Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka
wafugaji kuishi na watumiajiwengine wa ardhi kwa amani na sio kuleta migogoro.
Waziri Ndaki ameyasema hayo (02.11.2022) wakati akizungumza
na wananchi wa Kijiji cha Ngunichile wilayani Nachingwea mkoani Lindi alipofika
na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa lengo la kuwasikiliza wananchi wa
Kijiji hicho ambapo kuna mgogoro wa wakulima na wafugaji.
“Shughuli za ufugaji ni shughuli halali kama zilivyoshughuli
nyingine katika jamii, lakini shughuli hizi ni lazima zifanyike kwa kuzingatia
sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili ziweze kufanyika bila kuleta
migogoro,” Alisema
Waziri Ndaki amesema vitendo vya baadhi ya wafugaji kulisha
mifugo kwenye mashamba ya wakulima, kuwapiga na kuwaua ni vya kihalifu hivyo
watatafutwa kama wahalifu wengine na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Wafugaji wametakiwa kuishi kwa amani, kuwa na ushirikiano na
mahusiano mazuri katika jamii wanazoishi na kuacha tabia ya kuleta vurugu au
migogoro kwenye jamii hizo.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhandisi Hamad
Masauni amesema kutokana na tatizo la migogoro waliloliona kwenye mkoa wa Lindi
kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji amemuagiza Kamishna wa Operesheni na
Mafunzo Tanzania kuendesha operesheni ya kuwatafuta wafugaji waliosababisha
migogoro na kuchukua hatua.
Pia amewataka wafugaji kuzingatia mipango ya matumizi ya
ardhi iliyowekwa na kuhakikisha wanafuga mifugo kwenye maeneo yaliyotengwa kwa
ajili ya kazi hiyo, hivyo wafugaji ambao wamevamia maeneo bila kufuata taratibu
wametakiwa kutoka kwenye maeneo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni