Nav bar

Jumatano, 2 Novemba 2022

MRADI UHIFADHI WA KASA MBIONI KUTEKELEZWA

Na Mbaraka Kambona,


Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Taasisi ya SeaSense inayojishughulisha na uhifadhi wa samaki aina ya Kasa wapo mbioni kuandaa Mpango wa Kitaifa wa  kuimarisha ushirikiano wa Kitaifa, Kikanda na Kimataifa wa uhifadhi na usimamizi wa Kasa na Mazingira yake baharini.


Hayo yalifahamika wakati wa kikao baina ya  Mkurugenzi wa Uvuvi, Tanzania, Bw. Emmanuel Bulayi na  Mratibu wa Mradi huo unaotekelezwa na Taasisi ya SeaSense, Bw. Abdallah Ngaugula kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mtumba, jijini Dodoma Oktoba 26, 2022.

 

Akiongea katika kikao hicho ambacho kilishirikisha Wataalamu mbalimbali kutoka Sekta ya Uvuvi, Bw. Bulayi alisema kuwa mradi huo ni mzuri na ni muhimu kushirikisha wananchi tangu hatua za awali ili kuwajengea uwezo wa uhifadhi  wa Kasa ili mradi huo ufanikiwe na kuwa endelevu.


Alisema wao kama Serikali watakuwa bega kwa bega na taasisi hiyo kuhakikisha malengo ya mradi huo yanatimia huku akisisitiza ni muhimu kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo Wataalamu wa Wizara wakashirikishwa ili kuwa na uelewa wa pamoja wakati wote wa utekelezaji wake.


Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi huo, Bw. Abdallah Ngaugula alisema kuwa kimsingi mradi huo ni wa Serikali na wao ni wawezeshaji tu.


Alisema wanaishukuru Serikali kwa kuukubali mradi huo, na wanaomba Wataalamu kutoka Sekta ya uvuvi kutoa ushirikiana wa kutosha ili  kufanikisha malengo ya mradi huo.


Mradi huo wa uhifadhi na usimamizi wa Kasa na Mazingira yake baharini unasimamiwa na Taasisi ya SeaSense chini ya ufadhili Shirika la Kimataifa la Misaada la Kimarekani (USAID).

Mkurugenzi wa Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Mratibu wa  Mradi wa uhifadhi na usimamizi wa Kasa na Mazingira yake baharini, Bw. Abdallah Ngaugula pamoja na Wataalamu kutoka Sekta ya uvuvi muda mfupi baada ya kumaliza kikao chao  kilichofanyika kwenye Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mtumba, jijini Dodoma Oktoba 26, 2022.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa pili kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mratibu wa  Mradi wa uhifadhi na usimamizi wa Kasa na Mazingira yake baharini, Bw. Abdallah Ngaugula(wa pili kutoka kulia). Mratibu huyo alifika  Ofisini kwa Katibu Mkuu huyo kwa lengo la kujitambulisha na kueleza majukumu ya taasisi ya SeaSense. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mtumba, jijini Dodoma Oktoba 26, 2022.

Mratibu wa  Mradi wa uhifadhi na usimamizi wa Kasa na Mazingira yake baharini, Bw. Abdallah Ngaugula akiwasilisha mada kuhusu mradi huo katika kikao kilichofanyika kwenye Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mtumba, jijini Dodoma Oktoba 26, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni