Nav bar

Jumamosi, 11 Juni 2022

NDAKI AANIKA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amebainisha mikakati ambayo Wizara yake imeanza kuitekeleza ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi.


Mhe. Ndaki amesema hayo leo (06.06.2022) wakati akisoma taarifa ya Wizara hiyo kwenye mkutano wa timu ya wataalam wa uchambuzi wa Sera za Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinazolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika jijini Dodoma ambapo amesema kuwa Wizara yake imeanza kuhamasisha ufugaji wa kisasa ambao utawafanya wafugaji kupata tija ya kutosha kwa kutumia  maeneo madogo kutekeleza shughuli zao.


“Tunajua fedha tuliyopewa sio nyingi sana hivyo hatuwezi kukutana na wafugaji wote kwa wakati mmoja lakini tutaenda kukutana na wafugaji moja kwa moja na kuwaelekeza namna bora ya kufanya ufugaji wa kisasa ili waweze kutumia maeneo madogo waliyonayo kupata tija ya ufugaji wanaoufanya” Amesema Mhe. Ndaki.


Mhe. Ndaki ameongeza mkakati mwingine wanaoutarajia kuutekeleza ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi  ni  kuanzisha mashamba darasa ya malisho ya mifugo kwa wafugaji ambapo kwa kuanzia takribani wafugaji 1000 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo.


“Tuwafuata wafugaji wenye mifugo mingi na wanaotamani kuboresha namna ya ufugaji wao, watatuonesha mashamba yao kisha tutapanda malisho ya mifugo bure kabisa ambayo yatawanufaisha wao wenyewe na tunaamini faida watakayoipata itawawezesha kuimarisha zaidi uzalishaji wa malisho hayo” Ameongeza Mhe. Ndaki.


Aidha Mhe. Ndaki amesema kuwa msimamo wa Wizara yake kwa hivi sasa ni kuwahamasisha wafugaji kumiliki maeneo yao ya malisho jambo ambalo anaamini litaondoa migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi na  kupunguza uharibifu wa mazingira.


“Lakini kwa upande wa maji tumeamua kutengeneza malambo badala ya kuchimba visima kwa sababu tumegundua visima hivi hukauka baada ya muda flani hivyo ili kuepukana na ukosefu wa maji ya mifugo yetu kwa muda mrefu tumeona malambo ni sahihi zaidi kuliko hivyo visima” Amesema Mhe. Ndaki.


Akizungumzia kwa upande wa sekta ya Uvuvi, Mhe. Ndaki amesema kuwa Wizara yake inaendelea na kampeni ya kuwahamsisha wavuvi wote kuachana na uvuvi haramu ambao unalenga kupatikana kwa samaki wa muda mfupi bila kujali hatima ya siku inayofuata.


“Mtu anaenda kuvua samaki wa leo tu, kesho itajijua yenyewe na mimi nasema kesho haitajijua yenyewe bali itashughulika na watoto wetu” Amehitimisha Mhe. Ndaki.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akifafanua mikakati ya Wizara yake katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwenye mkutano wa wachambuzi wa sera za Kilimo, Mifugo na Uvuvi uliofanyika leo (06.06.2022) jijini Dodoma.


Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (maji baridi), Dkt. Iman Kapinga (kushoto) na Afisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Didas Mtambalike wakiandika maelekezo yanayotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) kwenye mkutano wa wachambuzi wa sera za Kilimo, Mifugo na Uvuvi uliofanyika leo (06.06.2022) jijini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni