◼️ Awahimiza wataalam ushirikiano
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema katika kuendeleza na kukuza sekta za Mifugo na Uvuvi ataanzia pale alipoishia mtangulizi wake Mhe. Abdallah Ulega ili kuendelea kuzifanya sekta hizo kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la taifa.
Dkt. Kijaji amesema hayo Disemba 15, 2024 wakati wa makabidhiano ya nyaraka za ofisi baina yake na Mtangulizi wake huyo katika hafla fupi iliyofanyika Makao Makuu ya wizara, Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
“Kaka yangu, Mhe. Ulega umefanya kazi kubwa ya kuipaisha wizara hii na mimi nitaendelea kujifunza kutoka kwako ili niweze kukimbia na kasi ambayo Mhe. Rais anaitaka” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt. Kijaji ameongeza kuwa dhamira yake ni kuona sekta za Mifugo na Uvuvi zinakuwa miongoni mwa sekta muhimu katika ustawi wa uchumi wa Wananchi na taifa kwa ujumla huku akiwahimiza wataalamu kushirikiana hasa katika kuwahudumia wafugaji na Wavuvi ambao ndio wazalishaji wakuu wa uchumi wa sekta hizo.
Kwa upande wake aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amesema kwa kipindi cha miaka saba ndani ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wataalamu wamefanikiwa kuiweka Wizara hiyo kwenye twasira ya kitaifa kupitia miradi mikubwa iliyozinduliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambayo ni ujenzi wa bandari ya Kilwa Masoko, Ugawaji wa Vizimba na Boti kwa ajili ya ufugaji wa samaki.
"Mhe Waziri kitu ambacho ninajivunia katika miaka saba kwenye wizara hii ni utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko na ule wa ugawaji wa Vizimba na Boti kwa wavuvi hapa nchini kwa sababu ni miradi ambayo imekwenda kugusa wananchi moja kwa moja" alisema Mhe. Ulega
Mhe. Ulega ameongeza kwa kuwataka wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kumpa ushirikiano Mhe. Dkt. Kijaji ili aweze kuisaidia wizara kufanikisha usimamiaji wa miradi ili kuleta tija kwa Wananchi.
Awali akizungumza kwenye Makabidhiano hayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema Wizara itaendeleza maono ya Mhe Ulega katika kutekeleza majukumu ya wizara katika kukuza ustawi wa sekta za mifugo na uvuvi huku akimshukuru Waziri huyo kwa uongozi wake.