Watanzania wametakiwa
kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambao takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya
watu 60,000 hufariki duniani kila mwaka huku wastani wa matukio ya majeraha kwa
binadamu yanayotokana na kuumwa na mbwa ni 3,387 kila mwaka.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule wakati wa maadhimisho ya kilele cha
siku ya kichaa cha mbwa duniani yaliyofanyika kwenye eneo la mnadani kata ya
Mpunguzi Septemba 28,2022 jijini Dodoma.
Senyamule amesema kuwa kwa
mujibu wa repoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2017, ugonjwa wa kichaa
cha mbwa husababisha wastani wa vifo vya binadamu 1,500 kila mwaka nchini
Tanzania. Takwimu zaidi zinaonesha kuwa watoto chini ya umri wa miaka 15 ndiyo
hupatwa zaidi na madhara haya kwa kuwa na ukaribu na urafiki na mbwa.
Aidha, amesema kwa hapa
Tanzania, kila mwaka kuna wastani wa matukio 2,030 ya mbwa wanaodhaniwa kuwa na
kichaa. ‘’Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Afya za Wanyama Duniani
(WOAH) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) kwa pamoja yamekubaliana
kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa ifikapo 2030.
“Njia kuu ya kufikia
malengo haya ya dunia ni pamoja na kutoa chanjo kwa mbwa wote kila mwaka,
kupunguza idadi ya mbwa, kuzingatia ufugaji bora wa mbwa ikiwa ni pamoja na
kufungia mbwa wasizurure mitaani,’’ alisema Senyamule
Mbali na hilo, amesema kuwa
Tanzania ina mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa wa
mwaka 2019. Lengo lake ni kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha mbwa na hatimaye
kuutokomeza kabisa ifikapo 2030. Pia, kuna Mpango Mkakati wa Afya Moja
(2015-2020) unaotoa wajibu wa kila mmoja katika kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha
mbwa kwa njia ya chanjo.
Aidha, Senyamule amepongeza
jitihada zilizochukuliwa na Wizara uamuzi wa kidhibiti kichaa cha mbwa kwa
mfumo wa kuendesha kampeni kwani njia hii inasaidia kufikisha ujumbe kwa
watanzania wengi zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya
Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga amesema
kuwa kupitia kampeni hii watahakikisha mbwa wote wanachanjwa ili kuwakinga na
ugonjwa huo. Hivyo ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha mbwa wao wanachanjwa
katika kipindi hiki cha kampeni.
Prof. Nonga amesema kuwa hata baada ya kampeni
hii kumalizika, uchanjaji wa mbwa utaendelea kufanyika kwa mwaka mzima.
Perez Rumolwa ambaye ni
mfugaji wa mbwa alisema kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa huweza kusababisha kifo
ikiwa mtu hatowahishwa hospitali.
"Ndugu yangu mwenyewe,
aling’atwa na mbwa ikasababisha kifo chake.’’ alisema
Hapa nchini, kuna takribani
mbwa milioni 4.5 na paka milioni 2 wanaofugwa kwa malengo mbalimbali ikiwa ni
pamoja na ulinzi, kusaidia kuchunga mifugo na uwindaji. Maadhimisho ya kilele
cha wiki ya Kichaa cha Mbwa Duniani yanaongozwa na Kauli Mbiu inayosema “Kichaa
cha Mbwa; Afya Moja, Vifo Sifuri”
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.
Rosemary Senyamule akiongea na wafugaji wa mbwa wa kata ya Mpunguzi (hawapo
pichani) wakati wa maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani na kuwahimiza
kuchanja mbwa na paka wao Ili kupunguza maambukizi ya kichaa cha mbwa na kupunguza
vifo vya mbwa na wananchi kwa ujumla, Septemba 28,2022 Mkoa Dodoma.
Mkurugenzi wa Huduma za
Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga akitoa elimu ya
chanjo na madhara ya kutochanja mbwa kwa wafugaji wa mbwa Mkoani Dodoma (hawapo
pichani) wakati wa maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani
kilichofanyika kwenye kata ya Mpunguzi Septemba 28,2022.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Mhe. Rosemary Senyamule akikabidhi kadi ya chanjo ya mbwa kwa Mfugaji wa mbwa
kata ya Mpunguzi, Bw. Perez Rumolwa ambaye amechanja mbwa wake kwenye
maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani yaliyofanyika kitaifa Mkoani
Dodoma, Septemba 28, 2022
Mmoja wa mbwa akipatiwa
chanjo wakati wa maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani kwenye kata ya
Mpunguzi Septemba 28,2022 Mkoani Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni