Nav bar

Jumatano, 19 Oktoba 2022

MIFUGO NA UVUVI WAIBUKA VINARA SIKU YA CHAKULA DUNIANI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeibuka kinara kwenye Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.


Wizara imetangazwa kushika nafasi hiyo jana (16.10.2022) ambapo imeshinda kwenye kipengele cha Taasisi zilizoonesha ubunifu wa bidhaa na huduma kwa upande wa Wizara ambapo ilikuwa ikishindana na Wizara ya Kilimo.


Akizungumzia yale yanayofanywa na Wizara hiyo muda mfupi kabla ya kukabidhiwa Tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa amesema kuwa uwepo wa Maonesho hayo ni fursa kubwa kwa Wizara na Taasisi zake kuonesha kwa vitendo mikakati mbalimbali waliyonayo ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya Mifugo na Uvuvi.


"Kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu inatupa ujumbe wa kuhakikisha tunazalisha chakula cha kutosha huku tukilinda mazingira na chakula hicho kiwe na virutubisho stahili kwa ajili ya kuyafaa makundi yote kuanzia ngazi ya kaya na Taifa kwa ujumla" Ameongeza Dkt. Mwilawa.


Dkt. Mwilawa amesisitiza kuwa Wizara inaendelea kufanya jitihada za kuongeza matumizi ya mazao ya mifugo na Uvuvi ili kuendana na kiwango kinachopendekezwa na Shirika la Chakula na kilimo Duniani (FAO).


"Tunatambua maelekezo ya FAO ni kila Mtanzania kunywa maziwa kiasi cha lita 200 kwa mwaka lakini kwa sasa anakunywa lita 62 tu na upande wa nyama kwa sasa kila mtu anakula kilo 15 tu kwa mwaka ikilinganishwa na kilo 60 zinazopendekezwa na Shirika hilo na hata kwa upande wa ulaji wa samaki bado kiwango kipo chini kwani mtu mmoja anapaswa kula kilo 20.5 tofauti na kilo 8.5 anazokula sasa" Ameongeza Dkt. Mwilawa.


Kwa upande wa mikakati ambayo Wizara imeiweka ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa lishe ya mifugo nchini, Dkt. Mwilawa amesema kuwa Wizara imeboresha miundombinu ya upatikanaji wa maji kwa muda wote ili kuondokana na changamoto ya athari za ukame.


"Lakini pia ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nyama bora wakati wote tunaendelea kuboresha afya za mifugo kwa kuwa na majosho bora na kusambaza chanjo za mifugo hiyo huku pia tukiendelea kuboresha huduma za ugani ambapo katika mwaka huu wa fedha tunatarajia kuongeza pikipiki nyingine 1200 ambazo zitapelekwa katika ngazi za kata na vijiji" Ameongeza Dkt. Mwilawa.


Kwa upande wa Sekta ya Uvuvi, Dkt. Mwilawa amesema kuwa Wizara inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza kwenye sekta hiyo hasa kwa upande wa ukuzaji viumbe maji ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa samaki nchini.


"Wizara imedhamiria kuzalisha jumla ya vifaranga vya samaki milioni 30 ili kusambaza kwa wakuzaji viumbe maji waliodhamiria kuwekeza kwenye ufugaji wa samaki" Amesema Dkt. Mwilawa.


Dkt. Mwilawa amehitimisha kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikihamasisha matumizi ya mazao ya Mifugo na Uvuvi kupitia Maonesho mbalimbali yakiwemo Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani, Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane), Siku ya Nyama choma na Siku ya Yai.


Maadhimisho ya Siku ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanatarajiwa kufanyika Mkoani Simiyu kwa miaka mingine miwili ijayo ambapo kuanzia Mwakani yatafanyika katika Viwanja vya Nyakabindi.

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (kulia) akimkabidhi zawadi ya kikombe Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa mara baada ya Wizara yake kuibuka kinara kwenye Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya chakula Duniani mwaka huu kipengele cha Taasisi zilizoonesha ubunifu wa bidhaa na huduma kwa upande wa Wizara tukio lililofanyika jana (16.10.2022) kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.


Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa (kushoto) akimuelezea Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (kulia) aina ya malisho ya Mifugo yaliyopo kwenye banda la Wizara hiyo mara baada ya Mhe. Bashe kufika kwenye banda hilo jana (16.10.2022) ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuhitimisha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (kulia) akishauri namna ya kufanya Uhimilishaji wa kuku aina ya "kuchi" na kuku chotara ili kuongeza uzalishaji wa nyama na mayai mara baada ya kufika kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi jana (16.10.2022) ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuhitimisha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (kushoto) akielezea namna chanjo za Mifugo zinazozalishwa hapa nchini zinavyosaidia kutokomeza magonjwa ya Mifugo mara baada ya kufika kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi jana (16.10.2022) ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuhitimisha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu. Kulia ni Daktari Utafiti wa Mifugo Mwandamizi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kanda ya Ziwa Mashariki Dkt. Raphael Paulo.

Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Kitengo cha Uthibiti Ubora na Usalama wa Mazao ya Uvuvi kanda ya Ziwa Victoria Bw. Prosper Mremi (katikati) akimuelezea Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (kulia) uchakataji wa samaki aina ya Sangara mara baada ya Mhe. Bashe kufika kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi jana (16.10.2022) ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuhitimisha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu. Kushoto ni Afisa Uvuvi Mkuu Msaidizi Bi. Amina Kiaratu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni