Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah leo (22.09.2022) amelikabidhi Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) nyaraka za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya shirika hilo ikiwa ili kuipa fursa Bodi ya Uendeshaji ya Shirika hilo kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi tukio lililofanyika kwenye Ofisi ndogo za Wizara hiyo zilizopo eneo la Temeke Vetenari jijini Dar-es-Salaam.
Katika taarifa yake kabla ya kukabidhi nyaraka hizo Dkt. Tamatamah ametoa rai kwa Bodi hiyo kuhakikisha Shirika hilo linajiendesha kwa kushirikiana na sekta binafsi badala ya kutegemea Serikali ambapo amewataka kuanza kutafuta Taasisi za sekta binafsi ambazo zitakuwa tayari kushirikiana na Serikali kuliendesha Shirika hilo.
“Ni Imani ya Serikali kuwa Uendeshwaji wa Shirika hili hautafanywa na Serikali pekee hivyo ni lazima mshirikiane kikamilifu na sekta binafsi na kuifanya kuwa mshirika wa kweli katika mipango yenu ya uzalishaji na kutoa huduma” Amesisitiza Dkt. Tamatamah.
Dkt. Tamatamah ameongeza kuwa uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo ambao ulifanywa na Mhe. Rais na ule wa wajumbe ambao ulifanywa na Mhe. Waziri wa Mifugo na Uvuvi ni ushahidi tosha kwamba Serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inaendelea kukua kwa kasi na kutoa mchango wa kutosha kwenye pato la Taifa hivyo aliwataka kila mmoja kwa nafasi yake kuendelea kuongeza ufanisi kwenye shirika hilo.
Miongoni mwa nyaraka alizokabidhi Dkt. Tamatamah kwa Bodi hiyo ni pamoja na Menejimenti ya Shirika hilo yenye watumishi 11, majengo ya Shirika yaliyopo mkoa wa Dar-es-Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Mwanza na Kigoma.
Nyaraka nyingine ni pamoja na zile zinazojumuisha Muundo wa Shirika hilo wenye Vitengo 10 na ofisi moja, bajeti ya Shirika iliyoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ya kiasi cha shilingi milioni 407, rasimu ya nyaraka muhimu za Shirika ambazo zinapaswa kukamilishwa ili kuliwezesha Shirika kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na Rasimu ya kanuni za fedha, rasimu ya kanuni ya masuala ya watumishi, rasimu ya miundo ya maendeleo ya utumishi, rasimu ya orodha ya kazi, rasimu ya maelezo ya kazi ya watumishi, mpango mkakati wa miaka 5 wa Taasisi na mpango wa biashara wa shirika.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa nyaraka hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo Prof. Yunus Mgaya mbali na kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua kushika wadhifa huo, amemshukuru Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa kuteua wajumbe wa bodi hiyo ambapo amemuomba Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah kuendelea kuwapa ushirikiano pale watakapohitaji msaada wake.
Kukabidhiwa kwa nyaraka za Utekelezaji wa Bodi ya Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) ni hatua ambayo itaipa fursa Bodi hiyo kuanza kufanya shughuli mbalimbali zinazolenga kulifufua Shirika hilo linalotarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kukuza sekta ya Uvuvi nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akimkabidhi nyaraka za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO), Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo Prof. Yunus Mgaya wakati wa hafla fupi ya zoezi hilo iliyofanyika leo (22.09.2022) kwenye Ofisi ndogo za Wizara hiyo zilizopo eneo la Veternari, Temeke jijini Dar-es-salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah (wa pili kutoka kushoto mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi, waalikwa na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) muda mfupi baada ya kuikabidhi bodi hiyo nyaraka za utekelezaji wa majukumu zoezi lililofanyika leo (22.09.2022) kwenye Ofisi ndogo za Wizara hiyo zilizopo eneo la Veternari, Temeke jijini Dar-es-salaam.Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Uvuvi nchini (TAFICO) Bi. Ester Mulyila akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo wakati wa kikao cha kwanza cha Bodi ya Shirika hilo kilichofanyika leo (22.09.2022) kwenye Ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo eneo la Vetenari, Temeke jijini Dar-es-salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni