Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Wizara yake kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo watapeleka mradi wa 'Kopa Ng'ombe Lipa Maziwa' kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya vijijini ili kuwawezesha vijana na kinamama kujikwamua kimaisha.
Waziri Ulega aliyasema hayo alipofanya ziara kwenye Halmashauri ya mji Mdogo, Mbalizi, Wilaya ya Mbeya Agosti 5, 2023.
"Mbunge wenu ameniomba mambo mengi ikiwa pamoja na kuifanya Mbeya kuwa ni eneo la kielelezo la kufuga kisasa na kibiashara, hivyo, nitawatafutia mradi mzuri wa Kopa Ng'ombe Lipa Maziwa, Mbunge nataka uwatafutie uchumi watu wa hapa Mbeya", alisema Ulega
Waziri Ulega alimuelekeza Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mhe. Oran Njeza kufika katika Ofisi za Shirika la Heifer International na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya (TADB), mkoani humo kwa ajili ya kuanza taratibu za kuwezeshwa kupata mradi huo huku akimuahidi kuwa atahakikisha wananchi wa Mbeya vijijini wanapata mradi huo ili waweze kunufaika nao.
Naye, Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mhe. Oran Njeza alimshukuru Waziri Ulega kwa kuwapelekea mradi huo huku akisema kuwa mradi huo utasaidia sana kuinua uchumi wa Wananchi mkoani Mbeya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni