Ufugaji wa kibiashara unaofanywa na baadhi ya vijana katika Sekta ya mifugo na Uvuvi ni jibu la changamoto ya uhaba wa ajira iliyokumba vijana wengi hapa nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega 15.12.2021 wakati akiongea na Viongozi wa Kituo cha Utafiti Kongwa (TALIRI), Agricultural Sector Support Trust Fund (PASS ) na Kituo cha Ubunifu wa Kilimobiashara ( AIC.) Kwa lengo la kukagua shughuli zinazofanywa na taasisi hizo.
Mhe. Ulega alisema kuwa vijana wengi wakiingia katika kujiajiri kwa kufanya ujasiriamali wa shughuli za Ufugaji ,Kilimo na Uvuvi itakuwa ni jibu kwa tatizo la ajira hapa nchini.
"Vijana wengi baada ya kuhitimu Masomo yao hawakupata ajira na matokeo yake wengi wamebaki wakikaa majumbani kwa wazazi bila shughuli ya kufanya wengine wamekuwa vijiweni bila shughuli ya kufanya kwa vijana kama taifa tegemeo la kesho", alisema
Vijana ambao wameteuliwa kupata mafunzo katika taasisi ya AIC wanaopata mafunzo ya ujasiriamali wa unenepeshaji wa mbuzi watakuwa wamejiajiri na kupunguza pengo la ajira la vijana ambao hawajaajiriwa hapa nchini.
Aidha, aliwataka AIC kupanua wigo wa shughuli ya kunenepesha na kuanza kuchinja na kuuza nyama ya mbuzi yaani usindikaji ili kuongeza thamani ya bei ya Mbuzi.
Aliongeza kwa kuwataka AIC kwa kushirikana na TALIRI kupanua shughuli hizi kwa kuongeza uwekezaji katika kituo cha unenepeshaji na kuchoma nyama kitaalam, kusindika ngozi na shughuli nyingine za kuvutia wananchi wasafiri kupita na kujipatia huduma mbali mbali ikiwemo nyama safi na bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha ubunifu wa Kilimobiashara (AIC), Bw.Tamim Amijee amesema kituo chao kwa kushirikiana na TALIRI, kituo atamizi cha kilimo biashara cha vijana cha PASS-AIC na TALIRI farm, kilianzishwa mwaka 2019 kwa lengo la kuwawezesha vijana katika sekta ya Mifugo na Kilimo kuweza kuanzisha kuendesha na kumiliki biashara binafsi huku wakipata uzoefu na ushuri wa ufugaji wa kisasa.
Mkurugenzi huyo amezungumzia changamoto wanazo kabiliana nazo ni uhaba wa ardhi, mitaji midogo na magonjwa ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo ya kituo hicho.
Hivyo ameiomba serikali kuangalia suala hilo ili vijana wapate mikopo ya riba nafuu na maeneo ya kufanyia kazi ambayo wanamiliki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni