Na. Edward Kondela
Halmashauri za wilaya kote nchini ambazo zimekuwa hazitoi chanjo za mifugo, zimeagizwa kuanza kutoa chanjo za mifugo mara moja kuanzia Mwezi Julai mwaka huu na kutakiwa kutumia chanjo zinazozalishwa hapa nchini ili kudhibiti magonjwa ya mifugo na kukuza soko la chanjo hizo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametoa agizo hilo (11.04.2022) katika Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma, wakati akizindua chanjo ya kudhibiti ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo kitaifa inayozalishwa na kiwanda cha Hester Biosciences Africa Limited kilichopo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani na kubainisha kuwa, kuanzia Mwezi Julai atakuwa akipokea taarifa ya kila halmashauri namna inavyotekeleza zoezi la utoaji chanjo za mifugo.
Waziri Ndaki amewataka maafisa mifugo katika halmashauri hizo kuhakikisha wanatumia chanjo zinazozalishwa ndani ya nchi zikiwemo za kutoka Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), inayomilikiwa na serikali pamoja na chanjo zinazozalishwa na viwanda vinavyomilikiwa na sekta binafsi.
“Halmashauri ambazo hazitoi chanjo kwenye mifugo yao, kuanzia Mwezi Julai mwaka huu, mifugo yote ianze kuchanjwa na mimi nitaanza kupokea taarifa ya kila mwezi ya uchanjaji wa mifugo yetu, ili tujue baada ya mwaka mmoja mifugo yetu yote itakuwa imechanjwa? Na pia chanjo zitakazotumika ziwe zinazozalishwa hapa nchini na hatuna sababu ya kuagiza chanjo kutoka nje ya nchi.” Amesema Mhe. Ndaki
Katika uzinduzi huo wa chanjo kitaifa dhidi ya ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo, Waziri Ndaki amesema ni muhimu kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwani husaidia bidhaa hizo kuwa na soko la uhakika na hivyo kukuza pia ajira na kwamba chanjo za mifugo zinazozalishwa nchini, zinatengenezwa katika mazingira rafiki hivyo ni rahisi kutumiwa na wafugaji.
Aidha, amekishukuru kiwanda cha Hester Biosciences Africa Limited kwa msaada wa chanjo 700,000 zenye thamani ya Shilingi Milioni 245 walioipatia wizara kama mchango wao kwa jamii na kutoa wito kwa wadau wengine katika Sekta ya Mifugo kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto zilizopo katika sekta hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Hester Biosciences Africa Limited Dkt. Furaha Mramba amesema kiwanda hicho kitazalisha aina 37 za chanjo za mifugo ili kuhakikisha magonjwa yote ya mifugo yanakuwa na chanjo za kuyadhibiti ukiwemo ugonjwa wa homa ya nguruwe ambao wataanza kuufanyia utafiti wa kisayansi.
Dkt. Mramba amesema kiwanda kinatarajia kuzalisha dozi zisizopungua bilioni 1.5 kwa mwaka pale kitakapokuwa kinazalisha chanjo zote zilizokusudiwa na matarajio ni kuuza asilimia 20 ya chanjo hizo ndani ya nchi na asilimia 80 zinategemewa kuuzwa katika nchi jirani za Afrika Mashariki na nyingine kwenye nchi za Afrika.
Ameongeza kuwa katika uzinduzi wa chanjo kitaifa dhidi ya ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo katika Wilaya ya Kongwa, Mkoani Dodoma, chanjo hiyo itapatikana kote nchini ambapo katika uzinduzi huo Wilaya ya Kongwa imepatiwa bure dozi za chanjo hiyo ambapo wafugaji hawatagharamia kiasi chochote cha fedha ambapo katika wilaya zingine bei elekezi ya chanjo hiyo ni Shilingi 350 hadi 400 kwa mbuzi na kondoo.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amesema kumekuwepo na changamoto za uwepo wa magonjwa mbalimbali ya mifugo, ambapo magonjwa mengi yanadhibitiwa kwa njia ya chanjo ukiwemo ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo ambapo lengo ni kuutokomeza kabisa ugonjwa huo.
Prof. Nonga ameongeza kuwa chanjo ni njia nafuu katika kudhibiti magonjwa ya wanyama na kwamba tiba ni bei ghali endapo mnyama akiugua kwa kuwa wafugaji wamekuwa wakiingia gharama kubwa kutibu mnyama na kusisitiza matumizi ya chanjo ili kudhibti magonjwa ya wanyama kwa kuwa ni njia isiyokuwa na gharama kubwa.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi walioshiriki uzinduzi wa chanjo kitaifa dhidi ya ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo, Mbunge wa Jimbo la Kongwa Mhe. Job Ndugai, ameupongeza uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na kiwanda cha Hester Biosciences Africa Limited kwa kuwezesha kupatikana kwa chanjo ya ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo kwa kuwa ugonjwa huo umekuwa ukisumbua sana wafugaji na wengine kukata tamaa akiwemo yeye mwenyewe katika ufugaji wa mbuzi na kondoo.
Amekiomba kiwanda hicho kwa kushirikiana na serikali kuendelea kuzalisha chanjo nyingi zaidi dhidi ya magonjwa ya mifugo ili wafugaji waweze kufuga kwa tija na kupunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa ambayo yamekuwa yakiwasababishia hasara.
Ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo ni moja ya magonjwa yaliyomo katika mkakati wa kutokomezwa duniani ifikapo Mwaka 2030 na Tanzania ni nchi mojawapo yenye ugonjwa huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni