Nav bar

Alhamisi, 17 Novemba 2022

WATENDAJI WATAKIWA KUFANYA MABADILIKO YA KIFIKRA KUKUZA SEKTA YA MIFUGO

Na. Edward Kondela


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Bw. Tixon Nzunda amewataka watendaji serikalini kufanya mabadiliko makubwa ya kifikra, kiutendaji na mifumo ya kiuendeshaji ili kukuza sekta za uzalishaji mali nchini.


Bw. Nzunda amebainisha hayo (04.11.2022) Mjini Unguja Visiwani Zanzibar, wakati akifungua kikao kilichowakutanisha baadhi ya wataalamu wa Sekta ya Mifugo wa wizara pamoja na taasisi na vitengo vinavyoshughulika na sekta hiyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo amesema sekta za uzalishaji mali ndizo zinazobeba uchumi wa nchi.


Amezitaja sekta za uzalishaji mali kuwa ni kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili ambazo zinabeba uchumi wa nchi hivyo watendaji serikalini wana wajibu wa namna ya kusimamia maslahi mapana ya nchi kwa kuongeza tija katika sekta hizo.


“Lazima tuangalie ubora wa mifugo tunayoiandaa, tunayoifuga, mbari za mifugo zenye ubora unaotakiwa, madume yaliyo bora, lakini pia tija kwa maana ya kuongeza uzalishaji likiwemo la uhimilishaji.” Amesema Bw. Nzunda  


Aidha, ameongeza kuwa katika kuhakikisha sekta za uzalishaji mali zinakuwa na tija ni muhimu kuimarisha huduma za mifugo kwa maana ya afya ya mifugo, kinga ya mifugo, udhibiti wa magonjwa na kuimarisha miundombinu muhimu ya huduma ya mifugo.


Pia, katibu mkuu huyo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kikao hicho cha ushirikiano juu ya Sekta ya Mifugo kati ya watendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni muhimu katika kutatua changamoto zilizopo Visiwani Zanzibar na Tanzania Bara ili kuwa na mwelekeo wa kuimarisha huduma za utafiti na ugani kwa mapana zaidi.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bw. Seif Shaban Mwinyi akizungumza katika kikao hicho amesema moja ya nyenzo ya kupata rasilimali watu iliyo bora ni lishe na hususan unywaji wa maziwa yatokanayo na mifugo, ambapo amefafanua kuwa bado unywaji wa maziwa uko chini ya asilimia 100 kwa kuwa mtu mzima kwa mwaka angalau anapaswa kunywa lita 200.


Ameongeza kuwa ili mtoto akue vizuri kiakili na afya kwa ujumla ni unywaji wa maziwa ambapo ametoa wito kwa wakazi wa Visiwani Zanzibar kuhakikisha wanakunywa maziwa kwa wingi ili kuondokana na udumavu na utapiamlo huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiendelea kuboresha mikakati mbalimbali ya kukuza Sekta ya Mifugo visiwani humo ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa maziwa yatokanayo na mifugo.


Katika kikao hicho kilichowakutanisha baadhi ya wataalamu wa Sekta ya Mifugo kutoka wizara pamoja na taasisi na vitengo vinavyoshughulika na sekta hiyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yamepitishwa maazimio kadhaa yakiwemo ya kuongeza zaidi ushirikiano kwa kufanya tafiti zenye tija na kushirikisha sekta binafsi ili kuwa na maono mapana zaidi ya kuongeza tija kwa taifa.


Kikao pia kimeazimia kutoa kipaumbele kwa wawekezaji wa ndani ya nchi kutoka Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar kuwekeza katika maeneo hayo katika ufugaji, kuanzisha viwanda vya Sekta ya Mifugo au mashamba ya malisho ili kuongeza tija na fursa nyingi zaidi za uwekezaji.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akifungua kikao Mjini Unguja Visiwani Zanzibar, kilichowakutanisha baadhi ya wataalamu (hawapo pichani) wa Sekta ya Mifugo wa wizara pamoja na taasisi na vitengo vinavyoshughulika na sekta hiyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo amesema sekta za uzalishaji mali ikiwemo mifugo ndizo zinazobeba uchumi wa nchi na kuwataka watendaji serikalini kufanya mabadiliko makubwa ya kifikra, kiutendaji na mifumo ya kiuendeshaji ili kukuza sekta za uzalishaji mali nchini. (04.11.2022)


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bw. Seif Shaban Mwinyi (kulia) akizungumza Mjini Unguja Visiwani Zanzibar, katika kikao kilichowakutanisha baadhi ya wataalamu (hawapo pichani) wa Sekta ya Mifugo wa wizara pamoja na taasisi na vitengo vinavyoshughulika na sekta hiyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo amesema unywaji wa maziwa yatokanayo na mifugo bado uko chini ya asilimia 100 kwa kuwa mtu mzima kwa mwaka angalau anapaswa kunywa lita 200. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Tixon Nzunda. (04.11.2022)


Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Bw. Venance Ntiyalundura akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio au yatokanayo na kikao ambacho kimefanyika Mjini Unguja Visiwani Zanzibar, kilichowakutanisha baadhi ya wataalamu (hawapo pichani) wa Sekta ya Mifugo wa wizara pamoja na taasisi na vitengo vinavyoshughulika na sekta hiyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (04.11.2022)


Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Tixon Nzunda (wa pili kutoka kushoto waliokaa), Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bw. Seif Shaban Mwinyi (kushoto kwake) na Naibu Katibu Mkuu wake Dkt. Omar Ali Ameir (wa kwanza kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Bw. Venance Ntiyalundura (wa kwanza kulia) wakiwa na baadhi ya wataalamu wa Sekta ya Mifugo wa wizara pamoja na taasisi na vitengo vinavyoshughulika na sekta hiyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kikao cha kuimarisha ushirikiano wa Sekta ya Mifugo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kilichofanyika Mjini Unguja. (04.11.2022)


Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Tixon Nzunda (wa pili kutoka kushoto waliokaa), Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bw. Seif Shaban Mwinyi (kushoto kwake) na Naibu Katibu Mkuu wake Dkt. Omar Ali Ameir (wa kwanza kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Bw. Venance Ntiyalundura (wa kwanza kulia) wakiwa na baadhi ya wataalamu wa Sekta ya Mifugo wa wizara pamoja na taasisi na vitengo vinavyoshughulika na sekta hiyo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kikao cha kuimarisha ushirikiano wa Sekta ya Mifugo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kilichofanyika Mjini Unguja. (04.11.2022)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni