongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa bandari ya uvuvi katika eneo la Kilwa-Masoko na ujenzi huo utahusisha gati lenye urefu wa mita za mraba 315, jengo la utawala na vyumba baridi vya kuhifadhia samaki kwa gharama ya Shilingi Bilioni 289.5 umefikia asilimia 79 na ujenzi utakapokamilika unakadiriwa kuhudumia tani 60,000 za mazao ya uvuvi kwa mwaka na kutoa fursa za ajira takriban 30,000.

Mwisho Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 serikali itaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko mkoani Lindi pia kuanza ujenzi wa bandari ya uvuvi katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na kuimarisha huduma za utafiti, mafunzo na ugani.



Ijumaa, 4 Aprili 2025

WATUMISHI WA LITA WAHIMIZWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Na. Stanley Brayton

◼️Ataka watumishi kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina amewataka watumishi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) kuzingatia Kanuni za Maadili ya Utumishi wa umma kwani taasisi yeyote ambayo haizingatii maadili ya Utumishi wa Umma ni vigumu sana kupata utendaji wenye tija.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe leo Aprili 04, 2025 Dodoma katika Kikao cha Utoaji Taarifa za Mkutano wa Kumi na mbili (12) wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Mhina amesema kuna baadhi ya Watumishi wanashindwa kuzingatia Kanuni za maadili na Sheria za utumishi wa umma kutokana na uzembe na matokeo yake kuleta matokeo mabovu katika Taasisi.

"Tufanye kazi kwa bidii na kwa uaminifu kazini kwa kufuata misingi Mikuu ya Uadilifu, ikiwemo uwajibikaji na uaminifu," amesema Dkt. Mhina

Aidha, Dkt. Mhina amesema mtumishi anapaswa kutunza siri za ofisi kwa kutotumia taarifa za Serikali visivyo sahihi au bila idhini ya Utawala kwani Kanuni zinawataka kutunza taarifa kwa siri.

Vilevile, Dkt. Mhina ameitaka Menejimenti ya LITA kuwajengea watumishi wao uwezo na kuhakikisha wana utendaji mzuri kazi, na wanakuwa na uadilifu kwa kuzingatia Sheria na kanuni na Taratibu za Utumishi wa umma.

Dkt. Mhina amewapongeza LITA kwa mpangilio mzuri wa kampasi ambao zimekuwa zinatoa fursa mbalimbali zinazoonekana kwa wafugaji. 

Halikadhalika, Dkt. Mhina amesema bado kuna jukumu kubwa la kutoa mafunzo ya mifugo kwa wafugaji kwani chuo hakiwezi kuendelea kama hakiwekezi kwenye Miundombinu na ushirikishwaji wa jamii kwenye kutoa Mafunzo ya Mifugo.

Pia, Dkt. Mhina, ameipongeza Kamati ya Wajumbe wa Baraza Kuu LITA kwa kuendelea kujenga Vyuo vingine katika sehemu mbalimbali na amewataka Baraza kuisaidia Menejimenti katika kubuni Miradi mingine, ikiwa pamoja na kupima kama Mipango inaleta tija ambayo itaenda kufanya mabadiriko makubwa katika Taasisi baada ya miaka kadhaa ili kufanya maboresho makubwa zaidi.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Mwambene amesema wamepata nasaha kubwa kutoka kwa Mgeni Rasmi, na kuahidi kushirikishana katika Mipango yote ambayo imepangwa kwa Mwaka ujao wa fedha.

Dkt. Mwambene amesema wataendelea kuzingatia Maadili ya Utumishi wa Umma kwa kutekeleza Majukumu waliopewa na Serikali na kuwajibika ili kuleta matokeo chanya kwa Taasisi na nchi nzima.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni  Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina, akitoa Hotuba katika Kikao cha Utoaji Taarifa za Mkutano wa Kumi na mbili (12) wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar, Aprili 4, 2025, Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Mwambene, akielezea Historia ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) pamoja na Mafanikio na Changamoto za Taasisi hiyo, katika Kikao cha Utoaji Taarifa za Mkutano wa Kumi na mbili (12) wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Taasisi  hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar, Aprili 4, 2025, Dodoma.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) ambaye ni Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma Utafiti na Ushauri LITA, Dkt. Anna Ngumbi, akitoa neno la shukrani kwa Mgeni Rasmi (hayupo pichani), katika Kikao cha Utoaji Taarifa za Mkutano wa Kumi na mbili (12) wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Taasisi  hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar, Aprili 4, 2025, Dodoma.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni  Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina (katikati) na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Mwambene (kushoto), wakiimba wimbo wa  Mshikamano Daima wa Wafanyakazi wa LITA, katika Kikao cha Utoaji Taarifa za Mkutano wa Kumi na mbili (12) wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Taasisi  hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar, Aprili 4, 2025, Dodoma, kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi na Mkurugenzi  Msaidizi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Josephine Temihango (wa kwanza kulia), wakipitia Taarifa za Mkutano wa Kumi na mbili (12) wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Taasisi  hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar, Aprili 4, 2025, Dodoma.

Picha ni baadhi ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), wakiwa  katika Kikao cha Utoaji Taarifa za Mkutano wa Kumi na mbili (12) la Baraza hilo, kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar, Aprili 4, 2025, Dodoma.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambaye ni  Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), katika Kikao cha Utoaji Taarifa za Mkutano wa Kumi na mbili (12) wa Baraza Kuu la Wafanyakazi hao wa LITA, kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar, Aprili 4, 2025, Dodoma.