Na Mbaraka Kambona, Mwanza
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahimiza vijana wa Kanda ya Ziwa Viktoria kufuga samaki ili kujiongezea kipato na kuongeza fursa za ajira nchini.
Waziri Ulega alitoa wito huo kwa nyakati tofauti akiwa ziarani katika Wilaya za Ukerewe na Ilemela zilizopo mkoani Mwanza Agosti 20, 2022.
Alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kutumia fursa za uchumi wa buluu zilizopo ndani ya Ziwa Viktoria kuwawezesha vijana kufuga samaki kwa kutumia vizimba na kuuza samaki hao ndani na nje ya nchi ili kujiongezea kipato.
"Rais Samia ametoa bilioni 20 kwa ajili ya kuwezesha vijana kufuga samaki katika vizimba, hivyo ni wakati sasa wa kujipanga ili pesa hizo zitakapokuja tuweze kuzitumia vizuri kufanya uzalishaji wa samaki kwa wingi ili tuweze kuuza na kupata kipato", alisema
Aliongeza kwa kusema kuwa samaki aina ya sato wanahitajika sana ndani na nje ya nchi, uhitaji ni mkubwa hivyo vijana wajipange vizuri ili waweze kutumia fursa hiyo kujiinua kimaisha.
Kwa upande wa vijana wanaojishughulisha na ufugaji wa samaki, Bw. Bahati Paul kutoka Ilemela na Peter Emmanuel kutoka Ukerewe kwa nyakati tofauti walisema kuwa mpango huo wa Serikali wa kuwawezesha vijana utasaidia sana vijana kujiajiri na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.
Aidha, vijana hao waliiomba Serikali kutatua changamoto ya chakula cha samaki kwani imekuwa ikichangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa samaki nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega alisema mwaka huu pia Serikali itawakopesha wavuvi nchini kote boti za kisasa zaidi ya 150 ili wavuvi waweze kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wa samaki.
Aliongeza kwa kusema kuwa boti hizo zitafungamanishwa na teknolojia za kisasa zitakazomsaidia mvuvi kurahisisha shughuli za uvuvi.
Waziri Ulega aliendelea kufafanua kuwa mkopo huo wa masharti nafuu unalenga kuwawezesha wavuvi kuboresha uvuvi wao kwa sababu nia ya Mhe. Rais Samia ni kuwatoa wavuvi katika uvuvi wa kuwinda na kufanya uvuvi wa kisasa wa uhakika.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia)
akikagua moja ya kizimba katika miradi ya ufugaji wa samaki kwa kutumia
vizimba inayofanywa na Vikundi vya vijana vya Chapakazi na Catfish
alipotembelea miradi hiyo Wilayani Ilemela, Mkoani Mwanza Agosti 20, 2022.
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akipatiwa maelezo na mmoja wa vijana
wanaofanya miradi ya ufugaji wa samaki alipotembelea miradi hiyo Wilayani
Ilemela, Mkoani Mwanza Agosti 20, 2022.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni