Nav bar

Alhamisi, 22 Septemba 2022

MAJALIWA AZINDUA MPANGO KABAMBE WA SEKTA YA UVUVI

◼️ Ndaki abainisha vigezo vilivyotumika kuuandaa 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.  Kassim Majaliwa amesema kuwa  utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi utasaidia kukuza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka kutoka asilimia 1.8 ya sasa.


Mhe. Majaliwa amesema hayo leo (20.09. 2022) wakati wa uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi uliofanyika kwenye ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam.


 “Tutaendelea kupokea mapendekezo yenu ili tuweze kuboresha sekta hii, ubunifu wenu ni muhimu, wote tunataka tuzungumze lugha moja” Ameongeza Mhe. Majaliwa


Mhe. Majaliwa amesema kuwa mpango huo ambao utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 15 kuanzia 2021/2022 hadi 2036/2037 una umuhimu mkubwa katika ukuaji wa sekta ya uvuvi na utekelezaji wa sera ya Uchumi wa Buluu.


Aidha Mhe. Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau wote wa sekta ya uvuvi kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ina nia ya dhati ya kuhakikisha kila mmoja ananufaika na rasilimali zinazotokana na sekta hiyo.


“Uwepo wa mipango mbalimbali katika sekta ya uvuvi utawezesha rasilimali hiyo kulindwa, kusimamiwa, kuendelezwa, kuhifadhiwa na kutumiwa kwa njia endelevu na hatimaye kuchangia kikamilifu katika kutoa ajira, kipato, chakula na lishe kwa jamii ya Watanzania kwa ujumla” Amesisitiza Mhe. Majaliwa.


Akisoma taarifa yake kabla ya kumkaribisha Mhe. Waziri Mkuu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa maandalizi ya mpango huo yamezingatia Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015, maelekezo ya ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 na mipango,mikakati na miongozo ya kitaifa, kikanda na kimataifa.


“Aidha mpango huu umezingatia mchango wa sekta ya Uvuvi katika kuiwezesha nchi kikamilifu fursa zilizopo kwenye uchumi wa Buluu na changamoto zilizoibuliwa na wadau katika maeneo mbalimbali yaliyofikiwa wakati wa kuandaa Mpango huu” Ameongeza Mhe. Ndaki.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa historia inaonesha utekelezaji wa shughuli za uvuvi hapa nchini umekuwa ukifanyika kwa kuzingatia mipango kabambe ya uvuvi na wa mwisho kabla ya ule uliozinduliwa leo ni mpango kabambe wa mwaka 2002-2015.


“Kumalizika kwa kipindi cha utekelezaji wa Mpango huo kulipelekea Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanya mapitio ya mpango huo na kuandaa mpango kabambe mpya utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 15 (2021/2022-2036/37)” Amesema Dkt. Tamatamah.


Mpango huo uliozinduliwa leo unatarajiwa kuwa chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya uvuvi kutoka tani 473,592 zilizozalishwa kupitia mpango uliomalizika hadi hadi kufikia tani 639,092 ambazo zitakuwa ni sawa na ongezeko la asilimia 35.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mpango kabambe wa miaka 15 wa sekta ya Uvuvi uliofanyika leo (20.09.2022) kwenye Ukumbi wa Maktaba-Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, Kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya  Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (kushoto) akizungumza na wadau wa sekta ya Uvuvi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango kabambe wa miaka 15 wa sekta hiyo iliyofanyika leo (20.09.2022) kwenye Ukumbi wa Maktaba-Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji Dkt. Christine Ishengoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah, Mwakilishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-salaam na Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) muda mfupi baada ya kuwasili kwenye Ukumbi wa Maktaba- Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam ambako amezindua Mpango kabambe wa miaka 15 wa sekta ya Uvuvi leo (20.09.2022).

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (mwenye tai nyekundu mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi na watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi muda mfupi baada ya kuzindua Mpango kabambe wa miaka 15 wa sekta hiyo hafla iliyofanyika leo (20.09.2022) kwenye Ukumbi wa Maktaba-Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni