Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 Serikali imeshapeleka katika Halmashauri 80 jumla kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kwa ajili kukamilisha ujenzi wa majosho.
Mhe. Ulega aliyasema hayo Januari 31, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kalenga, Mhe. Jackson Kiswaga aliyetaka kujua ni lini serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga majosho katika jimbo lake.
Akijibu swali hilo, Mhe. Ulega alisema tayari Serikali imekwisha peleka kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya ujenzi wa majosho 257 na tayari majosho 88 yameshakamilika huku mengine 169 yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi na yanatarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2023.
Aidha, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Bupe Mwakang’ata ambaye alitaka kujua ni lini serikali itajenga majosho katika Kata ya Miula, wilayani Nkasi, Naibu Waziri Ulega alisema kuwa katika bajeti ya 2021/2022 serikali ilishapeleka kiasi cha shilingi milioni 108 kwa ajili ya ujenzi wa majosho katika Halmashauri ya Nkasi katika vijiji vya Pande, Katani, Chala, Mikukwe, Chalatila na Sintali ambayo yapo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa.
Aliongeza kwa kusema kuwa Wizara inaendelea kuwasiliana na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ili kukamilisha ujenzi wa majosho hayo na kutoa fursa kwa serikali kutenga fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi wa majosho mengine Wilayani Nkasi Kusini ikiwemo kata ya Milula.
Mhe. Ulega aliendelea kufafanua kuwa serikali inaendelea kuwahamasisha wafugaji kuendelea kushirikiana na serikali ikiwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo majosho.
Kuhusu swali la Mbunge wa Geita Mjini, Mhe. Constantine Kanyasu alilotaka kujua mikakati ya wizara kuhusu ujenzi wa majosho na kuyawekea maji ya uhakika, Naibu Waziri alisema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Maji wamekubaliana kufungamanisha maeneo yenye miundombinu ya maji kwa ajili ya binadamu wataweka na miundombinu kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni