Nav bar

Jumatano, 19 Oktoba 2022

UNYWAJI MAZIWA SHULENI WAFIKIA SHULE 68.

◼️ FAO na UNICEF waongeza nguvu. 


Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imebainisha kuwa mpango wa unywaji maziwa shuleni iliouanzisha tangu mwaka 2007 sasa umezifikia shule 68.


Hayo yamesemwa leo (13.10.2022) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki katika hotuba yake aliyoisoma kwenye sehemu ya maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.


"Kiwango hicho kinaonekana kuwa ni kidogo kwa sababu mpango huu unawahusisha zaidi wazazi kwenye kuchangia ili watoto wapate huduma hiyo wakiwa shuleni na bahati mbaya muitikio wa kampeni hiyo kwenye baadhi ya maeneo upo chini sana" Ameongeza Mhe. Ndaki.


Mhe. Ndaki amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya zinaonesha kwa nchi nzima jumla ya watoto milioni 3 wana changamoto ya udumavu jambo ambalo ameweka wazi halina taswira nzuri kwa hatma ya watoto hao mbeleni.


"Wataalam wa afya wanasema mtu akinywa maziwa anapata aina zote za viini lishe kwenye chakula lakini bahati mbaya matumizi ya maziwa kwa hapa kwetu bado yapo chini na hivyo kukosa viini lishe hivyo ". 


Mhe. Ndaki amesema kuwa licha ya mikoa ya kanda ya Ziwa kuongoza kwa wingi wa mifugo bado takwimu zinaonesha kiwango unywaji wa maziwa kwenye kaya zilizopo mkoani humo kipo chini huku maziwa mengi yakipelekwa maeneo ya mjini kwa ajili ya kuuza.


Akielezea mikakati ya kuongeza idadi ya shule zitakazonufaika na mpango wa unywaji maziwa shuleni, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya amesema kuwa Bodi yake kupitia msaada wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNICEF na FAO imepata fedha ambazo zitaziwezesha shule nyingi zaidi kufikiwa na mpango huo.


"Tunatambua kuwa watumiaji namba moja wa bidhaa yetu ya Maziwa ni watoto ambao wengi ni wanafunzi wa shule za msingi hivyo tumejipanga kuhakikisha tunawafikia wanafunzi wengi zaidi na hili limewezekana kupitia kazi kubwa iliyofanywa na Serikali Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwatafuta wadau hawa wa Maendeleo" Amesema Dkt. Msalya.


Licha ya changamoto ya kiwango duni cha matumizi ya maziwa kwa wananchi, Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira yatakayosaidia kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo ikiwa ni pamoja na kuondoa kodi kwenye vifaa vya kusafirishia na kufungasha bidhaa hiyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akimpa maziwa mmoja wa wanafunzi wa shule za Msingi zilizopo Mkoani Simiyu tukio lililofanyika leo (13.10.2022) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kitaifa Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea katika Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani humo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akipokea maelezo yanayohusu mashine maalum ya kutotoleshea vifaranga vya kuku kutoka kwa mmoja wa wajasiriamali waliopo Mkoani Simiyu Bw. Hery Ulamba muda mfupi leo (13.10.2022) baada ya kuwasili kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani humo yanakofanyika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akipokea maelezo ya mashine ya kukatia malisho ya mifugo kutoka kwa Meneja Msaidizi wa kampuni ya pembejeo za kilimo ya "Poly Machine" Bw. Samwel Laizer mfupi leo (13.10.2022) baada ya kuwasili kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu yanakofanyika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni