Nav bar

Jumatano, 19 Oktoba 2022

SERIKALI YAWAHAKIKISHIA USHIRIKIANO WAWEKEZAJI SEKTA YA MIFUGO

Na Mbaraka Kambona,


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inaunga mkono uwekezaji unaofanywa katika sekta ya mifugo hapa nchini hivyo wataendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji hao ili kuhakikisha malengo ya uwekezaji wao yanafikiwa kama walivyotarajia.


Nzunda alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake aliyoifanya Mkoani Pwani na Dar es Salaam Oktoba 12, 2022.


Akiwa katika ziara hiyo ambapo alitembelea Kiwanda cha kuzalisha chanjo za mifugo cha HESTER, Kiwanda cha kuchakata nyama cha TANCHOICE na kampuni ya kuzalisha Hereni za Kielekroniki za mifugo, kwa nyakati tofauti alisema wanawashukuru wawekezaji hao kwa sababu uwekezaji wao unaenda sambamba na mipango ya Serikali ya kukuza na kuimarisha Sekta ya mifugo nchini.


"Tunawashukuru kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali hususan katika kuimarisha mpango wa mabadiriko wa sekta ya mifugo na tutaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili Sekta hii iweze kukua zaidi",alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazosababisha kukwamisha uwekezaji ikiwemo mlolongo wa tozo ili kuendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini.


Naye, Mtendaji Mkuu, Kiwanda cha Kuzalisha chanjo za mifugo cha HESTER, Dkt. Furaha Mramba alisema anamshukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji huku akiongeza kuwa kiwanda hicho kitaleta faida kubwa nchini ikiwemo fedha za kigeni kupitia uuzaji wa chanjo za mifugo nje ya nchi.


Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha TANCHOICE, Bw. Rashid Abdillahi aliiomba Serikali iangalia utaratibu wa usafirishaji wa mifugo nchini hususan katika mizani kwa sababu ilivyo sasa unasababisha gharama za uendeshaji wa biashara ya nyama kuwa kubwa.


Aidha, katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Nzunda alieleza pia namna ambavyo Serikali imejipanga kuanzia mwaka huu wa fedha kuleta mabadiriko katika sekta ya mifugo ikiwemo kuboresha shughuli za ugani, kujenga majosho, minada na kuifufua NARCO pamoja na mashamba mengine ya Serikali.

Mkurugenzi Mkuu, Kiwanda cha kuchakata nyama cha TANCHOICE, Bw. Rashid Abdillahi (kushoto) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (kulia) alipotembelea kiwanda hicho kilichopo mkoani Pwani Oktoba 12, 2022.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda(kushoto) akikagua shughuli za utengenezaji wa Hereni za Kielekroniki za mifugo katika Kiwanda cha S&J kilichopo jijini Dar es Salaam Oktoba 12, 2022.

Mtendaji Mkuu, Kiwanda cha Kuzalisha chanjo za mifugo cha HESTER, Dkt. Furaha Mramba(kulia) akitoa taarifa fupi kuhusu Kiwanda hicho kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda(kushoto) alipotembelea Kiwanda hicho kilichopo Mkoani Pwani Oktoba 12, 2022.

Mtendaji Mkuu, Kiwanda cha kutengeneza chanjo cha HESTER, Dkt. Furaha Mramba (kulia) akimuonesha Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Bw. Tixon Nzunda sehemu ya mitambo ya kuzalisha chanjo alipotembelea kiwanda hicho kilichopo mkoani Pwani Oktoba 12, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni