Nav bar

Jumanne, 11 Januari 2022

WAFUGAJI WAHIMIZWA KUMILIKI MAENEO YA MALISHO

Na Mbaraka Kambona, Geita

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amewahimiza Wafugaji kuwa na maeneo ya kulishia Mifugo yao jambo ambalo litawapunguzia  migogoro inayowakumba kila uchao.

Waziri Ndaki alitoa wito huo alipokuwa akiongea na Wafugaji wa Vijiji vya Luhembela na Masumbwe vilivyopo Wilayani Mbogwe, Mkoani Geita Disemba 15, 2021.

"Wafugaji tukumbuke kwamba maeneo mengi tunayotumia kuchungia mifugo yetu ni maeneo huria yanayomilikiwa na Serikali, lakini ni vizuri sasa tukaanza kuwa na maeneo yetu na tuyalinde kisheria kwa kuyakatia hati ya kimila au ya kawaida", alisema

Alisema kuwa haiwezekani Mfugaji awe na Ng'ombe 1000 halafu eneo la kuchungia hana, huo ndio mwanzo wa mahangaiko na kuingia katika migogoro na watumiaji wengine wa ardhi hususan Wakulima.

"Sisi Serikali tutawasaidia, maeneo hayo mtakayoyanunua yarasimisheni, yakatieni hati ili yawe ya kwenu, angalau uwe na eneo la kuanzia ili hata unapoiambia Serikali kuhusu malisho una eneo la kwako la kuanzia", alisistiza

Aliongeza kwa kusema kuwa endapo Wafugaji wataendelea kufuga kwa kutegemea maeneo huria wataendelea kuwa katika migogoro na itafika mahala watakosa pa kuchungia na hatimaye watawauza Ng'ombe wote.

Awali, Mfugaji wa Kijiji cha Luhembela, Maisha Magenya alimueleza Waziri Ndaki kuwa Ng'ombe wanao na wanahitaji kuendelea kufuga lakini wanakosa elimu ya namna bora ya ufugaji kwa sababu ya uhaba wa Wataalamu katika Wilaya yao.

"Katika Kata yetu ya Luhembela tuna Mtaalamu mmoja tu ambaye anapata changamoto ya kufikia Wafugaji kulingana na ukubwa wa eneo alilopangiwa kutekeleza majukumu yake", alisema Magenya

Aidha, katika hatua nyingine Waziri Ndaki aliwahimiza Wafugaji hao waanze kujipanga kulima malisho katika maeneo yao kwa ajili ya mifugo huku akiwaeleza kuwa kwa kufanya hivyo kutawasaidia kuondokana na changamoto ya kukosa malisho wakati wa Kiangazi.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Wafugaji  katika Mkutano uliofanyika Wilayani Mbogwe, Mkoani Geita Disemba 15, 2021. Akiongea na Wafugaji hao Mhe. Ndaki aliwahimiza Wafugaji kumiliki maeneo yao ya malisho ili kuondokana na changamoto wanazozipata sasa za migogoro kati yao na watumiaji wengine wa ardhi wakiwemo Wakulima. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa Pili kushoto waliokaa) akimsikiliza Mfugaji, Mabula Kaseba akitoa maoni yake katika Mkutano uliofanyika Wilayani Mbogwe, Mkoani Geita Disemba 15, 2021. Kaseba alimuomba Mhe. Waziri kuwasaidia maeneo ya malisho kwasababu maeneo yaliyopo katika Wilaya hiyo hayatoshi kwa kulishia Mifugo yao. 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni